UCHUMBA ~ 02.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 24, 2019
- 4 min read

Shalom…
Kwa ufupi.
Uchumba wa Mariamu na Yusufu ( Mathayo 1:18)
Mariamu alikuwa ameposwa na Yusufu. Mariamu alikuwa ni binti mdogo ( labda alikuwa kati ya umri kuanzia miaka 12 -17). Biblia inaweka mkazo wa usafi wake kwamba alikuwa bikira, yaani hakumjua mume, kuonesha alikuwa ametulia. Lakini hata hivyo Mariamu alipata neema kati ya wanawake wote wa kipindi kile kwa kubeba mimba ya Yesu, haikuwa ni jambo la kawaida. Kuna mambo muhimu ya kujifunza kupitia Mariamu mama yake Yesu katika kipindi alichoposwa na Yusufu.
01.Alisubili ndoa / alikuwa bikira (Luka 1:27)
Ingawa Mariamu alikuwa ameposwa na Yusufu lakini bado alikuwa bikira yaani hakulala na Yusufu wala mwanaume yeyote katika uchumba wake. Jambo hili ni kubwa la kujifunza hasa unapokuwa na mchumba ukitarajia ndoa, kumbe inawezekana kwa mtu mwenye mchumba na kisha asimguse mpaka ndoa ifungwe. Lakini Je ni wangapi wanagusana kabla ya ndoa??? Kama Mariamu mtu wa mfano katika wadada aliweza basi kila binti / dada anapaswa kuweza kutulia thamani tuli bila kutembea kabla ya ndoa. Lakini Yusufu naye akiwakilisha wakaka, mtu ambaye ni mfano mzuri, aliyejiepusha kutembea na mchumba wake kabla ya ndoa na akafanikiwa, basi na wakaka/mkaka anaweza asitembee na mchumba wake kabla ya ndoa.
Usiseme leo haiwezekani!!!! Ni wewe tu ndio huwezi, kwa maana wapo wanaoweza! Na ikiwa wapo wawezao kwa nini wewe usiweze??? Fikiria wewe ambaye leo upo kwenye ndoa, vipi kama usingekuwa kwenye ndoa ungeliweza kutomgusa mpezi wako mpaka ndoa? Bila shaka unaweza. Ni kujilegeza tu, na kujiona hauwezi lakini inawezekana kuishi bila mapenzi hususani ikiwa upo katika uchumba. Shida ipo wapi? Kwa nini mchumba una haraka namna hivyo, kwani huyo si wako? Tena bado kitambo kidogo tu mtafunga ndoa, kuna haja gani ufunge ndoa na umeharibu usichana/uvulana wako?
02. Yusufu alikuwa mtu wa haki. (Mathayo 1:19)
Biblia inaeleza sifa ya kijana Yusufu aliyemchumbia Mariamu, ya kwamba alikuwa ni mtu wa haki. Nini maana ya kuwa “mtu wa haki“, kuwa mtu wa haki ina maana ni hali ya kuhesabiwa haki isiyotokana na matendo bali imani ( to be righteous is to be justified by faith / Justification is to be declared righteous). Hivyo Yusufu mtu alikuwa mwamini, leo hii tungelimwita “ Yusufu ni mtu aliyeokoka” Hivyo, Mariamu alichumbiwa/aliposwa na mlokole sio mpagani, wala sio mwanaume aliyekataa kuokoka! Yusufu kama kijana aliyeokoka anaweza kuwakilisha kijana wa kiume wa leo aliyeokoka.
Sasa kijana anayekuchumbia leo, vipi kaokoka? Au unaimani kama baadhi ya wadada wa mjini wanavyoamini kwamba wanaweza kumbadilisha mume kwa maombi wanapoingia kwenye ndoa!! ??? Ni ngumu kama nini uolewe na kijana mpagani alafu uwe na mtazamo wa kumbadilisha aje kuamini mkiwa ndani ya ndoa, kwa maana wengi waliojaribu kufanya hivi walijikuta wao ndio wanabadilishwa imani zao.
Lakini biblia inaeleza pia kwamba “ Yusufu hakutaka kumwaibisha Mariamu ” na kwa sababu hiyo aliazimu kumwacha kwa siri. Bila shaka kwa sababu yeye Yusufu alikuwa mtu wa haki na amethibitisha kuwa mchumba wake ana mimba. Hali hii ikamsumbua hata kutaka kumwacha ili asiaibike. Lakini malaika wa Bwana akamtoa wasiwasi kwamba asimwache bali amchukue mkewe maana mimba hiyo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Kile ambacho malaika wa Bwana alichokitaka kwa Yusufu ni kutokuachana kwa sababu ya mimba kwa maana ni Roho mtakatifu. Bila shaka Bwana anachukia kuachana,mimi ninafahamu kwamba hata kama mimba isingelikuwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu bado Roho mtakatifu asingelidhia kuachana.
Leo hii, ingiwa umetenda dhambi, ukalala na mchumba wako, ujue hiyo ni dhambi kama ilivyo dhambi ingine. Na kulala kwenu ukashtukia mchumba wako ana mimba. Hapo ujue hutakiwi kuitoa mimba wala kumwacha kwa maana mtoto huyo ndani ya tumbo hana kosa lolote bali kosa ni la kwako na huyo binti. Ni vyema ukakubali kulea mimba na hatimaye mchumba wako ajifungue kwa maana umevuna ulichokipanda, na hakuna haja ya kukimbia ujauzito wako.
Tazama neno hili;“Yusufu hakutaka kumwaibisha Mariamu ” ndani yake Yusufu alimthamini sana Mariamu hata hakutaka jamii imdharau. Ebu jiulize mtu uliyempata yupoje? Je ni mtu anayetaka uaibike? Je anajali kiasi gani? Hivi unajua kama mchumba wako hawezi kukujali sasa basi hata baadae hataweza kukujali! 😝😝😝 Waswahili wanasema “ nyota njema huonekana asubuhi!!! Ebu jiulize tena, unapopata shida mchumba wako anajali kiasi gani? Je yupo tayari kukukingia kifua ili usiaibike?
Fikiria; ikiwa mchumba wako hajali wazazi wako hali bado hamjaoana, tena mtu yoyote kutoka kwenu, hajali wadogo zako lakini anajifanya kukujali wewe! Au fikiria; mchumba wako anaweza kukujibu vibaya pale unapotaja ndugu zako ukiwa naye! Ujue mtu wa namna hii, sio sahihi kwako, na ni vyema uchukue tahadhari mapema;ikiwa kama ndio hajafanya taratibu za uchumba ni bora umwache mapema, kwa maana atakusumbua sana kwenye ndoa yako.
Tena ukiona mchumba wako anakutaka kimwili tena amekuwa akikusisitiza jambo hilo, ujue huyo sio mtu sahihi au kama ni mtu sahihi basi ana mapepo na lazima kwanza mapepo hayo yatoke ndipo mwendelee na uchumba hatimaye ndoa, la sivyo atakuletea watoto wengine wa nje. Atakusumbua baadae. Sasa, mtu anayekutaka kimwili hali wewe bado ni mchumba tu na sio mwanandoa, ujue huyo hakujali kabisa! Atakusumbua baadae!!!
Kumbuka ;
Mchumba ninayemzungumzia ni mtu yule aliyechumbia/kuchumbiwa akiitazamia ndoa hivi karibuni pasipo kufanya tendo la ndoa kwa sababu wao si wanandoa. Na kwa sababu hiyo, kwa mila na tamaduni za leo binti huvalishwa pete “pete ya uchumba ” ili jamii itambue kwamba binti huyo amekwisha chumbiwa, na anataraji ndoa. Hivyo binti anapaswa kutulia akisubiri ndoa. Vivyo hivyo kwa kijana, anapaswa kutulia akisubiri ndoa…
ITAENDELEA…
Ikiwa kama umejifunza kitu, nifahamishe na Kwa msaada zaidi piga;Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
What’sapp namba+255 746 446 446 .
Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários