UNACHOWEKEZA SASA KITAAMUA HATMA YAKO.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 5, 2019
- 4 min read
Updated: Aug 30, 2022

Neno “kuwekeza” ni neno la kibiashara,lenye maana ya “kutumia pesa/mali au nguvu au muda katika kitu fulani kwa lengo la kupata faida” Hata hivyo mwekezaji anaweza kupata hasara ikiwa kama atawekeza bila maarifa mazuri.
Mungu ni mwekezaji.
Mungu ndiye mwekezaji wa kwanza na mkubwa. Yeye amewekeza ndani yetu “karama na vipawa” mbali mbali,akitaraji kuona karama hizo zinakuwa na kuongezeka kiroho na tunazitumia sawa sawa na mapenzi yake. Yeye ni mfano wa mtu atakaye kusafiri,kisha akaweka mali zake kwa watumwa wake;huyu talanta tano,na yule talanta mbili na mwingine talanta moja,kwa kadiri ya uwezo wa kila mmoja ( Mathayo 25:14-29).
Hii ina maana kwamba, kila mmoja aliyeookoka amepewa kitu ndani yake/uwezo wa kiroho ili kusudi aweze kutumika na kuuletea faida ufalme wa Mungu;( Tumepewa talanta tofauti tofauti,kwa kadiri ya uwezo wetu wa kuzalisha).
Sisi pia ni wawekezaji.
Mungu huyo huyo ametupa nafasi ya kuwekeza katika ufalme wake sawa sawa na karama alizoweka kwetu. Wewe ni mwekezaji katika ufalme wa Mungu maana kuna karama iliyopo ndani yako,na ndio maana ametupa mambo manne “ Neema ya wokovu,pesa/mali,nguvu na muda” ili kusudi tuweze kuwekeza vyema katika ufalme wake. Sasa,jiulize Neema ya wokovu uliyopewa unaitumiaje? Mali ulizopewa,umezielekeza hasa wapi? Unazitumiaje? Je kwa ufalme wa Mungu au wa kwako? Ujue pale ambapo umeweka mkazo wa utumiaji wa pesa/mali zako,hapo ndipo hatma yako ipo.
Nguvu zako umeziwekeza hasa wapi? Unazitumiaje nguvu zako? Ujue tena hapo ulipotumia nguvu zako sana,hapo hapo ndipo hatma yako ya maisha ilipo. Lakini muda wako,unautumiaje? Je unautumia kwa ajili ya Bwana au kwa ajili yako,hapo hapo unapotumia muda wako sana,ujue ndipo hatma yako inapoanza. Mfano; mtu aliyewekeza muda wake katika mizaha/kusogoa/masihara basi ujue atakuwa na hatma mbaya ya maisha yake.
Lakini mtu yule aliyewekeza muda wake katika kazi na kulitafakari Neno la Mungu mtu huyo atafananishwa na mti uliopandwa kando kando ya vijito vya maji,uzaao matunda yake kwa majira yake, yaani atakuwa na hatma njema iliyofanikiwa ( Zab.1:1-3).
Hivyo chochote unachowekeza sasa kwa muda au kwa nguvu,au kwa pesa yako ujue kitu hicho kitaamua hatma yako ya baade. Wengi leo wamekuwa hivyo walivyo kwa sababu hawakuwekeza vyema katika maisha yao ya nyuma. Ukichunguza sana jambo hili,utagundua maisha yako kuna mahali ulitakiwa ufike/uwe lakini bado upo pale pale au upo chini sana,na ukiangalia maisha yako ya nyuma utagundua hukutumia vyema muda wako,au nguvu zako,au pesa/mali zako!!! Sasa umejikuta pabaya,lakini hata hivyo,bado kuna nafasi ya kuwekeza tena sasa.
Mimi nilipokuwa kabla ya kuokoka,nakumbuka niliwekeza muda wangu na nguvu zangu kanisani. Ingawa nilikuwa katika dini,sikujua hata wokovu maana yake nini,lakini nilijikuta nikipenda kutumika madhabahuni. Hivyo nikawekeza sana hapo. Huwezi amini,sasa ni mchungaji ambaye nafanya kazi ya madhabahuni. Hii ni sawa na kusema nimelipwa sawa sawa na nilichopanda/nilichowekeza. Hivi,fikiria hapo;kama ningeliwekeza katika uovu,leo hii ningelikuwa wapi?
Mimi sijui,lakini najua jambo moja tu,ningelilipwa lichopanda.!!!
Wana wa kuhani Eli,waliwekeza kwenye uovu mbele za Bwana hali baba yao Eli akijua. Nao wakapokea hatma mbaya ya maisha yao,kwa maana Bwana aliwaadhibu pamoja na nyumba yote ya Eli pamoja naye ( 1 Samweli 2:12-17,3;14). Lakini ipo pia mifano mingi iliyoandikwa kwenye biblia kusudi ikuoneshe kwamba utakachokifanya sasa, utapokea malipo yake baadae,na hatma ya maisha yako yataathiliwa.
Angalia mfano wa Daudi, maana kuna kipindi alilala na mke wa mtu japo ni kwa siri sana Lakini dhambi hiyo ilimgharimu maisha yake ( 2 Samweli 11:2-13,12 yote). Ebu cheki kile alichowekeza hapo,muda mfupi kwa tendo baya la siri lakini malipo yake ni maisha yake. Hata kwako,waweza kufanya jambo fulani kwa siri ikawa unajua wewe tu au ukajua wewe na huyo uliyefanya naye. Lakini ujue kwamba kwa kufanya hivyo,ni sawa na kuwekeza kitu ambacho lazima utavuna,na kitaathili maisha yako ya baadae.
Nini kifanyike?
Ni vyema uwe mwangalifu sana,katika matumizi ya pesa/mali,nguvu na muda wako. Ukijua kwamba utakapotumia chochote kati ya hivyo ni sawa na kujiwekea hakiba ya baadae. Sasa ikiwa umetumia vyema kwa ajili ya Bwana, utavuna mema na utumishi uliotukuka. Lah! Ukitumia vibaya,chamoto kitakufuata hapo baadae.
Mfano kuna watu,wamekosa uaminifu katika ndoa zao,kwa hiyo wanatumia pesa/mali,muda na nguvu kutembea nje ya ndoa zao/wakilala na mtu ambaye si mwanandoa wake. Na hufanya hivyo kwa siri ili mwenzake asijue,lakini wamesahau kwamba Mungu anawaona na anajua kila kitu. Sasa,uzinzi huo wanawekeza,ipo siku watajulikana tu! Na hatma ya maisha yao itakuwa ni mbaya hata itafikia wakati wa kujuta na kusema “kwa nini niliruhusu jambo hili? Kwa nini nimetoka nje ya ndoa yangu? “Yafuatayo yaweza kukusaidia,
Tubu katika yote uliyoyapanda. Ikiwa unashuhudiwa kwamba kuna mambo ya siri,au ya wazi ulipowekeza muda wako kutenda,basi tubu sasa; Kisha weka azimio la kutokurudia tena ubaya huo.
Tumia Neno la Kristo, kujifunza kila siku. Neno ni silaha itakayokupa nguvu ya kutokutamani kurudia uchafu uliofanya mwanzo. Pia MAOMBI ni muhimu sana. Kwa maana maombi yanakwenda pamoja na Neno.
Hata,hivyo nguvu ya kuenenda na Bwana haitoki ndani ya mtu,bali Mungu ndiye chanzo kikubwa. Hivyo kama hujampa Yesu maisha yako,fanya hivyo leo,uokoke kwa kunipigia simu tuombe pamoja sala ya toba.
Kumbuka;
hatma ya maisha yako inaanzia sasa,ni vyema ukajifunza kutumia vyema muda na nguvu zako ili kwamba ufikapo katika uzee wako,uwe na hatma njema.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe.
Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
Whatsapp namba .+255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments