top of page

UFAHAMU KUHUSU NDOA~01

Na Mch.G.Madumla.


Bwana Yesu asifiwe….

Ni vyema siku ya leo ukajifunza kiundani kuhusu ndoa takatifu ili kusudi ufahamu huu ukusaidie katika maamuzi yako ya kuoa au kuolewa. Lah! Ukiwa kama umekwisha kuwa ni mwanandoa basi ufahamu huu ukusaidie kuikarabati ndoa yako ili ndoa yako sasa ielekee katika mpango kamili wa ndoa.

Kumbuka jambo moja kwamba tunapozungumzia “ndoa takatifu” tunazungumzia ndoa zilizo katika makusudi ya Mungu. Ikiwa ni hivyo basi,ni dhahili kwamba zipo ndoa nyingine zilizo nje ya mpango wa Mungu. Je utaijuaje ndoa yako kama ipo katika mpango na kusudi la Mungu?

Kupitia fundisho hili,utapata mwanga wa kuiangalia ndoa ipoje. Au kwako wewe ambaye bado hujaingia katika ndoa basi fundisho hili litakuelekeza namna ya kutembea vizuri ili usije ukakosea kuoa. Ni afadhali sana ukosee vitu vingine lakini usikosee kuoa/kuolewa na mtu asiye chaguo la Mungu kwako. Hivyo utajifunza mambo yafuatayo;

  1. Maana ya ndoa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya 1971

  2. Vigezo au sifa ya ndoa kisheria ( Kiserikali)

  3. Mtazamo wa kiroho kuhusu mahakama katika ndoa

  4. Maana ya ndoa takatifu katika Kristo. (Kiimani)

  5. Mpango wa Mungu katika ndoa

  6. Kwa nini ndoa?

  7. Vigezo/sifa za ndoa takatifu.

  8. Je upi ni wakati sahihi wa kufunga ndoa? Ukiwa na mtu wako tayari au ukiwa bado hujapata yaani ukiwa single?

  9. Je waliokwisha kuishi kama mke na mume,ni wana ndoa? Sheria inasemaje na neno la Mungu linasemaje? 

  10. Watu wa namna hiyo walioishi wakitaka kufunga ndoa wanabariki? Au wanafunga ndoa? Kwa nini?

  11. Je kuna kuachana katika ndoa ya Kikristo? 

  12. Mengineyo.

01. MAANA YA NDOA KISHERIA.

Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971,ambayo sheria hii inasimamia mambo ya ndoa hapa nchini kwetu,imetafsiri ndoa kuwa ni muunganiko wa hiyari kati ya mwanaume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao.

Katika tafsiri hii ya neno ndoa tunaona kwamba Muunganiko huo unabeba sura ya kimkataba baina ya mtu mke na mtu mume,kwa sababu hiyo serikali utoa vyeti viwili ( marriage certificate) kama nakala maalumu ya kuthibitisha ndoa iliyofungwa.  Katika tafsiri isiyo ya kikatiba inasema ndoa ni muunganiko maalumu (formal union) kati ya mwanaume na mwanamke wa kuishi kisheria kama mke na mume.

Kumbuka; neno “ muunganiko wa hiyari” ni ule muunganiko unaowafanya watu wawili wenye kutofautiana katika jinsia zao,wakati mwingine kutofautiana katika kabila,rangi,muonekano,fikra/mtazamo wao n.k na sasa kukubaliana kuishi pamoja kwa kuziweka mbali tofauti zao. Na likifanyika hilo,basi ndipo tunasema watu hawa wameungana kwa hiyari yao wao wenyewe.

02.VIGEZO/SIFA YA NDOA KISHERIA.

Zifuatazo ni sifa za ndoa kufanyika ndoa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya 1971. Kwa ufupi kabisa ninazitaja hapa chini;

  1. Muunganiko lazima uwe ni wa hiyari.

  2. Muunganiko ni lazima uwe kati ya mwanaume na mwanamke.

  3. Wenye kufunga ndoa lazima wawe na akili timamu.

  4. Wafunga ndoa lazima wawe wametimiza umri unaokubalika kufunga ndoa – Sheria ya kwetu inawataka wawe na umri wa miaka 18 na kuendelea. Kwa mwanamke anaweza akafungishwa akiwa na umri kuanzia miaka 15 na kuendelea. Mwanaume 16 na kuendelea. 

  5. Muungano lazima ubebe kusudi la kudumu.- Ndoa itakuwa batili endapo itafungwa katika kusudi la muda mfupi.

  6. Wanaofunga ndoa wasiwe ndugu (hudusani ndugu wa karibu)- Sheria ya ndoa ya 1971 katika kifungu cha 14 inakataza maharimu ( ndugu wa karibu) kufunga ndoa. Mfano wa ndugu hao ni kuoa/kuolewa na baba au mama,mtoto wa kuzaa au kurithiwa (adopted child),dada au kaka,,shangazi au mjoba n.k

  7. Kusiwepo na muunganiko wa kindoa mwingine zaidi ya huo.

  8. Kukosekana kwa mashahidi – kwa mujibu wa sheria,ndoa itakuwa batili kama wakikosekana mashahidi.

  9. Kutokuwepo kwa wanandoa hao. -Ndoa ni batili ikifungwa hali wana ndoa hawapo,kwa maana ndoa hiyo haitakuwa halali kabisa.!

  10. Kukosekana na mamlaka ya kufungisha ndoa- Ni lazima anayefungisha ndoa awe amepewa mamlaka na serikali juu ya kufungisha ndoa.

  11. Muunganiko unahitaji kutolewa taarifa rasmi ya wazi kwa watu wote ndani ya siku 21 ili kusudi kama kuna kipingamizi chochote kilicho halali na kitolewe mara moja.

  12. Hali ya ugonjwa ikiwa imezidi kwa mmoja hakutakuwa na muunganiko kwa haraka mpaka arejee katika afya yake. -maana haitafungwa ndoa ikiwa mmoja amebebwa hajiwezi.

  13. N.K

03. MTAZAMO WA KIROHO KUHUSU MAHAKAMA KATIKA NDOA.

Japo kwa ufupi,ni vyema tukajua nini maana ya mahakama kiserikali.Mahakama ni moja ya muhimili wa serikali. Ni chombo cha kutatua masuala ya kisheria ya nchi tena chombo hiki kinawajibu wa kutoa tafsiri ya sheria za nchi.Dola yetu ina mihimili mitatu nayo ni;

i. Bunge – kutunga sheria na kuisimamia serikali;

ii. Mahakama – Kutoa fasiri za sheria za nchi;

iii. Serikali – Kusimamia na kutekeleza sheria pamoja na kutunga na kusimamia sera.

Mahakama pia;inashughulikia kesi za ndoa wakati mwengine kufungisha ndoa kwa mujibu wa kisheria. Katika mtazamo wa kiroho ndoa,mahakamani ni sehemu ambapo ndoa nyingi zinapelekwa kwa mashauri ya kuvunjwa. Hivyo eneo hilo linafanyika kama eneo la kusuluhisha na hatimaye nyingine kuvunjwa. Ukiona ndoa iliyofungwa kanisani imepelekwa mahakamani basi ujue hakuna shwari kwenye ndoa hiyo.

Ni sawa na kusema “ kanisa lafungisha,mahakama yavunja”. Sijawahi kuona ndoa zikivunjwa kwa talaka katika kanisa. Ikiwa kanisa ni chombo cha kusuluhisha kiroho kwa lengo la kupatanisha basi ni dhahiri ndoa zilizo na migogoro zilipaswa kupelekwa kanisani kwanza kabla ya mahakamani. Ikiwa kanisa limeshindwa kusuluhisha ndipo wapeleke mahakamamani. Ikiwa tunamuamini Yesu katika ndoa,basi kamwe hawezi kushindwa.

ITAENDELEA…

Na Mch.G.Madumla

Kwa msaada zaidi na huduma ya maombezi,piga +255 683 877 900

What’s app number ni +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page