UFAHAMU KUHUSU NDOA ~04
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 1, 2017
- 5 min read

Na Mch.Madumla.
08.JE UPI NI WAKATI ULIO SAHIHI WA KUFUNGA NDOA?
Bwana Yesu asifiwe…
Leo hii,tunajiuliza kwamba ni wakati gani hasa ulio sahihi wa kufunga ndoa? Je ni wakati ukiwa na mtu uliyempenda au ukiwa bado hujampata yaani ukiwa single ?
Awali ya yote ni lazima ufahamu kwamba maamuzi na mtazamo uliyopo kati ya mwanaume na mwanamke anayetaka kufunga ndoa unatofautiana sana. Kwa sababu jamii yetu tulionayo imekaa katika mfumo dume kwamba anayefanya maamuzi ya juu katika kufunga ndoa huwa ni mwanaume (kwa kuwa yeye akipenda kufunga ndoa anafunga,lakini utakuta binti akawa anataka kufanya maamuzi ya kufunga ndoa,na gafla mwanaume akakataa au akakubali lakini akamchelewesha sana kiasi kwamba wakawa wanaishi tu pasipo ndoa huku siku zinaenda,miaka inakatika na uzee unakuja)
Hivyo katika mfumo huu,mara nyingi mwanaume ndiye hufanya maamuzi ya mwisho. ( hali ya ndoa katika nchi kama india kwenye baadhi ya makabili,mwanamke ndie anayeoa kwa maali) Mfumo dume tulionao;unawachanganya sana mabinti zetu kwa maana utakuta binti akifuatwa na kijana,yeye binti ufikiria suala zima la kuolewa,lakini kumbe kijana hana haja ya kuoa bali anamtaka amchezee. Sasa ikiwa binti kama hajasimama vizuri,hujikuta ameangukia dhambini na amekosa kuolewa vile vile.
Lakini katika hayo yote,upo wakati ulio sahihi kwako wa kufunga ndoa na ubavu wako. Tunapozungumzia wakati,hatuna shabaha ya kuangalia sana kigezo cha umri;kwa sababu kigezo cha umri hakitoi majibu yaliyosahihi sana ingawa kinahitajika kidogo. Mfano tuchukulie binti wa miaka 20 anaweza akaolewa kwa kuwa umri huo sio mbaya,lakini ikiwa binti huyo hana uwezo wa kubeba majukumu( hajitambui bado),basi ni dhahiri hawezi kustahimili ndoa na utakuwa sio wakati wake ulio sahihi.Kigezo cha umri kinapewa kipaumbele kwamba vijana wanaohitaji kufundoa wasiwe ni watoto ( Angalau kuanzia umri wa miaka 20 kwa binti,na 25 kwa kijana wa kiume).
Katika mtazamo sahihi wa kiroho;
Ili kusudi tuweze kujua vyema wakati ulisahihi,basi hatuna budi kuliangalia jambo hili katika mtazamo wa kiroho. Hivyo yafuatayo ni majibu sahihi kwako katika kufanya maamuzi ya kuoa au kuolewa katika wakati uliokusudiwa;
01. Wakati uliokusudiwa na Bwana.
Mambo ya ndoa hayatakiwi kuendeshwa kimwili wala kulazimishwa. Kwa maana huwezi kuoa kwa sababu tu unapesa za kuolea. Au huwezi kuolewa kwa sababu umepevuka na una miemko miemko. Hapana! Bali wakati wako ulio sahihi ni ule wakati uliokusudiwa na Bwana. Swali la kujiuliza ni hili,wakati huo ni wakati gani?
JIBU;
Ni wakati ambapo Mungu amekuletea ubavu wako utokae kwako,sawa sawa na hitaji la moyo wako. Kamwe Mungu hawezi kukuletea mtu katika wakati usio sawa. Tena; kuwa Mungu wetu katika Kristo Yesu hufanya kazi yake katika uzuri na utaratibu,basi ukifika wakati uliokusudiwa atakuletea mwanaume na sio wanaume kwa kuwa huendi kuolewa na wanaume bali mwanaume mmoja aliye wa Bwana na ni vivyo hivyo kwa mwanaume anayetaka kuoa. Kumbuka kuna wakati wa Bwana uliokusudiwa “ …. ili awakweze kwa wakati wake…” 1 Petro 5:6. Hivyo ukitambua hilo,basi hutakiwi kulalamika wala kulia kwamba kwa nini umechelewa hujaolewa/hujaoa.
Unaweza ukaolewa/kuoa katika umri ulioenda na ikawa kwako ndio wakati ulio sahihi;kwa sababu kuoa/kuolewa ukiwa kijana haina maana kwamba ndio wakati ulio sahihi. Wewe una wakati wako,lakini Mungu pia ana wakati wake ulio sawa kwako. Ikiwa kama umeomba na bado hujaona kitu,basi kumbuka kuna wakati wa Bwana,ungoje kitakatifu nao utakuja tu,uwe na uhakika kabisa. Ukifika wakati wako,hakuna awezaye kuzuia,jifunze kwa Daudi yeye aliyepakwa mafuta awe mfalme lakini aliendelea kuchunga kondoo,akarudi shambani huku akiwa amepakwa mafuta ya ufalne,
Lakini ulipofika wakati wa Bwana Sauli hakuweza kuzuia bali Daudi akaja na kuketi katika kiti cha kifalme. Kitu gani kilikuwa kinafanya yote haya ni kimoja tu nacho ni wakati wa Bwana ulikuwa hujakusudiwa,lakini sasa umewadia… usife moyo,kwa maana wakati sahihi kwako ni ule utokao kwa Bwana. Na ikifika wakati wako wa kuoa/kuolewa na aliye wa Bwana utaona ishara nyingi kwako,Mungu atasema nawe kwa namna mbali mbali.
02.Wakati unapokuwa single ( kabla ya kuwa na mahusiano)
Unapokuwa single,unaweza kumuomba Mungu akupe mtu aliye sahihi kwa mapana zaidi kwa sababu hutaweza kumfikilia mtu fulani maana huna. Ni vyema ukaanza kujiandaa mapema ukiwa peke yako,kisha ukamuomba Mungu yule utakaye kwa vigezo vyako huku ukivipeleka vigezo hivyo mbele za BWANA. Wale wote waliofanya hivi kwa kumaanisha walipata watu sahihi maishani mwao,
kwa maana kama atakuja asiye wa Bwana basi uwe na uhakika ataondoka muda mfupi katika mahusiano yenu. Lakini leo,hali imebadilika kwa maana wengi wana watu wao tayari alafu papo hapo wanaomba Mungu awape watu sahihi wa kuoa/kuolewa,Sasa ikiwa umekwisha jichagulia tayari,unamuomba Mungu afanye nini? ( Yaani ukiwa tayari unaye,unaomba nini tena kwa Bwana)
Na Je ikiwa nina mtu wangu tayari,nifanyeje? Au ni wakati ulio sahihi wa kufunga naye ndoa?
Ikiwa una mtu tayari,yafaa umpeleke huyo mtu mbele za Bwana katika maombi ukimuomba Mungu akuoneshe kwamba huyo ni wa Bwana au lah! Lakini unatakiwa usilale naye kabisa. Kwa maana ukiwa unashiriki tendo la kujamiana,ni dhambi;Sasa huwezi kuwa na kibali kusimama mbele za Mungu na kuweza kuisikia sauti ya Mungu. Kumbuka hili Mungu hawasikii wenye dhambi. Lah! Ukiwa ulidondoka naye dhambini,mkalalana,basi uingie kwenye toba halisi na msiendelee kabisa kitendo hicho ili Mungu awe upande wako,akujibu maombi yako.
03.Wakati unapoweza kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wako pia uweze kujitambua na kubeba majukumu ya kindoa.
Hakikisha una mahusiano mazuri na Mungu wako katika Kristo Yesu. Na ikiwa umefanikiwa kumuona wa kufunga naye ndoa basi naye ni lazima awe na mahusiano mazuri na Mungu wake. Kuwa na mahusiano mazuri na Mungu ni kule kufanyika mwenye haki,kwanza kwa kuipokea neema ya wokovu/kuokoka na kuendelea kuukulia wokovu. Hii ni muhimu sana kwa sababu ndoa sio suala la kibinadamu ingawa ni sisi ndio tunalolipokea,ndoa ni suala la Kiungu.
Pili,Kwa mwanaume,anatakiwa aweze kubeba majukumu ya kifamilia,awe amepevuka kiakiri. Maana asiwe mwanaume ambaye bado mwenye mtazamo wa kusaidiwa na wazazi kwa kila kitu. Awe amejiandaa kujua kwamba sasa yeye anaingia kwenye kutegemewa na familia. Kwa mwanamke awe ni yule mwenye kuweza kubeba majukumu ya familia kama mama mfano kulea n.k
09. JE WALIOISHI KAMA MKE NA MUME PASIPO NDOA TAKATIFU,NI WANA NDOA? SHERIA INASEMAJE ? NENO NALO LINASEMAJE?
Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya kwetu,inamtambua mtu kuwa mke au mtu kuwa mume wa.. baada ya kuishi pamoja kwa muda usiopungua miezi 6 hivi. Watu hawa wanaitwa mke wa fulani na mume wa fulani kwa sababu kwa muda huo wameshiriki tendo la kulala pamoja. Lakini hili ni jambo la kimwili na la kawaida lisilo na mashiko katika imani yetu. Kiimani watu hutambulikana wanandoa halisi baada tu ya kufunga ndoa kanisani.
Wapo wale wanaofunga bomani/mahakamani n.k.Watu waliofunga huko,huitwa wanandoa,lakini bado wanahitajika waje kanisani katika kanisa la kiroho waanze na moja. Kwa sababu tunaamini ndoa inafungwa na Mungu kwenye mahali pa madhabahu yake kupitia mtumishi wake aliyemuweka Yeye.
Neno linasema kuwa ndoa na iwe safi yenye kuheshimiwa na watu wote ( Waebrania 13:4). Hivyo wale walioishi pasipo ndoa takatifu si wanandoa halali hatama wameshiriki mara nyingi tendo la kulala pamoja,bali wanandoa huweza kutambulika katika usahihi pale tu wanapofunga ndoa kwenye madhabahu ya Bwana. Hili ni muhimu sana. Leo tunashida kubwa sana na vilio vingi katika ndoa kwa sababu ya watu kuchukuana tu na kuamua kuishi pamoja kisha baadae wanajiita wao ni wana ndoa. Je Mungu amehusika katika mpango huo wa kuishi pamoja na huyo mwenzako? Ikiwa lah! Basi ujue hapo hakuna ndoa takatifu…..
ITAENDELEA…
Inawezekana unahitaji huduma zaidi katika maeneo haya ya mahusiano na ndoa,tafadhali usisite kunipigia simu sasa kwa namba hizi +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments