top of page

ULINZI WA KIUNGU ~ 01.

Updated: Aug 30, 2022

Kwa ufupi,


Miaka fulani hivi nilikuwa ninafanya kazi kwenye moja ya kampuni hapa hapa Dar- Tanzania. Kipindi hicho,kulikuwa na gharama ya kulaza containers/Makontena na yenyewe ilikuwa ikichajiwa kwa siku. Kwa hiyo kama container italala kwa siku tatu kwenye bandari kavu/Yard,itailazimu kampuni kulipa gharama ya kila siku kwa siku tatu tena sio katika shilingi bali kwa fedha za kigeni/ dollars.


Lakini ulinzi haukuwa tu kwa makontena,bali kwa magari na mali nyingine,ambapo kila mali ililindwa kwa gharama kubwa,walinzi waliajiriwa kulinda ofisi na mali zake, hata magari makubwa yaliyopokuwa safari za mbali,yalihitaji kuwa na uangalizi mkubwa. Ukumbuke kwamba, kila ulinzi unaotolewa,tunazungumzia kuhusu pesa. Ninachotaka uone ni kwamba, ulinzi umebeba gharama kubwa sana! Si jambo jepesi jepesi,bali kuna hali ya kukubali kulipa gharama kubwa ili mali zako zisiibiwe au kupotea!


  1. Kwa nini kuna ulinzi?


01.Kwa sababu ya kuzuia uharibifu uliokithili juu ya mali tulizonazo.


Laiti ingelikuwa sisi sote tungelibakia kwenye asili ya Mungu aliyotuumba nayo,basi ulinzi usingelikuwa na maana. Ebu fikiria, kama kila mmoja wetu angempenda Mungu kwa moyo wake wote,akili zake zote,nguvu zake zote,na kwa roho yake yote,Bila shaka,na jirani yake angempenda tu! Sasa,Je mtu huyo angeliweza kuiba ikiwa anampenda Mungu pamoja na jirani yake? Unamlinzi kumwibia mtu unayempenda?


Au, Angeliweza kuvunja benki,au kunyanganya mali isiyo yake? Bila shaka hakuna mtu angekuwa na time/muda wa mali ya mtu mwingine. Na hatimaye watu wangeliweza hata kulala milango wazi,mageti ya nini? Maana hakuna wezi!!!


Na huko benki-pesa ingewekwa tu wazi wazi,hakuna wa kuiba!!! Lakini kwa sababu ya kutawaliwa na mifumo ya kishetani, imetulazimu kila mmoja alinde mzigo wake. Unajua kuna siku moja nilipanda daladala moja hivi,lilikuwa limeandikwa maneno haya “abiria chunga mzigo wako” hapo nilielewa kwamba hakuna wa kumwamini hata mmoja,kwa maana kila mmoja huwaza ya kwake tu! Hivyo,Ulinzi upo kwa sababu ya kuzuia uharibifu uliokithili katika mali zetu. Yupo mwenye kuharibu,kuiba na ndio maana tunahitaji ulinzi wa hali ya juu.


02. Kwa sababu ya mali tulizonazo zimebeba thamani kubwa,hatupo tayari kuzipoteza.


Mtu akilinda kitu,ujue kitu hicho kina thamani kwake,ndio maana anakilinda. Lakini ni ajabu kulinda kisicho na thamani. Hata hivyo,kuna siku nilishangaa,ebu sikia; – Mtu mmoja alinijia na kuomba msaada kidogo juu ya maombi. Akaniambia yeye ameajiliwa kwenye kampuni moja akashike nafasi ya ulinzi. Anasema,kwenye kampuni hiyo,aliyoajiriwa kama mlinzi haikuwa na mali yoyote kwa maana ofisi yenyewe ilikuwa imevunjwa kitambo tu, na hatimaye kulibakia magofu ya ofisi ya kale.


Naye ndiyo kaajiriwa ayalinde magofu. Hivyo,kulikuwa na uzio wa geti moja,naye huja kila siku kuketi getini kisha huondoka na kumkabizi lindo mlinzi mwingine alinde kwa zamu ya usiku.

Alikuwa haelewi kwa nini analinda magofu ya nyumba iliyobomolewa zamani,maana hakuna mali yoyote iliyoachwa! Hili ni jambo la kushangaza ambalo sikuwahi kuliona kabla!!!Yaani kulinda kitu kisicho na thamani!!! Ni sawa na kulinda hewa usiyoiona!!!Lakini nilipotafakari nikagundua kwamba, lazima kuna kitu cha thamani ndani ya uzio ampapo yeye alindalaye hakukijua!!Kwa maana huwezi kulinda kitu kisichobeba thamani.


Kumbuka “Chochote kinacholindwa kina thamani yake” Ndio maana watu hulinda benki kwa sababu ndani yake kuna thamani ya pesa. Migodi nayo hulindwa kwa sababu kuna vito vya thamani! Na ndivyo ilivyo hata kwako,Mungu anakulinda kwa sababu wewe u wa thamani kwake.


Lakini hata hivyo,ulinzi wa kibinadamu wenyewe una mipaka yake. Kwa maana kuna mambo yasiyowezekana kulindwa kwa silaha za kimwili. Mfano huwezi ukamzuia jini au pepo kwa bunduki,au mkuki wa mlizi aliyekaa getini mwako. Hata kama mlinzi ana bunduki ya kisasa namna gani!,lakini nataka nikuambie jina au pepo likitaka kupita litapita tu! Tena litapita hapo hapo aliposimama mlinzi. Hapo ndipo nikagundua kwamba tunahitaji ulinzi mwingine mkubwa kuliko huo. Biblia inasema;


“ Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.” 1 Petro 1:5


Kumbe! Kuna ulinzi utokao kwa Mungu, kwa njia ya imani…. Najaribu kufikiri kama Mungu angetudai tulipie japo pesa kidogo kwa ajili ya ulinzi wake anaotupa,hivi ni nani angeliweza kulipa gharama hiyo?


Kwa maana tumeona gharama tunazolipa kwa ulinzi wa kawaida jinsi zilivyo kubwa, Je ni kiasi gani ungedaiwa katika ulinzi wa kiungu kama ingepigiwa hesabu? Bila shaka hakuna angesimama na kulipa gharama hiyo. Biblia inasema kuna ulinzi tuupatao kutoka kwa Mungu,na huu huitwa “ulinzi wa kiungu”…


ITAENDELEA…


Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe tupate kumtukuza Mungu pamoja na


kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI, piga kwa +255 683 877 900.

Whatsapp namba .+255 746 446 446


Mch.G.Madumla 2014


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page