UKOMBOZI WA ARDHI.
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 5, 2018
- 4 min read

Mch. Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa kifupi.
Ardhi.
Ni sehemu ya nchi kavu kwenye uso wa dunia (The part of Earth which is not covered by oceans or other bodies of water.)
• Ardhi imeumbwa na Mungu
Mwanzo 1:1 “ Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.“. Neno “ nchi” kwenye biblia hutafsiriwa kuwa “ardhi”. Andiko hili linakuonesha / kukufundisha kwamba “ardhi nayo,imeumbwa” Hivyo unapoitazama ardhi leo,uitazame kama mali iliyoumbwa na Mungu.
• Kwenye ardhi,Mungu alifanyiza ;
Mimea ( Mwanzo 1:11),Wanyama wa kila aina ( Mwanzo 1:24),mwanadamu naye ni matokeo ya ardhi ( Mwanzo 2:7),. Ardhi imesheheni mali nyingi za Mungu ( Zab.104:24). Ukihitaji dhahabu,chuma,na vito vya thamani basi huna budi kuvitafuta ardhini. Hivyo utajiri umefichwa kwenye ardhi.
• Mungu ndiye mmiliki wa ardhi. “
“ Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA,Dunia na wote wakaao ndani yake. ” Zab.24:1. Kwa kuwa ardhi imeumbwa na Mungu, basi Yeye ndiye mmiliki wa hiyo ardhi. Tambua leo kwamba “ardhi” ni mali ya Mungu,ili kama ukitaka kumiliki ardhi basi ujue ni lazima umwombe mwenye nayo mbaye ni Mungu. Hapo mwanzo,Bwana Mungu aliwaambia watu wake kwamba “nchi haitauzwa kabisa,kwani ni yangu mimi…” Walawi 25:23 ,ili kuwapa mipaka,na waweze kujua ardhi ni ya Mungu.
• Bwana Mungu anaipenda ardhi. Zab.33:5
“ nchi imejaa fadhili za Bwana ” hii ni sawa na kusema nchi imejaa pendo la Bwana. Kumbuka hili; ikiwa kila alichokiumba Mungu alikiona ni chema,ardhi na yenyewe aliiona ni njema. Na akaipenda. Fahamu pia ; Bwana Mungu hakuumba chochote pamoja na uharibufu. Bali vyote vilikuwa ni vizuri na vyema.
Mwanadamu na ardhi.
Mwanadamu amemilikishwa ardhi
“ Mbingu ni mbingu za BWANA,Bali nchi amewapa wanadamu. ” Zab.115:16.
Swali ; kwa nini nchi / ardhi amepewa mwanadamu? . Bila shaka Bwana Mungu ametupa ardhi ili tuitawale kwa kuilima na kuitunza. Ni mapenzi ya Mungu sisi wanadamu tumwishie Yeye kwenye ardhi, pia tukiwa kwenye ardhi tuwe na maisha y utajiri kwa umaskini wake Kristo Yesu ( kwa sababu utajiri kwenye ardhi, na Bwana anataka tuishi kwenye huo utajiri katika Kristo Yesu).
Hata hivyo,shida iliingia ulimwenguni. Mwanadamu akaishi kwenye laana badala ya baraka.
Ufunuo 12:7-12 – inatueleza juu ya vita vilivyopiganwa kati ya lile joka la zamani,ibilisi ,shetani na malaika wa Mungu. Joka shetani akapigwa na kutupwa chini ( hata nchi) . Sasa tunaona jinsi gani shetani ameshushwa kwenye ardhi ambayo ilikuwa na mibaraka kibao. Kumbuka hili “ shetani alitupwa bila kunyanganywa nguvu zake,lakini alishindwa kwa Neno la ushuhuda na damu ya Mwana-kondoo”
• Matokeo ya dhambi ya Adamu na Hawa ni kulaaniwa kwa ardhi.
“Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Mwanzo 3:17-19
Ni jambo la ajabu hilo,kwa sababu aliyefanya dhambi ni Adamu lakini ardhi ikalaaniwa kwa kosa la Adamu. Unaona hilo lakini??? Yaani swali la kujiiuliza ni kwamba ; “kwa nini ardhi ilaaniwe ikiwa aliyekosa ni Adamu? ” Ukweli ni kwamba, kulaaniwa kwa ardhi, ni kulaaniwa kwa Adamu kwa sababu maisha ya Adamu yalitegemea ardhi kama uti wake wa mgongo wa maisha ya kila siku.
Dhambi moja ilisababisha laani kubwa kwenye ardhi. Neno hili linakufundisha leo,kwamba sababu moja kubwa ya laana ya ardhi ni “dhambi” kama ilivyo kwa Adamu na Hawa. Ebu fikiri zaidi juu ya hilo,alafu leta picha hiyo mahali uishipo leo. Je hukukuwa na dhambi yoyote iliyofanywa hapo uishipo? Ikiwa umejenga au umepanga;
Jiulize tena ;
“ Je una uhakika gani na hiyo ardhi unayoishi juu yake? Je haikupokea damu kama damu ya Abili yule mwenye haki? Je hapo hakuna uovu uliofanywa kabla yako? Ukijiuliza hivyo,utagundua lazima uovu ulikuwepo hapo kwanza. Na sasa unachukua hatua gani?
• Matokeo ya ardhi iliyobeba laana;
Kuzaa mapooza ( 2 Wafalme 2:18-22). Ardhi isiyozalisha.
Kuzaa michongoma na miiba ( Mwanzo 3:18). Kizalisha kwa shida sana. Au kutembea kwenye ukaufu wa hali ya juu. Kama ndio umejenga basi unajikuta unaishi kwenye ufukara wa kupindukia.
Kukosa kibali katika kile ukifanyacho kwenye hiyo ardhi. N.K
Nini cha kufanya?
01. Toba
Ikiwa ardhi imepokea laana,huna namna ya kuiombea kwanza ni kuiombea toba. Kawaida ya ardhi inasikia na inakinywa. Ebu tazama nini Bwana alisema baada ya Kaini kumwua ndugu yake huko uwandani,biblia inasema
“ Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; “ Mwanzo 4:11
Ardhi inamiliki kinywa,na ndio maana pia inauwezo wa kusikia inaponenewa. Ardhi ina uwezo wa kutunza kumbukumbu na ndio maana ardhi inapolaaniwa utuza na kubeba laana hiyo. Ni mambo ya ajabu san haya. Hivyo,ardhi inahitaji toba,Bwana aweze kuihurumia.
02. Damu ya Yesu,itakayofuta laana hizo.
Damu ya Yesu ina nena mema kuliko damu ya Habili. Kama kutakuwa n chukizo lililofanyika hapo ardhini,iitia damu ya Yesu. Shughulika ipatasavyo kumwaga damu ya Yesu ili kusudi kila laana ifutwe kwa damu. Kumbuka namna ambavyo adui shetani alivyoshughulikiwa na damu ya Mwana- kondoo ( Ufunuo 12:11).
03. Ni vyema awepo mchungaji hapo kwenye hilo zoezi.
Si lazima hata kidogo,lakini inapendeza awepo mchungaji hapo kukusaidia zaidi. Kwa maana wawili ni wawili. Kuna wakati mwingine unaweza usione vyote,lakini mtu wa Mungu akakusaidia kuon na kuombea ardhi ya nyumbani kwako / kwenu.
Ikiwa fundisho hili limekubariki na umejifunza kitu,basi nifahamishe . Pia ikiwa unahitaji MAOMBEZI PIGA kwa namba zangu + 255 683 877 900
WhatsApp ni +255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments