top of page

UNAMUHITAJI MUNGU AKUSAIDIE,KWA SABABU HUWEZI KUJISAIDIA WEWE MWENYEWE!

Na Mch. Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe. 

Kwa ufupi…

“ jisaidie,na Mungu atakusaidia…”  hayo yalikuwa maneno ya mmoja wa kiongozi wangu wa dini aliyekuwa kipofu wa kiroho maana sote tulikuwa katika dini zetu. Yeye alikuwa haoni kiroho maana shetani amepofusha macho yake shauri ya udini maana alikata kuokoka,kwa hiyo yeye ni kiongozi kipofu akiongoza vipofu wenzake wa kiroho ( watu walio gizani,ni vipofu wa kiroho). Sasa,tukiwa kwenye dini zetu ndivyo tulivyofundishwa hivyo,kwamba ujiokoe wewe ndipo na Mungu akuokoe au ujisaidie kwanza wewe ndipo Mungu akusaidie! Ulikuwa ni ujinga tuliokuwa nao,maana haiwezekani kabisa ukajiokoa wewe mwenyewe pasipo Mungu kukuokoa. 

Hakuna awezaye kujiokoa mwenyewe,wala hakuna awezaye kujisaidia mwenyewe. Bali tunaokolewa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu tu. Nilipookoka ndipo nilitambua hili,kisha nikaona kumbe kweli tulikuwa tukipotoshwa nasi tulipotoka kweli kweli kwa mafundisho ya kibinadamu wala hakuwepo Mungu wa kweli. Ili uweze kuokoka,unamuhitaji Mungu katika jina la Yesu Kristo. Tena,ili uweze kusaidiwa unamuhitaji Mungu ndiye akusaidie tu. Inawezekana hata sasa wewe ndivyo unavyofundishwa,ikiwa mtu anakufundisha hivyo,mwambie wazi wazi kwamba“ili upate msaada,unamuhitaji Mungu na huwezi kujisaidia mwenyewe”

Ebu,tuliangalie jambo hili kwa ukaribu katika neno,na tutapata kujua vyema zaidi. Tukianzia kwa Adamu na Hawa,walipofanya dhambi pale bustanini. Maandiko matakatifu yanatueleza hivi;

“ Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.” Mwanzo 3:7

Adamu anatuonesha kawaida ya mwanadamu kutaka kujisaidia mwenyewe pale hasa pale apatapo shida . Adamu na mkewe wanatengeneza nguo kwa majani ya mtini kama sehemu ya kujisaidia wenyewe baada ya kufanya dhambi na kujiona wapo uchi. Lakini wamesahau kwamba yale majani waliyoyachuma na kutengeneza nguo yatakauka na watarudi kuwa uchi vile vile. Hii ikiwa na maana kwamba,walikuwa hawawezi kujisaidia wenyewe kwa namna yoyote ile,isipokuwa Mungu tu ndiye awezaye kuwasaidia.

Ubaya wowote uliomkosa Mungu,huwezi kuuondoa wewe mwenyewe,ila Mungu katika Kristo Yesu ndiye akusaidie. Bila hivyo utaangamia huku ukijiona.Mara nyingi ufanyapo dhambi wewe unakuta ukijificha kwamba usionekane lakini umesahau huwezi kujificha mbele za Mungu. Biblia inasema ,;

“Mimi ni Mungu aliye karibu, asema BWANA, mimi si Mungu aliye mbali.Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema BWANA. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema BWANA.” Yeremia 23:23-24

Ndugu yangu,unaweza ukajiona upo salama kwa sababu unadhani umejificha,lakini ujue upo wazi kwa Mungu. Unaweza ukajificha kwa watu kwa jambo hilo ulilolifanya tena hata ukaamua kukimbilia mbali kwa lengo watu wafanikiwe kabisa kujua. Lakini unajidanganya tu,kwa maana Mungu anajua yote,na kwa sababu unataka kujisaidia wewe mwenyewe,basi ujue Mungu atakuumbua ili ujue Mungu hadhiakiwi. Ni vyema ukarejea kwa Bwana Mungu na kuomba toba,ili sasa Mungu mwenyewe akusaidie sasa. Mtazame Kaini aliyejificha na akamuua ndugu yake Habili,akijua kwamba Mungu hawezi kumuona wala mtu yeyote. Lakini alikuwa akijidanganya tu. Mungu alimuona tangia mbali. Na ndivyo ilivyo hata kwako Mungu anakuona tangia mbali. Unamuhitaji Mungu akusaidie kwa kweli.!!Wewe waonaje,unafikiri ulivyotoka nje ya ndoa yako,na unafikiri ni siri! Ni kweli umemficha mwenzi wako,lakini nataka nikuambie upo wazi sana mbele za Mungu. Na kwa sababu ya uovu huo unaoufanya na kutaka kujisaidia wewe mwenyewe,ujue huna siku nyingi Mungu mwenyewe atakuumbua tu” Huwezi kumdhihaki Mungu hata siku moja.

Adamu angelijua kwamba hawezi kujisaidia kwenye dhambi aliyoifanya,basi angelitubu na kuomba msaada utokao kwa Bwana naye angelisaidiwa. Lakini alijitutumua kutengeneza kwa siri mavazi kwa majani lakini kumbe ndivyo alivyokuwa akijipoteza kabisa! Ikiwa umekwisha fanya dhambi,huna ujanja mwingine bali ni kutubu tu na kuamua kuyaacha hayo yote kisha kuomba msaada utokao kwa Bwana Mungu. Usijifanye mjanja hata mara moja katika eneo hili maana usije ukaangamia! Yafaa kuvunja ukimya na mara moja chukua hatua ya kuomba msaada wa Mungu sasa kupitia watumishi wake.

Huwezi kuficha dhambi,na huwezi kujikwamua kwenye dhambi bila Mungu. Ukija kwa Bwana na kuokoka kwa toba ukimaanisha kuyaacha yote kwa ajili ya Bwana.hapo utaokoka. Waweza kunipigia simu yangu,ili tuombe pamoja muda huu,piga;

Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 655 111149/683 877 900/762 414 446.

Namba ya what’s app ni +255 655 111 149.

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comentários


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page