top of page

UMEKWAMA KWENYE WIMBI LA MADENI ?

Updated: Sep 30, 2022


fedha yangu hii

Kama hujawahi kujiuliza,emu jiulize sasa,kwa nini wewe ni mtu wa kukopa kila siku,angalia;mwaka jana wote wewe ni mtu wa madeni kila kona na hata sasa bado unaogelea kwenye madeni. Unajisikiaje unapodaiwa?  Au kwa nini ni wewe tu kila mwaka?

Unakopa mpaka unashindwa kulipa kwa maana madeni yamekuwa mengi hujui uanze lipi kulipa na umalize lipi kulipa ! Sasa jiulize hayo maswali muhimu sana kwenye maisha yako.

Jamani kudaiwa ni utumwa mbaya unaoumiza nafsi.


Hakuna maisha mabaya kama kuishi katika wimbi la madeni,kwa maana mtu aishiye kwenye wimbi la madeni hukosa amani siku zote. Inafika wakati mdaiwa hakopesheki tena kwa maana kila maana anadaiwa,je ni nani atakaye mkopa?  Madeni,madeni,madeni ni mabaya sana! 


Leo,watu wengi wanaishi ndani ya wimbi hili la kudaiwa kila kona. Cha kushangaza zaidi hata wapendwa wengi leo wapo ndani ya wimbi hili la kudaiwa daiwa,Utakuta mtu anadaiwa mpaka mtaa wa sita. Na ukimchunguza mtu huyo utagundua madeni yake yameanzia bank au saccos fulani hivi alikopaga kamkopo na hajamaliza kulipa hivyo kila mwisho wa mwezi anatakiwa kwa lazima apeleke makato yao,kwa ajili ya hali hiyo hushindwa kulipa fungu la kumi kiusahihi kwa sababu migawanyo ya madeni ilivyokuwa mingi.


Mtu mwingine utakuta anadaiwa hadi anaamua kubadilisha line ya simu au kubadilisha njia,anadaiwa dukani kwamba alikopa unga wa ugali,anadaiwa ela ya maji aliyochota kwa jilani,anadaiwa na jirani yake hajalipa,tena anadaiwa ela za vikoba ( upatu),hapo hapo bado hajalipa umeme,hajalipa pango,N.K 


Ukifikia hali kama hiyo ni lazima ukae chini kwanza,kisha ujiulize kwa nini unaishi katika mazingira ya utumwa namna hiyo?Je ni kweli huo ni mpango wa Mungu kuishi hivyo? Ukweli ni kwamba huo sio mpango wa Mungu kwako kwamba uishi kwa kukimbia kimbia,bali mpango wa Mungu kwako ni kuishi maisha ya utele,ukopeshe sio kukopa kopa ( Kumb.28:12) na ufanikiwe katika mambo yako yote na afya yako kama roho yako itakavyofanikiwa ( 3 Yoh.:2)


Ni kweli,inawezekana ukawa umeokoka,unampenda Mungu,lakini papo hapo bado unashangaa kwamba unapitia katika wimbi la kudaiwa na kuishi maisha ya utumwa. Ukiona hali kama hiyo basi ujue kwamba madeni ni roho kamili. roho ya madeni inawasumbua wengi leo,na kuwafanya wamuache Mungu wa kweli na wengine hudiliki kuigeukia miungu kwa kufikiri itawasaidia.


Si jambo la kawaida hata kidogo kudaiwa kila kona,kwa maana kuna kipindi ukijiuliza kwa nini ulikopa hujui na wala huna sababu ya kukopa,au kuna kipindi ukijiuliza matumizi ya ule mkopo unajikuta hujui hata hizo pesa umezifanyia nini,na zimeisha!!! Limebaki donda la deni !

Labda tuangalie biblia inasema nini kuhusu kukopa na hali ya madeni. Tusome andiko hili moja 2 Wafalme 4:1“ Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.”


Kupitia andiko hilo,tunamuona mwanamke  huyu mke wa mmoja wa nabii aliyekufa. Kwa lugha nyepesi tungelisema mke wa mtumishi wa Mungu,ambaye huyo mtumishi wa Mungu alikuwa amekufa. Lakini alikufa hali akidaiwa. Kumbuka huyu nabii ingawa alikuwa akimcha Bwana lakini alikuwa akidaiwa deni. Ni kama vile wewe leo,umeokoka lakini bado upo katika mfumo wa kudaiwa madeni na hujui yameanzaje anzaje.


Neno la Mungu limeeleza kuwa madeni ni utumwa,maana mwanamke huyu anasema “; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Kumbe kupitia mfumo wa madeni unasababisha hata watoto wako kuishi katika utumwa.


Leo,zipo familia nyingi ambazo zimeangukia kuishi maisha ya utumwa kwa sababu ya madeni yaliyokopwa na wazazi wao,yamkini wamekwisha kufa kama huyu nabii lakini deni lenyewe halijafa. Na deni hilo limewakamata watoto kuishi katika maisha ya utumwa,wengine wameshtuka wapo utumwani hata mali zao kufilisiwa,labda nyumba au viwanja N.K

ambapo mzazi alikuwa akisumbuliwa na roho ya madeni na akafa hali akidaiwa hata kusababisha kutaifishwa mali zake,na watoto au familia iliyobaki kuishi utumwani.


Biblia imetuambia hapo kwamba,mtu huyo alikufa lakini deni halikufa. Kumbe deni halifagi hata siku moja bali kufa kwa deni ni kulipa tu. Wale watalaamu wa biblia wanajua kwamba roho haifi,madeni ni roho. Bali roho hii inaweza ikaondolewa kwa jina la Yesu Kristo isiwe sehemu yako.


Ukianza kutazama madeni kama roho,itakusaidia kupambana na roho hizo ili zikuacha huru. Huyu mwanamke alikosa tumaini kwa maana kwanza alikubaliana na roho ya deni la mumewe. Kwa sababu alikuwa hana njia ya kujinasua mpaka pale alipokutana na mtu wa Mungu Elisha ambaye alimpa njia ya kulipa deni lake. Biblia haielezi kwamba Elisha aliomba deni lifutike,kwa maana alijua dawa ya deni si kulifuta kimaombi bali kulipa lakini Elisha alishughulika na mzizi wa roho hiyo.


Leo kumezuka imani mbali mbali ziendazo kinyume na neno la Mungu,wakiamini maombi yanaweza kufuta deni au kumfanya anaedai kulisahau deni lake. Kanuni za kiimani zinakutaka ulipe deni,lakini uanze na kushughulikia na mzizi wa roho hiyo,usikope kope.

Kwa njia ya maombi tunaweza kuiondosha roho ya madeni isiwe kwako,na kuomba mbele za Mungu ufanikiwe kulipa madeni yako kisha na kuanza upya na mfumo wa Ki-Mungu.


Kukopa sio dhambi,bali kukopa ni utumwa kwa yule aliyekukopesha. Labda kwa nini watu ukopa? Ukimuona mtu amekopa basi ujue alikuwa na uhitaji wa kitu na hana hicho kitu bsli kipo mahali fulani,hivyo anakihitaji kwa masharti fulani. Hayo masharti ndio utumwa wenyewe kwa sababu ni lazima uyafuate. Mfano kama mashariti yanakudai kulipa kiasi fulani,basi ni lazima utahakikisha unalipa.


Leo, kuna watu wameshindwa kufurahia wokovu kwa sababu ya madeni. Madeni yamewazuia wengine wasiende kanisani kwa sababu kuna watu wanawadai,madeni yamewazuia wengine kubarikiwa kwa maana hawatoi mafungu ya kumi vizuri wamekuwa wakitoa nusu na nusu nyingine inakwenda kulipa deni la mwisho wa mwezi,madeni yamefarakanisha ndugu,N.K 


Kupitia fundisho hili,tujifunze namna ya kushughulikia roho ya madeni na sio madeni kama madeni. roho ya madeni haishughulikiwi ki pesa bali kimaombi na kuzifuata kanuni sahihi za Mungu,bali madeni kama madeni hushughulikiwa na kulipwa tu.

Hakikisha unampokea kwanza Yesu ikiwa kama bado. Na kama ikiwa tayari basi hakikisha unaingia katika toba,ukitubu kwa maana yamkini umeziach njia za Mungu. Kisha omba msaada wa Roho mtakatifu akusaidie uombe ipasavyo.


  1. Vunja kila roho ya madeni iliyopo ndani yako. Kataa kushikiliwa na roho hizo / Jitenge mbali na roho ya madeni.

  2. Muombe Mungu akupe wepesi wa kulipa madeni yako,na uombe uanze upya na Bwana. Hakikisha unapata amani ndani yako.

  3. Lipa deni mara moja,pale upatapo pesa lipa na wala usiangalie kununua kitu kingine kwa maana umeingia agano na Mungu juu ya kufutwa kwa madeni yako. ( Asiye haki hukopa wala halipi,Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.” Zab. 37:21) Uwe mwenye haki,lipa deni zako.


Kumbuka; Unaweza kuishi maisha mazuri bila kudaiwa daiwa. Maana kuna watu wamejijengea maisha ya mikopo kwenye fahamu zao wakiamini kwamba huwezi kuishi bila kudaiwa daiwa,Ok sawa,lakini kudaiwa kwenyewe basi kuwe kwa kawaida hapo afadhali lakini isiwe unadaiwa mpaka unahisi kuchangajikiwa.


Labda inawezekana ukawa ni mmoja kati ya watu wanaosumbuliwa sana na roho hizi za madeni,basi waweza kunipigia kwa namba yangu tuombe pamoja.


Piga sasa; +255 683 877 900.

What’s app number ni +255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page