top of page

UFAHAMU KUHUSU NDOA~02.

Na Mch.G.Madumla


04. MAANA YA NDOA YA KIKRISTO.

Tafsiri ya ndoa sawa sawa na neno la Mungu inatofautiana sana na tafsiri ya ndoa kwa mujibu wa sheria ya nchi. Wakati sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inatumia jina la“ ndoa ni muunganiko wa hiyari wa kudumu” lakini neno linaeleza kuwa ndoa ni zaidi ya muunganiko wa kimwili. Hivyo tafsiri nyepesi na iliyo sahihi kuhusu ndoa ni; 

Ndoa ni muunganiko wa kiagano wa kudumu kati ya mwanaume mmoja na mwanamke mmoja wenye kuishi na kuwa mume na mke. Neno agano ni neno muhimu sana kwa sababu agano ni patano la milele ambaye shahidi yake ni Mungu mwenyewe wala si mwanadamu. Kwa lugha nyepesi,agano ni tofauti na mkataba kwa maana mkataba una muda wa kuisha,kuvunjwa n.k bali agano halina muda wa kuisha,wala halivunjwi kwa sababu aliyeliunganisha agano ni Mungu mwenyewe “aliyewaunganisha Mungu mwanadamu asiwatenganishe” Mathayo 19:6

Ndoa ni taasisi ya Mungu iliyojengwa juu ya agano la mume mmoja na mke mmoja wakiungamanishwa na agano hili na kuwa mwili mmoja Mwanzo 2:24. Tunapozungumzia “taasisi ya ya Mungu” tuna maana pana sana,kwamba ni kitivo cha mafunzo endelevu ambapo Mungu ndie mwanzilishi wao. Leo tunaona vile watu wawili wakifunga agano la ndoa alafu gafula wanapewa vyeti utafikiri wamehitimu mafunzo fulani lakini kumbe ndio kwanza wanaanza na mafunzo ya KiMungu katika kitivo hicho.

05.MPANGO WA MUNGU KATIKA NDOA.

Ndoa ni mpango wa Mungu wa kuitiisha nchi na vyote vilivyoumbwa( Mwanzo 1:28),Hivyo ni eneo muhimu ambapo Mungu alitamka baraka za namna yake. Si vyema mtu awe peke yake ( Mwanzo 2:18) bali Ni vyema mtu awe na mwenzi wa ndoa. Hii ikiwa na maana kwamba haipendezi mtu kuishi bila ndoa isipokuwa kama kuna sababu ya msingi,lakini Mungu alipomuumba mtu mume na mtu mke aliwakutanisha wawe pamoja kwa sababu ndio mpango wake.

Hapo mwanzo Mungu alimuumba mtu mwanaume na mwanamke waishi pamoja wakitegemeana kila mmoja. Adamu mtu mume hakuweza kufanya yote alihitaji msaidizi Hawa;naye Hawa mtu mke hakuweza kufanya yote alimuhitaji mumewe Adamu. Hivyo kila mmoja alikamilishwa na uwepo wa mwenzake na hakuna mmoja aliyekuwa juu ya mwenzake ( katika maana ya kwamba mmoja ana nguvu na mmoja ni dhaifu) bali wote walihitajiana.  Mungu aliwaumba kwa sura na mmfano wake ( Mwanzo 1:27-28). 

Je nini chanzo cha ndoa zaidi ya mke mmoja?

Haikuwa hivyo tangu mwanzo kwa mwanaume kuoa wake zaidi ya mmoja bali ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya watu ( Mathayo 19:8). Chanzo cha ndoa za wake wengi kilianzia kwa lango la Kaini katika kizazi chake cha tano yaani Lameki. Lango hili lililokuwa limekwisha haribiwa na dhambi,lango hili lilikuwa limepitisha roho ya mauaji na hapo ndipo ndoa ya wake wengi kwa mara ya kwanza katika biblia inatajwa,Neno linasema; “  Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.” Mwanzo 4:19

Hivyo, chanzo cha ndoa za wake wengi ni dhambi iliyoshikilia mioyo ya watu;maana Tangia hapo tunaanza kuona lango limefunguliwa la kuoa wake zaidi ya mmoja. Lakini lango hili lilikuwa la uharibifu kwa sababu sio mpango wa Mungu huo,lakini Mungu aliwaacha wayafanye wasiyoyapasa zamani zile za ujinga ( Matendo 17:30). Baadae sasa tunaona jambo hili likiendelea kwa watu wengine,mfano;

  1. Ibrahimu akizaa na kijakazi wake,Hajiri ( Mwanzo 16:16)

  2. Yakobo akiwa na wake Lea,Raheli na vijakazi wawili ( Mwanzo 29:21-35,30:1-5)

  3. Gedeoni alikuwa na wake wengi na kuzaa watoto 70 ( Waamuzi 8:30)

  4. Sulemani akaoa wake mia saba na masuria mia tatu ( 1 Wafalme 11:3) N.k

Yafuatayo ni mambo ambayo yanasimama na kuwa ni mpango wa Mungu katika ndoa;

  1. Ni mpango wa Mungu kuishi na mume/mke mmoja

  2. Ni mpango wa Mungu kutoa zawadi/baraka ya watoto katika ndoa

  3. Ni mpango wa Mungu kwa wana ndoa kuwa na upendo na kufurahiana kila mmoja. Na ndio maana ndoa na iheshimiwe na watu wote.

  4. Ni mpango wa Mungu kuwa na ndoa takatifu ambapo ibada ya kweli iwe inafanyika mara kwa mara.

06.KWA NINI NDOA?

Nilikuwa najiuliza kwa nini ndoa ziwepo? Kwani bila ndoa maisha yangelikuwaje? Sijui kama wewe umeshawahi kujiuliza hivyo. Lakini nikagundua kuna haja kubwa ya ndoa kuwepo. Swali la namna hilo linapanua wigo wetu tunapojifunza masuala ya ndoa. Jibu lake ni jepesi nalo ni;ndoa zipo kwa sababu ndio asili au chanzo cha utakatifu. Kusudi la utakatifu linaanzia kwenye msingi wa ndoa hatimaye familia,mpaka taifa.  Hivyo ndoa ni kama mzizi wa utakatifu wa kweli,na ndio maana shetani anapopambana na watakatifu anaanzia kwenye ndoa akiakikisha ndoa iwe na mvurugano.

Ndoa ikivurugwa hakuna utakatifu hata kidogo. Mfano,ikiwa umetofautiana na kugombana na mwenzi wako je wawezaje kuwa mtu mwenye haki? Au je wawezaje kuwa na mausiano mema na Mungu wako? Je maombi yako hayatazuiliwa ikiwa una maugomvi ndani  ya nyumba wewe na mwenzi wako? Tena nina kuambia katika hali hiyo huwezi kuwa na sifa ya kuliongoza kanisa la Bwana, biblia inasema ; “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” 1 Timotheo 5:8

Mbali na kuijaza dunia kwa ongezeko la kuzaa watoto,pia utakatifu kama sehemu ya kusanyiko la ibada linastahili kuanzia katika ndoa. Katika ndoa ndipo wawili waliokuwa mwili mmoja wanaweza kumuabudu Mungu katika roho na kweli,wakiomba na maombi yao yana nguvu sana. shetani anapata shida sana kuvamia ndoa zilizosimama kwa Bwana.

Hivi unajua ndoa ikiwa takatifu hata watoto husafishwa na kuanza mchakato wa kumlingana Mungu? Jifunze kwa familia ya Yusufu na Mariamu (Yusufu baba mlezi wa Yesu), watu hawa walikuwa ni wenye haki mbele za Mungu kiasi kwamba Mungu alikubali kuruhusu mwokozi kuzaliwa kwao,unafikiri wangelikuwa ni watu ovyo ovyo hivi,Mungu angeruhusu mwokozi Yesu azaliwe kwao?

Ukiitazama ndoa kama chanzo cha kanisa la Bwana utakuwa unapata maana kamili ya utakatifu yaani kutengwa na Bwana. Hata sasa,jaribu kuifanya ndoa yako imjue Mungu kisha utaona hata watoto wako watamuelekea Mungu na hapo ndipo watumishi wa Mungu watatokea…

ITAENDELEA

Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi nipigie +255 683 877 900

what’s app number ni +255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page