UKIFANYA HIVI, UTAJIZUILIA BARAKA ZAKO BURE !!!
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 25, 2018
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Kuna na mambo mengi tunayoyafanya yanayozuia Baraka zetu. Wakati mwingine tunafanya kwa kujua na wakati mwingine kwa kutokujua, lakini baadae tunaona matokeo yake, badala ya kubarikiwa tunalaaniwa, au tunabakia bila baraka. Nimesema yapo mambo mengi tuyafanyayo, lakini ni vyema nikuambie moja ya jambo ambalo linaweza kukuzuilia kubarikiwa kwako ni pale utakapokosa “ moyo wa ukarimu “. Moyo wa ukarimu ni moyo wa kujali hasa wageni (ni namna ile aliyokuwanayo mtu ya kuwaangalia na kuwahudumia watu hasa wageni). Ingawa fundisho hili sio fundisho la “ moyo wa ukarimu ” lakini nimeliona hili limekuwa ni moja ya chanzo kikubwa cha kuwanyima Baraka za Bwana kwa wale wanaoshindwa kuwa wakarimu. Nataka tumchukue Yakobo kama case atudy yetu leo. Kuna picha fulani naiona ya ukarimu uliokosekana ndani ya Labani pale ambapo Yakobo alipotaka kutoka kwa Labani.
Yakobo alikuwa ni mgeni katika nyumba ya Labani, na ndivyo ilivyo unaweza ukapata mgeni kwenye nyumba yako, huyo mgeni yamkini anaweza akawa mgeni mwenye busara, au anaweza akawa mgeni msimbufu. Vile vile unaweza ukapokea mgeni kazini kwako, labda mgeni huyo msimbufu au mzuri. Ujue kwa kupitia mgeni huyo waweza kubarikiwa au kukosa baraka kwa kadri utakavyomkirimia. Labda tuchukulie mgeni huyo aliyekujia ni msumbufu yaani hajatulia tulia, sasa kwa jinsi utakavyoweza kumchukulia kwa muda fulani tu, maana mgeni ni mtu wa kupita hata kama atakaa mwaka mzima lakini, ni lazima itafika wakati ataondoka.
Ukiweza kuonesha ukarimu wako, ujue inawezekana kupitia huyo ndio ikawa daraja lako la kupokelea majibu yako. Wewe hujawahi kuona mtu aliyetembelewa na mgeni ambaye ni ndugu yake. Tena mgeni huyo ni ameshindikanika kwao sasa kaja kwa ndugu yake ajifichie hapo. Na kwa sababu ya ukarimu wa ndugu yake, ukamfanya akazane kwenye maombi, kumwombea mgeni kwamba Mungu ambadilishe. Na kwa kitendo hicho cha kuongeza bidii kwa Mungu, huyo ndugu anajikuta, kwanza mambo yake ndio yanafunguliwa lakini pia mgeni wake kupokea uponyaji. Sasa angalia hapo, ni nani aliyemsukuma ndugu kuomba kwa kumaanisha? Jibu ; ni mgeni aliyemjia chini ya nyumba yake, ingawa alikuwa ameshindikanika, lakini kwa sababu hiyo hiyo ya usumbufu wake ndio ikawa ni daraja la kutokea kwa ndugu mwenye nyumba. Ebu tulitazame jambo hili kibiblia linasemaje;
“ Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote.Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.” Mwanzo 31:1-2
Yakobo alikuwa ni mbarikiwa, mwenye neema. Alipokuwa akimtumikia Labani, alisababisha mifungo pamoja na mali ya Labani kuongezeka. Lakini kwa bidii alimtumikia Labani kwa miaka 20 ( miaka 7 kwa kumpata Lea, miaka 7 tena kwa kumpata Raheli na miaka 6 kwa wanyama wa Labani) Mwanzo 31:41. Haikuwa kazi rahisi, bali alijitoa sana lakini kwa neema akafanikiwa kumaliza kazi ya utumishi. Sasa alipomtangazia mjomba wake Labani kwamba anataka kuondoka, ndipo hapo watoto wake Labani wakaanza kumuonea wivu kwa sababu sasa Yakobo amekuwa na utajiri mwingi uliotokana na baba yao Labani.
Labani hakumfanyia ukarimu tena, bali alimtazama vibaya. Watoto wa Labani wakapoteza ukarimu ( watoto hawa walikuwa ni wa kiume ukiwaondoa Lea na Raheli) . Labani mtu mzima akamchukia Yakobo ambaye alikuwa ni mgeni wake, sasa mwenye mali nyingi na ameoa binti zake wawili Raheli na Lea. Ebu angalia hapo vizuri, Labani laiti angekuwa na ukarimu mzuri kwa Yakobo ambaye amebarikiwa na yeye Labani angebarikiwa tu kwa sababu kule namna ya kujiambatanisha vizuri na mbarikiwa naye angekuwa ni sehemu ya baraka. Lakini hakulitambua hilo, badala yake akaingiwa na wivu, uchungu hata kukosa baraka zake kutoka kwa mgeni wake Yakobo.
Sasa, vuta picha hiyo hiyo, kisha ilete kwenye maisha yetu halisi. Na ujiulize; ni mara ngapi watu wamewasukumia mbali wageni wao, wakati mwingine ni kwa sababu ya wivu tu? Ni mara ngapi watu wamewakataa wageni kwa sababu zao wenyewe zisizokuwa na kichwa wala mguu? Jiulize, je kwa kufanya hivyo hawakupishana na mibaraka yao? Wewe, ni mara ngapi hutaki kuwapokea wageni na kuwakarimu,? Je hujui hao wanaweza wakawa kama akina Yakobo? Ndio, wanaweza wakawa kama akina Yakobo kwako. Mara fulani Yesu aliwaambia wanafunzi wake Kwa habari ya kuwatendea vyema wageni ambao ni wahitaji, akasema “ Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. ” Mathayo 25:31-40.
Inaonekana wana wa kiume wa Labani walimnungunikia baba yao, hata Labani baada ya kuyafikiri hayo, uchungu ukamjaa na kuanza kumtazama vibaya mgeni wake Yakobo, kama ukisoma kwa utulivu hiyo mistari miwili tuliyoisoma ( Mwanzo 31:1-2), utagundua hilo. Ndipo nami naliona balaa hili katika siku za leo. Kwamba watoto wako wanaweza wakakujaza maneno mabaya juu ya mgeni aliyekuja kwako, kisha ukayachukua hayo maneno bila hata ya kutafakari kisha ukaanza kumuhukumu mgeni wako na ukifanya hivi, ujue utakosa baraka zako alizokujanazo huyo mgeni. Wakati mwingine mumeo anaweza akakujaza maneno yasio ya kweli, alafu ukaenda moja kwa moja kumfukuza mgeni na hapo ukakosa baraka zako. Kumbe mgeni huyo alikujia ili Mungu kupitia huyo akufungue maeneo fulani. Si vyema kuwanyanyasa au kuchukulia vibaya wageni.
Kwa msaada zaidi wa maombi, na mengineyo waweza kuwasiliana nami kwa namba zangu zilizopo hapo juu.
Namba ni +255 683 877 900
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments