top of page

UFAHAMU KUHUSU NDOA~03

07.VIGEZO/SIFA ZA NDOA.

Na Mch.G.Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa kuwa ndoa ni tendo takatifu,hivyo ni vyema kuangalia vigezo vyake ili uweze kujipanga vizuri katika ndoa yako ikiwa kama bado hujaoa/hujaolewa. Au ukiwa umeoa/kuolewa basi ni vyema kujifunza zaidi mambo haya yakusaidie katika ndoa yako pia yakusaidie kuwaelimisha vijana wanaojiandaa katika eneo la ndoa. 

Hivyo ni lazima tujue kwa ni mwanaume ndie anayeoa mke mwema atokaye kwa Bwana. Lakini mwanaume mwenye kutaka mume mwema atokaye kwa Bwana ni lazima huyo mwanaume naye awe kwa Bwana. Akiwa kwa Bwana basi ujue atampata aliye kwa Bwana kama mwanaume/mwanamke huyo amempa uhuru wa kutosha Roho mtakatifu.

Mara nyingi aliyekuwa rohoni hufunga ndoa na aliye rohoni ingawa si mara zote. Hii ni sawa na kusema ukiwa mwilini utakutana na wa mwilini mwenzako!! Sasa tuangalie neno linasemaje kuhusu vigezo vya Kiungu vya ndoa tukianza kwa kumuangalia mwanamume;

BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” Mwanzo 2:15

Katika andiko hili tunaweza kujifunza mambo manne ambayo yanasimama kama sifa za yule anayetaka kuoa. Katika mambo hayo yote ni lazima yajengwe katika pendo la kweli lisilo na unafiki. Hivyo kupitia andiko hiyo,tunajifunza vigezo vitatu;

  1. Mwanaume mwenye uwepo wa Bwana.

  2. Mwenye kazi /na anayeweza kujitegemea.

  3. Ajuaye kutunza

  4. Mwenye pendo la kweli katika kuoa na sio kucgezea.

01. Mwanaume mwenye uwepo wa Bwana.

Mwanaume wa namna hii ni yule aliye katika wokovu mwenye hofu na Mungu. Biblia inamtaja Adamu kabla ya kupewavmsaidizi,adamu alikuwa uweponi mwa Mungu. Kigezo hiki ni muhimu sana kwa maana mwanaume mwenye hofu ya Mungu ndie baba bora katika familia yake. Unajua huwezi kuolewa na mwanaume yeyote kabla ya kuichunguza kiwango cha imani yake.

Ikiwa binti ameokoka anapaswa aolewe na aliyeokoka kwa sababu asije akafungiwa nira na asiyeamini ( 2 Wakorintho 6:14). Ni mapenzi ya Mungu kuiona ndoa inafanyika eneo la ibada likiongozwa na kichwa/kiongozi wa ndoa ambaye ni mwanaume;sasa ni vigumu ndoa kufanyika eneo la kiibada ikiwa mume (kichwa) amekuwa mbali na Mungu.

Hiki ni kigezo cha kwanza cha kiroho tunapojifunza ndoa takatifu. Unajua ukiwa wewe ni binti ni lazima uwe makini kuyajua haya,ili mwanaume anayetaka kukuo anapaswa kuokoka na awe mcha Mungu na huyo mwanaume akiingia katika ndoa ataweza kuisimamia vizuri ndoa yake. 

02.Mwanaume mwenye kazi

Ninajua ya kwamba binti anaweza kumpata mwanaume wa kuolewa naye,alafu mwanaume huyo akawa hana kazi ila kuokoka vizuri. Kibiblia mwanaume ndiye anayetakiwa kuitunza familia yake katika malazi,chakula na mavazi. Mambo hayo yote yanahitaji pesa, na pesa huja kwa kufanya kazi. Biblia inatuonesha Adamu alipewa kazi ya kuilima bustani,hii haikuwa na maana kwamba Adamu alipolima alipewa pesa za kumtunza mkewe bali ina maana kwamba Adamu hakuwekwa bure bustanini bali afanye kazi pia,kama ishara ya mwanaume katika familia ndie dira ya utafutaji wa pesa na mali kwa ajili ya mke na watoto.

Kigezo hiki ni muhimu japo leo wengine wanakifasiri vibaya sababu kuna mabinti wanaohitaji kuolewa na watu wenye kazi fulani hivi wanazozitaka wao. Wakiona mwanaume anafanya kazi wasizozitaka wao ingawa ni kazi nzuri na halali wanawakataa,mfano; binti mmoja alikuwa akitaka mwanaume mwenye kufanya kazi ya umeneja wa bank (bank manager au awe afisa wa bank) au anafanyia kazi ya kiafisa kwenye mitandao ya simu ( mfano awe mfanyakazi wa Vodacom,tigo,airtel,Zantel) Sasa kinachotokea anawakosa wanaume wa aina hiyo kwa sababu alikuwa akiangalia vigezo vya kimwili sana visivyo na maana na hatimaye akawapoteza watu sahihi.

Changamoto ya namna hii imewakumba wadada wengi kwa maana wanaangalia mwilini,wakitaka mwanaume fulani hivi handsome mwenye pesa nyingi au mwenye utajiri fulani hivi,mwenye gari nzuri na smart phones nk. Kumbuka ukimpata gafura mwanaume wa namna hii atakutesa huko mbele ikiwa hana hofu na Mungu, kwa sababu ni wanaume wachache sana wenye mali pamoja na kuwa na hofu ya Mungu,wengi wenye mali wameigeukia dunia.

 Ikiwa ni binti uliyeokoka na kumpenda Yesu basi usikubali kuolewa na mwanaume aliyeigeukia dunia ( mpenda anasa) hata kama anapesa(mali) kwa kigezo cha kusema mkishaoana utambadilisha imani yake aokoke awe kama wewe! Wengi waliojaribu kuolewa na watu kama hawa walijikuta wao ndio wakibadilishwa imani zao badala ya kuwabadilisha waume zao. Kumbuka;mwenye kubadilisha imani ya mtu ni Mungu,wewe huwezi kufanya hivyo kwa sasa labda uwe rohoni kwa viwango vya juu sana.

Kigezo hiki hakitakiwi kichukue nafasi kuliko kigecho cha kiroho,kwa sababu kazi za mwili ni za kawaida kabisa ingawa tunazihitaji. 

Ni kweli mwanaume asiye na kazi anaweza kuoa katika mapenzi ya Mungu lakini ni lazima aweze kujitegemea kiuchumi,hilo ni jambo la lazima. Kwa kuwa baada ya kuoa maisha yanaendelea ya ndoa,hivyo mwanaume awe mtafutaji (Mwanzo 3:19a)

03. Mwanaume mwenye kujua kutunza ndoa yake.

Katika eneo hili ni muhimu kujua kwamba jukumu kubwa la kuitunza ndoa ni la mwanaume. Kuitunza na kuilinda ndoa yako ni wewe mwanaume ndiye mwenye jukumu.  Kiasili,mwanaume ameumbwa na misuri aweze kuitunza na kuilinda ndoa na familia yote kwa ujumla dhidi ya uvamizi wa aina yoyote. Ni mpango wa Mungu kumuweka mwanaume awe kiongozi.

04. Mwanaume mwenye pendo la kweli.

Nimeshuhudia wanaume wengi wakiwanyanyasa wake zao kwa sababu wamekosa pendo la kweli. Unajua kwamba wanawake hawahitaji mambo mengi sana bali wanahitaji kupendwa tu.“ Wanawake wanahitaji kupendwa“Mwanaume  asiye na pendo la kweli ni yule anayemwambia binti “nimekupenda nataka nikuoe,lakini njoo tulale kwanza,lakini nitakuoa tu…”  huyo hafai. Kwa maana pendo lake si la kuoa bali ni la kuchezea tu kwa maana mwenye kuhitaji kuoa hana haja ya kulala na mwanamke. Biblia haifundishi kwamba wapenzi watembee kisha waoane! Bali waoane ndipo watembee. Epuka mtu wa namna hiyo mwenye kutaka penzi kwanza kisha ndipo aoe…

ITAENDELEA…

Kwa msaada zaidi pamoja na maombi tafadhali usisite kunipigia kwa simu +255 683 877 900

What’s app number ni +255 746 446 446

Mch.Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page