UINJILISTI.
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 25, 2018
- 4 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Kwa ujumla,Uinjilisti unazungumzia mambo makubwa matatu;
Mwanadamu amefanya dhambi ( Warumi 5:12,3:23)
Upendo wa Mungu dhidi ya mwanadamu ( Yoh.3:16,1 Timotheo 2:3-4)
Wokovu kupitia dhabihu ya dhambi,Yesu Kristo ( 2 Wakorintho 5:21)
Hivyo uinjilisti umejengwa kwenye neno hili “ Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; ” 1 Wakorintho 15:3-4
Uinjilisti ni kufa,kuzikwa na kufufuka katika wafu. Kila mwinjilisti awe ni mzungu,mchina,yaani mwinjisti yoyote ni lazima ahubiri mambo hayo matatu. Ni muhimu kujifunza hayo ili uweze kuimarisha injili yako.
Hivyo ni vyema ukajiuliza maswali haya machache;
Uinjilisti ni nini hasa?
Mwinjilisti ni nani?
Sifa gani alizonazo mwinjisti?
Njia za uinjilisti,ni zipi?
01. Uinjilisti ni nini hasa?
Uinjilisti ni kazi ya kuhubiri,kutanga na kueneza habari njema ya wokovu wa Yesu Kristo ( Marko 16:15). Pia ni agizo kuu ( sehemu ya agizo )- Mathayo 28:18-20. Uinjilisti ni ofisi maalumu katika zile ofisi tano ( Waefeso 4:11).
Kanisa lolote likikosa ofisi hii,hilo kanisa litakuwa na shida sehemu fulani,kwa sababu ni ofisi ya Bwana mwenyewe. Ninaposema neno “ ofisi” nina maana ya “huduma“,hivyo unapouangalia uinjilisti uutizame katika jicho la huduma kama zilivyo huduma nyingine mfano kama vile uchungaji,ualimu,n.k na “uinjilisti” ni huduma pia.
02. Mwinjilisti ni nani?
Kila aliyeokoka ni “mwinjilisti wa ujumla” (general evangelist). Ikiwa wewe umepata neema tu ya kuokoka basi ujihesabu kwamba unayo kazi ya kufanya,la ukiionea haya injili ya Bwana basi ujue utapata shida sana wakati Yesu atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu,kwa maana naye atakuonea haya ( Marko 8:38).
Unaweza ukahubiri injili kwa mali zako,fedha na utajiri uliopewa kwa kusapoti kazi ya injili isonge mbele. Ukifanya hivyo,basi utakuwa umeshiriki kazi ya injili pia. Jifunze kwa wale wanawake waliomuhudumia Yesu kwa mali zao ( Luka 8:3).
Lakini hiyo tu haitoshi. Bali unapaswa kumshuhudia Bwana kwa “kinywa chako“,ya kwamba upo wokovu. Hii ina maana ya kwamba huwezi kukosa cha kusema kuhusu wokovu ikiwa umeokoka. Na hicho ukisemacho ni injili. Na ndio maana injili ni kazi ya kila mkristo aliyeokoka.
“Special evangelist “ huu ndio uinjilisti ambao ni kwa watu wachache walioitwa kuifanya. Watu hawa wanaitwa “wainjilisti” ambao wamebeba wito wa injili, wapo tayari kufa kwa ajili ya injili.Mfano ;Biblia inamtaja Filipo kuwa ni mmoja kati ya winjilisti ( Matendo 21:8).
Lakini si hivyo,Yesu naye alikuwa ni mwinjilisti mzuri mwenye kutufundisha kuifanya kazi hii kwa moyo wote. Tazama,Yesu anakwenda kuhubiri injili huko Samaria na kwa sababu hiyo,inamlazimu kukaa siku mbili Samaria akihubiri,kisha biblia inatuambia watu wengi walikuja kuokoka kama matokeo ya injili iliyohubiriwa. Umeona hapo? Kwamba mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache,kiasi kwamba Yesu pekee ashinde akikaa Samaria kwa siku mbili. Soma mwenyewe hapa ( Yoh. 4:1-4,39-42)
Samaria ni wapi?
Samaria katika agano la kale ni tofauti na Samaria inayotajwa kwenye agano jipya,kwa kuwa Samaria ya agano jipya ilikuwa ni Samaria ya wamataifa ( ya wasiokuwa waisraeli). Kumbuka nchi yote ya Palestina katika agano jipya ilikuwa imegawanyika katika sehemu tatu,nazo ni;
Uyahudi sehemu ya kusini
Samaria – sehemu ya katikati ya palestina ( nchi ya katikati)
Galilaya – sehemu ya kaskazini.
Hivyo unaposoma kwamba “ Yesu alitelemkia Samaria ” ujue aliwaendea watu ambao si waisraeli ( chotara wa kiisraeli),watu wasiokuwa na Mungu. Haikuwa rahisi kama unavyoweza leo kusoma mara moja na kupita tu,ujue hapo mwanzo kazi ilikuwa kubwa sana.
Tunaona wainjilisti kama vile ; Paulo,Barnabas,Petro,Filipo,Yohana. N.K ambao wengine walikuwa ni mitume lakini papo hapo walifanya kazi ya injili, jifunze hapo. Maana leo mtu akiwa ni mchungaji au mtume au mwimbaji,basi hataki kubeba injili,jifunze kwa watu hao ambao walikuwa ni mitume wakubwa na papo hapo walibeba injili na kusonga mbele.
03. Sifa za mwinjilisti.( special evangelist / wale walioitwa)
Awe ni mwenye wito (,sio kuchaguliwa wala sio kusomea,bali Roho amwite kwanza)
Awe msomaji na mwombaji.
Awe na kutafakari neno kila siku na kuwa na muda wa ukimya mbele za Bwana.
Roho mtakatifu ajazwe naye ( awe akisikia kushudia injili bila woga)
Awe na maisha matakatifu ( maisha ya ushuhuda)
04. Njia za uinjilisti.
Injili ya nyumba kwa nyumba.
Injili kwenye halaiki ya watu ( mfano, sokoni,vituo vya basi nk)
Injili kwa njia ya vyombo vya habari ( mfano radio,mitandao ya kijamii)
Injili ya majukwaa.
Kumbuka ;
Uinjilisti sio chaguo,bali ni lazima kwako. Ebu jiulize sasa,Je hivi ndugu zako labda baba au mama au ndugu zako,mbona hawajaokoka hata sasa? Una mpango gani kwao? Au unafikiri watahubiriwa na nani kama sio wewe ?( ambaye Mungu amekupa neema ya kuokoka ili kusudi uwaimarishe hao) Fikiri mara mbili hapo!!!
Ebu fikiri kwamba; kama watumishi wa Mungu,wachungaji au wainjilisti wote wangelikuwa na injili kila kona,au kama wangelitumia mitandao ya kijamii kuhubiri injili tena bure,kama injili hii unavyoipata bure,Je tungelikuwa wapi leo? Lakini ebu angalia leo kile kinachofanywa na watumishi wa Mungu wa leo, kwenye mitandao ndio hutumia kuweka picha zao wakiwa na wake au waume zao kisha huandika “type/ andika chni amen na utabarikiwa” Khaaa!!! Ndio nini sasa,?
Badala ya kutufundisha neno wewe unaweka picha zako tu,tena wakati mwingine kwa kweli picha hizo zinaboa,maana utakuta mchungaji kamwombea mtu,basi mtu kadondoka na hiyo picha au video ndio anaiweka kwenye mtandao,Jiulize “sasa mimi au sisi inatusaidia nini ? . Tumia vyema nafasi yako ili kupitia wewe watu waokoke.
Ikiwa umebarikiwa na fundisho hili nifahamishe pia. Kwa maombezi pia nipigie kwa namba hizi hizi + 255 683 877 900
WhatsApp ni .+255 746 446 446
Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments