HEKIMA YA KUISHI NA MPUMBAVU.
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 16, 2022
- 4 min read
Updated: Aug 29, 2022

Kwa ufupi,
Hakuna mtu anayetaka kuishi na mpumbavu lakini kuna wakati huwa inatokea tu,unajikuta mtu uliyenaye ni mpumbavu wa kutupwa na huyo ndiye mtu wako wa karibu kiasi kwamba huwezi kumwacha maana ni mtu wako.
Fikiria kwamba mtu kama mumeo au mkeo ndio ni mpumbavu,Kwa kweli huwezi kumwacha kwa sababu ya upumbavu wake isipokuwa utakachohitaji ni hekima ya kuishi naye,maana ni wako huyo!
Au yawezekana mzazi wako akawa ni kama mtu mpumbavu,na hapo huwezi kumkataa Bali ni kujifunza namna ya kuishi naye.
Nikupe kisa kimoja ndani ya Biblia cha ndoa kati ya mwanamke aliyeolewa na mwanamme mpumbavu,tena alikuwa “mpumbavu wa kutosha!” Kisa na mkasa ni ndoa ya Nabali na Abigaili.
Na huyo ndiyo aina ya mpumbavu ninayemzungumzia,mtu ambaye ni mwovu,asiyekubali kumsikiliza mtu mwingine yeyote. Mtu wa visa Kila siku,ugomvi, kelele ni jadi yake,mtu asiyeuzuia ulimi wake katika matusi. Kwa kifupi mtu mbaya
Biblia inasema kuwa mume huyo Nabali alikuwa hana adabu,mtu mwovu katika matendo yake, mpumbavu tu wa kawaida! Bali mke wake alikuwa binti mzuri wa uso,mwenye akili,na ni mke mwenye hekima za kutosha ( 1 Samweli 25:3)
Ukiwa katika ndoa ya namna hii,kama huna hekima basi ujue ndoa itakushinda tu kwa maana sio jambo dogo kuishi na mtu kama Nabali. Sipati picha ndoa ya Abigaili na huyo Nabali ilikuwaje !!! But kwa sababu ya “hekima “ aliyokuwa nayo huyo Abigaili,alifanikiwa kuishi na mpumbavu mwanzo mpaka mwisho. Unajua biblia haijatuambia muda wa ndoa yao ulikuwa ni miaka mingapi lakini katika muda wote huo mwenye hekima alifaulu kuishi na mpumbavu.
Abigaili alijifunza wapi hekima ya kuishi na mpumbavu Nabali? Alikuwa akiishije na huyo jamaa ? Bila shaka kuna mambo machache hivi ya kujifunza kati mengi aliyokuwa nayo Abigaili.
01. Kujitambua na kumtambua Nabali vizuri
Abigaili alifanikiwa kujitambua yeye ni nani na anapaswa kusimama katika eneo lipi akiwa ndani ya ndoa yake. Pamoja na uzuri aliokuwa nao, uzuri haukumsumbua “kudanga” / kujiuza Bali alitulia katika ndoa na kukiweka katika nafasi yake kama mke. Lakini si hivyo tu mwanamke huyu alimjua vizuri mume wake ni mtu wa namna gani. Ndio maana mwanamke huyu alipokutana na hasira Kali ya Daudi, mwanamke alimwambia;
“..usimwangalie huyu mtu asiyefaa,yaani Nabali Kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye…na upumbavu anao…” 1 Samweli 25:25.
Kwa maneno haya,yanaonesha alimjua vizuri mume wake. Hivyo upumbavu wa mume wake haukumsumbua kabisa! Shida ya kwanza inayosumbua mtu hata kushindwa kuishi na mpumbavu ni hali ya kushindwa kumjua lakini laiti kama utamjua vizuri mpumbavu wako,utajua namna ya kuishi naye.
Waswahili husema “ ukitaka kula na kipofu,usimshike mkono” yaani ukishajua upumbavu wa mtu,basi usimshike mkono wake!
Ukiona mtu analumbana na mpumbavu wa aina yoyote basi hapo ujue kwamba shida itakuwa ni katika hali ya kwanza ya kumsom huyo mpumbavu. Na hii ndio hekima ya kwanza na iliyo kubwa. Mpumbavu akiinuka katika jambo lolote, mwenye hekima anapaswa ashuke ili mambo mengine yaendelee lakini kama mpumbavu akiinuka na papo hapo mwenye hekima naye akiinuka basi ujue kitakachofuata ni kitu kinaitwa “ vita ” na vita hiyo haitamwacha mwenye hekima salama!
02. Maneno mazuri ya kuishusha hasira ya mpumbavu.
Hatua ya pili muhimu ni kujifunza kuyatawala maneno Yako ukiwa na mpumbavu. Kwa maneno mazuri yanalegeza hasira ya mpumbavu na kujikuta akipoteza nguvu ya kuendelea katika upumbavu wake kwako. Ukiwa vizuri katika maneno ujue mpumbavu aweza kuwa mpumbavu kwa wengine lakini asiwe kwako! Umenipata hapo?
Kumbuka Neno like katika Mithali 15:1 (KJV) “ Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.”
Ni muhimu ujifinze kukitawala kinywa chako hasa unapoishi na mpumbavu Kwa maana mpumbavu hutafuta utajikwaa wapi kwa habari ya maneno yako na atakaponasa ulipojichanganya,basi ujue atakupigia hapo hapo .
03. Uwezo wa kuvumilia
Hii ni hekima kubwa unayopaswa uwe nayo ikiwa upo na mpumbavu.
Kwa maana kama kuudhiwa utaudhiwa sana na hapo kinachohitajika ni nguvu ya kuvumilia. Jamani mtu kama Nabali alikuwa ni mtu wa kuudhi watu na kukera sana,maana tunaona tu vile alivyowatukana watenda kazi wa Daudi.
Hata Abigaili alipojulishwa habari hiyo,aliweza kumvumilia mumewe sio kwamba alipenda mumewe afanyie hivyo,but ilimbidi tu avumilie matusi yote hayo ingawa alikuwa hatukanwi yeye.
Hii inatuonesha Abigaili alikuwa na nguvu ya kuvumilia matusi,ulevi na ugomvi wa mume wake. Na ukisoma katika ( 1 Samweli 25:36) utaiona hekima ya Abigaili ya kuvumilia Kwa maana hapo Nabali alikuwa amelewa kwa mvinyo chakali,kisha Abigaili mkewe hakumwambia neno lolote lilo dogo wala kubwa ingawa Nabali alikwisha haribu .
Kitendo cha Abigaili kuwa kimya mpaka kesho asubuhi ni kitendo cha uvumilivu na hekima ya juu sana.
Shida ya wengi leo wanajikuta wakitukanwa au kupigwa kwa sababu ya kukosa uvumilivu kidogo tu. Mfano kama huo,labda inatokea kwako Nabali wako naye siku kavulugwa kwa hiyo mudi yake si nzuri,Sasa wewe badala ya kumsubiria kesho atakapokaa sawa ndipo uzungumze naye,
lakini wewe siku hiyo hiyo alipovuligwa nawe unanganganiza kusema naye,nakwambia atakuvuluga na wewe usipoangalia,atakupigia!!! Abigaili alipomjua Nabali na upumbavu wake alimvumilia na hatimaye uvumilivu wake ulikuja kumlipa.
04. Maombi
Mpumbavu anaombewa vizuri tu na Mungu aweza kumsaidia katika upumbavu wake. Ukiishi na mpumbavu,suala la kumwinua mbele za Bwana ni suala muhimu sana litakalowezesha upate kibali cha kuwa naye, lakini pia maombi humnyongonyesha mpumbavu katika upumbavu wake na hatimaye aweza akawa mbali na upumbavu wake.
Abigaili naye bila shaka nguvu ya kuishi na Nabali aliipata kutoka Kwa Mungu na hii inaonesha alikuwa akiomba na ndio maana Bwana alimkumbuka na hatimaye akaja kuwa mke wa mfalme Daudi. Ni muhimu kumwombea Nabali wako bila kuchoka Kwa maana Bwana Mungu aweza kumgeuza,kuna siku na saa usiyodhani wewe atageuzwa na kuwa mtu mwema.
Kwa msaada zaidi na maombezi;
lakini ikiwa pia umebarikiwa nifahamishe kwa +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla
UBARIKIWE.
コメント