ULINZI WA KIUNGU ~ 02 (tamati)
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 2, 2019
- 3 min read
Updated: Aug 30, 2022

Kwa ufupi,
…ili ulinzi ukamilike,unahitaji mambo muhimu yahusishwe. Ni kama vile unavyotaka kuendesha gari,basi huna budi kuchukua hatua chache muhimu ili ufanikiwe kuendesha. Katika ulinzi wa kiroho,na wenyewe umebeba mambo muhimu sana kwa ajili ya kuukamilisha,hivyo ulinzi wa kiroho unahitaji;
Silaha.
Bila silaha,ulinzi bado haujakamilika kwa maana silaha ndio egemeo muhimu la ulinzi. Unajua hata kama mtu ni mpambanaji mzuri,lakini akikosa silaha, upambanaji wake ni bure!!! Kwa sababu kuna mahali upambanaji wake hautamsaidia kabisa! Ebu fikiria, mtu wa namna hiyo mwenye miraba minne,kajaza ile mbaya na ni mpambanaji hodari – halafu awekwe getini kulinda mali za mwenye nyumba. Kisha wakatokea wajanja fulani hivi wembamba,lakini wana silaha za kivita.
Hivi hapo ni nani atakayemkimbia mwenzake? Je si yule baunsa mpambanaji atakayekimbia? Je ni nini kinachomkimbiza hali yeye ni hodari wa ngumi? Bila shaka,kinachomkimbiza ni “ zile silaha “ ambazo yeye akiziona tu,ijapokuwa waliobeba silaha hizo ni vijamaa fulani tu,lakini wee! Akiona silaha, hapo ujue habaki mtu!!!
Wataalamu wa utengenezaji wa silaha wanajua mengi. Na moja ya jambo muhimu ambalo huna budi kujua ni juu ya aina za silaha.
Na zipo silaha za aina mbili tu,yaani “ silaha za kujilinda” na “silaha za kushambulia”. Mpiganaji hana budi kuwa na ufahamu kuhusu silaha atakazotumia wakati wa ulinzi/upambanaji wake. Bwana amekufanya wewe uwe mlinzi na mpambanaji katika ulimwengu wa roho.
Ulinzi wa kiungu umejengwa kwenye silaha zote za Mungu / the full armor of God. Silaha za Mungu alizokupa ni kama vile; zile silaha saba zipatikanazo katika kitabu cha Waefeso 6:13-18. ( Kweli viunoni,dirii ya haki,miguu ya utayari,ngao ya imani,chapeo ya wokovu,upanga wa Roho,na maombi). Silaha nyingine muhimu sana ni;
Jina la Yesu ( Yoh.17:12)
Yesu anasema “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.“ Jina la Yesu pekee bila kiambatanishi chochote,ni silaha ya kulinda,pamoja na linaweza kumtunza mtu. Ni muhimu kuelewa neno hili,kwa maana Yesu ameweka mkazo mkubwa katika jina lake, anasema kupitia hilo kuna ulinzi upatikanao. Ikiwa jina la Yesu pekee linaweza kulinda,kutunza – Je kuna haja gani ya kulindwa na mafuta au maji ya upako? Au kwa kutumia viambatanishi vyovyote?
Ukweli ni kwamba katika ulinzi wa kiungu,Bwana ametoa jina lake la Yesu, ili kila amwaminiye alindwe,aokolewe kwa jina hilo. Sarakasi za leo za kutumia mambo kadha wa kadha kwa ajili ya ulinzi ni janja janja tu za watu fulani lakini sio biblia isemavyo. Yesu najua ni ukuu wa namna gani unapatikana ndani ya jina lake,yaani jina tu,latosha kulinda. Kumbuka;Jina la Yesu ni silaha kubwa ya kiroho,
ni dawa tosha ituponyayo bila kudungwa sindano. Laiti kama tungelifahamu vyema jina la Yesu,tusingeliangaika kwa kubeba mambo mengi katika ulinzi wetu. Ni suala la imani tu katika jina la Yesu, basi!. Lakini hata hivyo,ulinzi wa kiungu umebebwa na silaha nyingine muhimu sana nayo ni;
Damu ya Yesu.
Unakumbuka kukombolewa kwa Israeli? Unakumbuka namna ambavyo damu ya Mwana-Kondoo ilivyotumika? Bila shaka, walipaka damu kwenye miimo ya kuta za milango yao,kisha mwaribu hakufanikiwa kuharibu nyumba ya watoto wa Mungu (Kutoka 12:13). Yesu katika agano jipya,Yeye ndiye haswa aliyeandikiwa habari zake,kwamba Yeye ndiye Mwana- Kondoo,aliyekufa kwa ajili yako.
Damu yake,ina nguvu kulinda na kukushindia vita yako. Ikiwa ndivyo,basi damu yake ni silaha kubwa katika ulinzi wa ki-Mungu. Je unaamini hayo?,…Ndio yakupasa uamini ushindi ndani ya damu ya Yesu.
Hata hivyo “ulinzi wa Kiungu ” umekwisha achiliwa kwako. Lakini Mungu anahitaji uamini tu,kisha uchukue hatua chache za kimaombi ukitumia silaha zake katika kupambana kiroho.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe tupate kumtukuza Mungu pamoja na
kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI, piga+255 746 446 446
Whatsapp namba .+255 746 446 446
Mch.G.Madumla
UBARIKIWE.
Comments