UMETOLEWA MISRI, LAKINI MISRI HAIJAKUTOKA.
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 1, 2018
- 4 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Kwa ufupi ….
Bwana Yesu asifiwe..
Ni mtu wa makamu hivi, ameokoka na kwa kweli anajitahidi kumpenda Mungu. Lakini maskini!!! ni mtumwa wa dhambi, kwa maana kila anapojitahidi kutenda mema hujikuta akitenda mabaya. Unajua si yeye bali ni nguvu itendayo kazi ndani yake, nguvu iliyopo ndani yake inamfanya afanye dhambi ingawa anachukia kufanya dhambi. Huyu ni mfano wa wengi wanaopitia kama yeye. Lakini kwa sababu ana bidii ya kukaza kwa Bwana, basi ni dhahiri atafunguliwa tu. Mimi ninayekuandikia ujumbe huu ninajua ni maumivu kiasi gani ayapatayo mtu wa namna hii kwa sababu hata sisi tulikuwa hivyo hivyo.
Picha tunayoiona kwa haraka haraka kwa mtu wa namna hii ni kwamba “ametolewa Misri, lakini Misri bado imo ndani yake” Yaani ingawa ameokoka Lakini ndani yake bado kuna nguvu ya dhambi.
Lengo mama la fundisho hili siku ya leo ni kukutangazia habari njema kwamba Mwana wa Mungu, Yesu Kristo yupo hai, hata sasa naye amedhihirishwa ili azifunje kazi za ibilisi (1 Yoh. 3:8). Na kuwatangazia mateka uhuru wao na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao ( Isaya 61:1).
Ninaifananisha Misri na utumwa wa dhambi ambao Bwana kwa huruma amekukomboa tena kwa damu ya thamani sana. Lakini bado utumwa huo wa dhambi haujakuacha. Ni kweli umeokoka lakini u mtumwa wa dhambi, ni kweli unajina la lilo hai lakini ni kana kwamba ni mfu. Ni kweli unajulikana umeokoka, lakini ndani ya moyo wako umefungwa kiasi cha kujikuta ukifanya mambo ya ajabu kinyume na wokovu. Inawezekana ukawa ukijitahidi kukimbia utumwa huu lakini hujaona mpenyo bado, mwamini Mungu leo inawezekana ikawa ndio ufumbuzi wako. Mungu anakupenda, hajakuacha amini hivyo. Ninaposema ;
“ utumwa wa dhambi “ ni nini hasa?
ni gereza au kifungo cha kuenenda kinyume na mapenzi ya Mungu kisha kujikuta ukiitumikia dhambi. Kazi kubwa ya shetani kwako ni kukufanya uwe mtumwa wa dhambi hata kama unaichukia. Hivi unajua ; Ni heri kufungwa jera ya kawaida kuliko kufungwa kwenye kifungo cha kuitumikia dhambi! Mfungwa hana uhuru kwa maana hawezi kufanya atakalo bali lile bwana wake atakalo. Na ndio maana Yesu alisema;
“Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.” Yoh.8:34
Ebu tutafakari pamoja maneno hayo ya Bwana, yana maana gani hasa. Awali ya yote fahamu ya kwamba Yesu alikuwa akizungumza na “ Wayahudi waliomwamini ” hii ni sawa na kusema Yesu alikuwa akiongea na watu waliomkubali na watu walioweka imani yao kwake. Ingelikuwa leo, tungelisema Yesu alikuwa akizungumza na baadhi ya wakristo waliomwamini. Ingawa Wayahudi hawa walimwamini lakini bado walikuwa kwenye kifungo cha kuitumikia dhambi. Kumbe waweza kumuamwamini Yesu, Lakini ukawa bado upo kwenye kifungo cha kuitumikia dhambi. Kile kilichokosekana kwa Wayahudi hawa ni “ kuketi kwenye neno ” na ndio maana anawaambia kwamba “ninyi mkikaa kwenye neno langu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli, tena mtaifahamu kweli na hiyo kweli itawaweka huru” Yoh. 8:31-32
Inaonesha wazi kabisa, Wayahudi hawa waliomwamini Yesu, walikuwa mbali na Neno. baba yao alikuwa ni shetani, ingawa walijifanya kumwamini Yesu kwa sababu walikuwa kinyume na Yesu, walitafuta kumuua. Lakini jambo moja tunaloweza kujifunza hapa ni kwamba, “ dhambi ni gereza la utumwa ” Yeyote aliyefungwa na roho za giza, humwasi Mungu, naye ni mtumwa wa dhambi azifanyazo.
Kwa nini U mtumwa wa dhambi ingawa umeokoka?
Leo, kuna mitazamo mingi ya wapendwa kuhusu jambo hili. Wengine husema ukiokoka tu yote yamekwisha, huna sababu ya kufunguliwa maana kitendo cha kuokoka kimeshughulikia mambo yote. Wengine husema ukiokoka ikiwa bado umefungwa unahitajika kufunguliwa ingawa umeokoka. Hiyo ni mitazamo ya watu, lakini vipi biblia inasema nini juu ya jambo hili, na kweli yetu ni Neno (biblia)
Kwenye Matendo 8:12-13,20-24. Ni habari ya Simoni aliyekuwa mchawi. Lakini baada ya kuhubiriwa akaiamini injili na baadae akaokoka, lakini akiwa kwenye imani ndani ya Yesu, tunaona kuna gereza la dhambi ilikuwa bado ikimsumbua hata kutamani kupata fedha kwa karama ya Maombezi. Hii ni dhahiri kwamba ingawa Simoni alikuwa akiaamini lakini bado alikuwa akisumbuliwa na kuhitaji kufunguliwa. Lakini pia tunayasoma maisha ya wana wa Israeli watu waliopendwa na Bwana, kwa huruma ya Bwana akawatoa utumwani Misri. Hivyo walitoka Misri lakini Misri haikutoka ndani yao sababu tunasoma mara nyingi wakitamani kurudi misri wanapokutana na adha. Hii ina maana bado walikuwa watumwa wa dhambi.
Na ndicho kinachosumbua wengi, yaani utakuta ni kweli wamekombolewa kutoka dhambini lakini bado dhambi ipo ndani yao, maana wanawaka tamaa hata sasa!
Kumbe inawezekana mtu kuwa ameokoka Lakini anahitaji kukombolewa / kufunguliwa. Maana kuokoka ni kitu kingine na kufunguliwa ni kitu kingine; ukichanganya mambo haya mawili unaweza ukashangaa kuona aliyeokoka lakini bado ni mzinzi, mlevi, mwongo!!! , n. K hapo ndipo wengine waliochanganyikiwa kwa mambo kama haya, ujikuta wakisema hakuna kuokoka duniani!!! Lakini ukweli ni kwamba kuokoka duniani kupo, lakini ukiwaona wafanyao mambo ya kale, ya aibu na wanayatamani ingawa wameokoka basi ujue Misri haijawatoka ndani yao! Wanahitaji kukombolewa.
Hivyo kwa Waisraeli“kutolewa Misri” kulikusudiwa kuwapa uhuru wa kuabudu na kumtumikia Mungu kama njia kubwa ya kuleta uhusiano mzuri na Mungu. Kitendo hiki kinafananishwa na kuokoka kwa mtu mmoja kutoka utumwani wa dhambi kwa lengo la kurejesha mfano na sura ya Mungu, na kumuabudu Mungu. Kubakia kwa Misri ndani ya Waisraeli ina maana kwamba ndani yao wanayatamani mambo ya kale ingawa wamekwisha tolewa katika mambo hayo. Leo hii kitendo hiki kinaonekana sana kwa watu, kwamba ameokoka lakini ndani yake kuna kiu au shauku ya kutenda dhambi. Hivyo mtu wa namna hii, hawezi kutulia maana ni mtumwa wa dhambi ;shetani ni mwongo sana! Anajua kwamba umemkimbia na mambo yake, anachokifanya kukuletea hisia mbaya za dhambi ili akukamate kwenye dhambi umuache Mungu.
Mimi ninafahamu kwamba inawezekana ukawa umehangaika sana kuacha dhambi fulani na mpaka sasa kwa kweli umeshindwa, ujue unahitaji msaada zaidi, ufunguliwe kwenye gereza hilo. Na usijihukumu maana si wewe utendaye bali roho ya shetani inafanya kazi ndani yako kinyume na mapenzi ya Mungu. Fahamu ya kwamba hakuna awezae kuacha dhambi asipowezeshwa na Roho mtakatifu. Nawe unamuhitaji sana Roho mtakatifu akusaidie kama alivyotusaidia sisi.
Ikiwa umetolewa Misri, basi ni lazima Misri ikuachie leo. Nataka uchukue hatua ya imani ya kunipigia ili tuongee mengi pale ulipokwama pamoja na tuombe pamoja, piga kwa;namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments