UAMINIFU KATIKA NDOA ~ 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 9, 2020
- 5 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Kinyume cha uaminifu katika ndao ni usaliti! Na usaliti ndio sumu kubwa ya kuimaliza ndoa. Maumivu ya usaliti ni makali mno kiasi cha kutamani kufa. Ni mara mia ukosewe na makosa mengine kuliko umpendaye akusaliti maana machozi ya usaliti ni mazito yasiyokauka haraka! Hivyo dawa pekee ya kulinda ndoa yako ni uaminifu. Wakati mwingine ninaufananisha uaminifu ni sawa na “kufumba macho” dhidi ya kile kinachoweza kukuangusha! Ni kwa namna gani kufumba macho kunafanana na uaminifu/mwaminifu?
Ni kwa sababu hii; kukosa uaminifu ni matokeo ya kutamani ambapo huanzia kwa macho,ikiwa cha kutamanika kikipita mbele yako hali wewe hukioni kwa sababu umefumba macho,basi ujue huwezi kukitamani wala kuwa na shughuli nacho! Ikiwa mwanandoa ambaye macho yake ya kawaida kabisa hayaoni tamaa ya aina yoyote ile basi ujue atakuwa salama tu. Biblia inaeleza kisa cha na chanzo cha mwana ndoa “ Hawa ” mke wa Adamu,jinsi alivyoanguka dhambini. “ Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” Mwanzo 3:6
Macho ya mwanamke huyu yalikuwa wazi,alipoona mti wafaa kwa chakula akauchuma. Lakini ukumbuke mti huo ulikuwa hapo siku zote,kwa nini asingelichuma tunda hilo siku zote hata siku hiyo? Adui ibilisi alicheza na fikra za mwanamke kupita “macho” yake,akamjaza matamanio, hatimaye akaupotosha na moyo wake. Msamiati wa kufumba macho ni hali ya kupotezea unachokiona,ama ni hali ya kujifanya mjinga kwa kile ukionacho hali ukijua madhara ya hicho ukionacho. Fikiria yule apitaye machoni pako,au yule unayemsikia,ukampotezea/ukaona si kitu/ukafumba macho,je utaangukaje dhambini hata kupoteza uaminifu? Ukweli ni kwamba mwili hutamani ukidanganywa na macho yaonayo.
Hakuna msingi ulio imara na wenye nguvu wa kuijenga ndoa imara kama “uaminifu“, kwa maana uaminifu ni msingi na ndio uchochea penzi. Wala hakuna uhusiano mzuri ikiwa hakuna uaminifu,hivyo utagundua “uaminifu ” ndio kila kitu kwenye ndoa. Uaminifu ni hali ya kujizuia kufanya kisichotakiwa kufanyika. Uaminifu pia ni pale mtu anapokuwa na imani kwa Mungu,akijitunza njia zake asije akakosa ( Zab.39:1). Uaminifu ni zaidi ya tendo la ndoa,ni zaidi ya maneno mazuri ya kimapenzi.
Uaminifu unaanzia wapi?
Kawaida Uaminifu asili yake ni Mungu,kwa maana Yeye ndiye haswa mwaminifu wa waaminifu (Warumi 3:3). Hivyo kama uaminifu umetokana na Mungu basi ni dhahiri ili mtu awe mwaminifu hana budi atokane na Mungu. Hii ikiwa ina maana mtu mwaminifu huzaliwa mara ya pili/kuokoka. Lakini ni vyema ukajiuliza kwamba,mbona hata waliookoka wengi tu si waaminifu? Ni kweli kabisa,kwamba idadi kubwa ya watu waliokosa uaminifu kwa sasa inaonekana ni kutoka kanisani??? Ukweli huu unaeleza kwamba wakristo waliookoka wamemwacha Bwana. Kwa hiyo ingawa wamwokoka lakini bado si waaminifu, wana mambo yao binafsi.
01.Uaminifu unanzia kwako!
Ukitaka mwenzako awe mwaminifu basi anza wewe kumwonesha uaminifu wako. Maana mabadiliko yanaanzia na wewe mwenyewe! Mwalimu mzuri ni yule anayefundisha kile anachokiishi,na ndivyo ilivyo katika suala la uaminifu katika ndoa yako unaanzia na wewe mwenyewe. Maana huwezi kumsisitiza hata mtoto wako kwamba awe mwaminifu asiibe sukari ya kulamba ikiwa wewe mwenyewe unalambaga! Kwa watoto wa kizazi hiki cha doti kom! Watakwambia wazi tu,kwamba “ mbona na wewe unalambaga lakini?!!! ” na ndio maana Yesu alisema kwamba “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?“ Mathayo 7:3
02.Uaminifu ni motokeo ya kuwa na hofu ya Mungu./ Hofu ya Mungu husababisha uaminifu.
Ikiwa hakuna hofu ya Mungu, mtu hawezi kujizui kwa chochote. Ndani ya ndoa,- kama hakuna hofu ya Mungu, mwanandoa atachepuka,ama atafanya yoyote anayoyajua. Kumbuka;hofu ya Mungu ni zao la kuokoka na kudumu katika Neno ukilitafakari pamoja na maombi. Ukichunguza Watu wengi waliokosa uaminifu utagundua kwamba hawako sawa na Mungu/hawana mausiano mazuri na Mungu. Hata waliookoka ikiwa kama wokovu wao ni vugu vugu basi ujue hawawezi kuwa waaminifu kwa sababu hakuna vugu vugu kwa mtu mwenye hofu ya Mungu. Na kukosa hofu ya Mungu ndio sababu kubwa na pekee yenye nguvu ya kumfanya mwanandoa kukosa uaminifu. Wewe cheki tu kwa manandoa aliyembali na Mungu, angalia kiwango chake cha uaminifu katika ndoa yake,ndipo utagundua hiki nisemacho hapa.
Nini kinachosababisha kukosa uaminifu katika ndoa?
Kama ilivyotangulia kueleza,sababu kubwa ni kukosa hofu ya Mungu/ kuwa mbali na uhusiano na Mungu. Lakini sababu nyingine ndogo ndogo ni kama vile;
01. Mtazamo usiofaa.
Wana ndoa wengi wamegubikwa na mitazamo mibaya isiyofaa kabisa katika ndoa zao wengine hali wameokoka. Kwa maana wapo watu katika ndoa huona hawaridhishwi/hawafikishwi sawa sawa. Hivyo watu wa namna hii uwa na mtazamo wa kutoka nje ya ndoa wakitafuta kuridhishwa/kufikishwa. Lakini ukweli ni kwamba hata wakitoka nje bado hawawezi kupata wanachokitafuta kwa maana yule wa ndani ndio bora kuliko wa nje. Ukichunguza kwa makini jambo hili,utagundua shetani yupo hapo akihusika lakini pia mtazamo wa mtu unachangia sana. Wengine hufikiria kwamba wa nje ni watamu kuliko wa ndani,lakini Je ni kweli? Lah! hata kidogo,ni mtazamo mbaya tu!!!
02. Elimu isiyofaa na marafiki waovu pamoja na mila potofu.
Kuna baadhi ya wanandoa wameingia kwenye ndoa zao na elimu mbaya ya kuhusu ndoa. Kwa mfano,wadada/wanawake ambao wamefundishwa maadili na mafundisho yasiyo na maana kwenye baadhi ya kitchen party za wahuni. Ama wakaka waliopatiwa elimu ya ndoa na baadhi ya wazee wahuni tu ambao husema “ huwezi kupika kwa figa moja” ( yaani huwezi kulidhishwa na mtu mmoja huyo wa ndani tu). Pia rafiki waovu wana mchango wao wa kupotosha uaminifu ndani ya mwana ndoa.
03. Ibilisi na utandawazi.
Ibilisi huchochea tamaa kama ile ya Adamu na Hawa kutamani kula tunda walioagizwa wasile. Pia leo,utandawazi umewafanya wana ndoa kujifunza mapenzi kwa kuangalia maigizo,filamu na michezo. Mengi yanayotoka huko magharibi hayana Mungu isipokuwa yamejawa na ushetani. Ebu fikiria mapenzi yalivyogeuzwa geuzwa,na bahati mbaya wanandoa hujifunzia humo. Mfano mdogo tu,utakuta mwana ndoa aliyeokoka akihitaji ashiriki tendo la ndoa kwa mikao ya ajabu ajabu na mwenzi wake. Sasa anapogundua mwenzi wake hataweza kumfanyia hivyo,hapo ndipo huangalia nje ambapo atamtafuta atakaye mfanyia hayo aliyoyaona kwenye mtandao.
Wakati mwingine kupitia utandawazi,wana ndoa hupoteza uaminifu ndani ya ndoa zao kwa kujifunza wizi wa kimapenzi. Utakuta kabla ya kujikita kwenye mitandao wana ndoa walikuwa hawana haja ya kuchepuka,lakini kwa sababu ya mtandao unaoonesha mbinu za kuchepuka kwa siri,kisha kurudi “kinyemela ” ndani ya ndoa na mwenzi wake asijue,basi hapo ndipo mwana ndoa atatumia mbinu zote ajifunze.
04. Majini zinaa / majini mahaba.
Kuna wana ndoa wengi leo wanaotembelewa na majini mahaba kwenye ndoa zao. Wakishiriki tendo la ndoa na roho zilizovaa uhusika wa kiume ama za kike kisha kuwaingilia wana ndoa. Ikitokea hivi,basi ujue ndoa hiyo haiwezi kuwa na amani,yaani wana ndoa hao hawawezi kufurahiana katika tendo la ndoa kwa sababu ipo roho inayomwingilia mmoja wao ( ama wote wakati mwingine). Hapo jina mahaba anapokuwa kwa mmoja basi huyo mwingine ni rahisi kukosa uaminifu kwa mwenzake. Kwa maana anaweza akatoa nje ya ndoa yake,ama la! Anaweza akakosa uaminifu tu kwenye eneo lolote la ndoa yake.
05) vifungo kutoka katika roho chafu.
Wapo watu katika ndoa zao wamefungwa kabisa hata wamejikuta wanayoyafanya wao wenyewe hawayaelewi! Wengine ni roho za kurithi kutoka wa waliowatangulia. Watu wa namna hii,hawawezi kutulia kwenye ndoa zao, uaminifu haupo kwao. Hata kama wakiolewa / kuoa hawawezi kutulia mpaka uwe mzinzi na hata hapo hatulii. Watu wa namna hii kweli wanaweza wakajitahidi kutulia kwa akili zao,lakini baada ya muda mfupi tu,wanarejea pale pale pabaya…
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Na kwa huduma ya MAOMBI ushauri na msaada zaidi,piga sasa +255 655 111 149/683 877 900/762 414 446
What’s app namba +255 655 111 149.
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments