top of page

UFAHAMU KUHUSU “ BARAKA “

Updated: Sep 30, 2022


Mojawapo ya ndoto niliyokuwa nayo kipindi kile cha utoto, ni ndoto ya kufika ulaya na kuishi huko kwa wazungu . Tulipokuwa tukiangalia tamthilia zinazoeleza maisha ya watu wa magharibi hususani wazungu basi sote pale kijiweni tulijua kwamba “ wazungu wote wamebarikiwa” kwa kigezo cha maisha yao kwenye tamthilia.


Ni kweli tulikuwa tukijua kwamba wanaigiza tu, lakini tuliwakubali ile “mbaya” na kusema ama kweli wamebarikiwa wazungu wote. Kati ya vitu nilivyotamani sanaa, ni kuishi na wazungu, yaani we acha tu!


Siku moja mwenzetu kwenye maskani yetu alifanyiwa mpango na ndugu zake waliokuwa wakiishi Ujerumani kwamba aende kuishi kule. Dah! Ilituuma nakwambia! Basi kabla ya kuondoka akiwa kwenye maandalizi, tulianza kumuona mbarikiwa maana ndio shida zake bye bye! Baada ya muda, jamaa huyo akakwea pipa na kutuacha solemba! Miezi fulani hivi ikapita, jamaa akatutumia picha tukamuona amezungukwa na wazungu, hapo ndipo alipotuchanganya dah!


“ Yaani jamaa ndio kashatuacha, anapigwa na kipupwe cha wazungu kama namuona vile” hayo yalikuwa maneno ya rafiki yangu mmoja aliyekataa shule maana ndoto zake ni kupata “zali la ulaya” mimi nikasema “one day yes! ”


Akaja kutuchanganya tena mmoja wetu pale alipofanikiwa kwenda south africa, dah! Tukasema jaama kabarikiwa sana! Na kashatuacha maskani tukiangaika na jua letu! Hivyo, ndoto hii ilikuwa ndio ndoto mama kwa sisi vijana wa Sinza. Kila mzungu au mtu yeyote aishie ulaya, tulimuona amebarikiwa sana.


Nakumbuka wazungu fulani hivi walikuja mitaa yetu, alafu gafla nikazoeana nao nikasema hapa hapa na mimi nitabarikiwa kwenda zangu Ulaya ” Wazungu wenyewe walikuwa wakivuta masigala yao mabayaa!!! Na mapombe ya ulaya ndio zao, lakini sisi tulisema hawa jamaa wamebarikiwa bhana! Kigezo kikubwa cha kubarikiwa tuliangalia maisha mazuri ya magari n. K!


Na hili ndilo tatizo la wengi wetu, tunaamini ya kuwa wazungu wote wamebarikiwa na waafrika wote wamelaaniwa! Si kweli hata kidogo. Wahubiri wengine husema waafrika wamelaaniwa kwa sababu Nuhu alimlaani Kanaani mtoto wa Hamu ( Mwanzo 9:20-29). Lakini si kweli kwamba waafrika wamelaaniwa maana aliyelaaniwa ni Kanaani na sio Kushi.

Laana ilikuwa juu ya mtoto mmoja wa Hamu aitwae Kanaani, maana Hamu alikuwa na watoto wengi. ( Mwanzo 10:6).


Hivyo, nadharia ya kusema sisi watu weusi wamelaaniwa si kweli na ni makosa kabisa. Mimi sijui wamepata wapi kusema wafrika tumelaaniwa ikiwa biblia haikusema hivyo! Unajua sasa inanikera sana, maana sisi tunasema “tumelaaniwa” na wazungu na wao husema “waafrika wamelaaniwa” sasa haya maneno ndiyo yanaumba laana mahali pasipo na laana.

Imefika wakati sasa hata kwenye tamthilia za watu wa magharibi wakiigiza nafasi ya shetani wanamuweka mtu mweusi kuashiria mwafrika.


Cheki filamu nyingi kama utamuona shetani ni mzungu!!! Au wachoraji wa kimagharibi wakimchora shetani watamuweka mapembe, makucha na vitu vyote vya kutisha kisha mwishowe watahakikisha ni mweusi kama mwafrika. Kwanza shetani mwenyewe hawajawahi kumuona! Huu ni upuuzi, Wafrika hatujalaaniwa, bali tumejilaani wenyewe kwa kumuacha Mungu maana tulikuwa waabudu sanamu, watu tuliombali na Mungu wa kweli. Lakini leo ukirejea kwa Bwana, wew ni mbarikiwa haijalishi rangi yako.


Sasa nimekuwa bhana! Kumbe tulikuwa tukipotea kabisaa! Kumbe baraka hazipimwi kwenye wingi wa mali au fedha bali “ baraka ni kukutana na Yesu” mitazamo yetu haikuwa sahihi kama mitazamo ya wengine leo. Baraka ni kitu kingine kabisa na kuwa na mali au fedha ni kitu kingine kabisa!


  1. Baraka ni nini?


Kwa mujibu wa biblia ; baraka ni nguvu ya Mungu iletayo mafanikio. Ni uwezo wa kiungu wa kusababisha kufanikiwa sawa sawa na neno la Mungu. “ Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke,… ” Mwanzo 1:28. Wanadamu walipoumbwa, Bwana Mungu akawabarikia yaani Bwana Mungu aliweka uwezo wa kufanikiwa sawa sawa na kile alichokitamka “neno“.


Kama Mungu asingembarikia mwanadamu katika eneo la kuzaa, maana alisema “zaeni mkaongezeke” basi ni ukweli kabisa mwanadamu asingeweza kuzaa / kupata watoto. Tunazaa simply, Mungu ameweka nguvu ya kuzaa kama sehemu ya baraka tu.

It’s wonderful! Baraka hutembea kwenye neno “akawabarikia, akasema” hii ni sawa nguvu ya Mungu ya kusababisha kufanikiwa kwako hutegemea neno lake Mungu.


And this is a formula! Nje ya Neno hakuna baraka.! jifunze hilo,. Ni Mungu ndie mwasisi wa baraka ndani ya Kristo. Na ndio maana ukiwa ndani ya Kristo, wewe ni mbarikiwa tena kwa baraka zote za rohoni. ( Waefeso 1:3)


Hivyo wewe ni bora kuliko mali na fedha na utajiri wa dunia hii. Wewe ni mbarikiwa! Kipimo cha kujua nani kabarikiwa ni katika kumjua Bwana Mungu. Kweli pesa na mali ni moja ya matokeo ya baraka au matokeo ya Neema tu, au matokeo ya dhuluma! Na kwa sababu hiyo fedha na mali imebeba matokeo mengi, basi huwezi kusema moja kwa moja kwamba kila mwenye fedha na mali amebarikiwa, kwa maana wengine ni majizi tu! Ni vyema leo upate ufahamu kuhusu baraka ili wasikuchanganye hao wengine wanaojiita wamebarikiwa sivyo ndivyo!


Kuna wakati mwingine Mungu anaweza kuruhusu baraka zimfikilie mtu ambaye hamjui Mungu, Lakini hali hii huwa ni kwa Neema tu na kwa huruma za Mungu. Hali ya namna hii ikitokea ujue kuna mpango na kusudi maalumu la Mungu kwa mtu aliyebarikiwa nje ya Yesu. Kwa mfano Ishimaeli hakuwa mtoto wa agano, lakini Mungu alimbariki.


“ Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu.” Mwanzo 17:20

Lakini ni lazima ujue kwamba, tofauti kati ya Ishameli na Isaka sio ishu ya imani ( kuokoka au kuwa ndani ya Yesu) bali ni ishu ya agano la Mungu mwenyewe.


Haikuwa jitihada ya yeyote kati yao bali ilikwishapangwa na Mungu akawabariki wote wawili. Mmoja baraka nje ya agano na mwingine baraka ndani ya agano. Na hiyo ndio tofauti ya mibaraka yao.


Ingawa Ishimaeli alibarikiwa pia lakini ukweli ni kwamba baraka zao zilitofautiana sana. Hivyo;umuonapo mtu wa mataifa kafanikiwa usiogope kwa maana kufanikiwa kwake ni tofauti na kufanikiwa kwako hata kama yeye ana mali na fedha nyingi, hata hivyo hamuwezi kufanana bado. Baraka za mtu wa Mungu ni baraka za kipekee mno bali za wa mataifa ni kwa Neema tu!


Hata hivyo ukweli utabakia ukweli tu kwamba Leo ni tofauti kidogo kwa maana “ Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye BWANA“ Zab. 128:4

Mkazo wa baraka umeelekezwa kwa wale tu wamchao Bwana, waliompokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao. Watu wa namna hii, wamekwisha barikiwa tayari. Changamoto ni kuchukua baraka hizo na kuziweka kwenye maisha, lakini baraka zipo tayari.


  • Mfumo wa baraka.


Mungu ndie aliyeweka baraka kwa utaratibu wa mkubwa ambariki mdogo( Waebrania 7:7). Ukubwa unaozungumziwa hapa hauna maana moja kwamba ni mkubwa kimwili bali maana ya mkubwa kwanza katika kumfahamu Mungu. Mfano unaweza ukawa ni mtoto pekee uliyeokoka kwenye familia yako. Upo na kaka na dada zako pamoja na wazazi wasiookoka. Katika ulimwengu wa roho wewe ni mkubwa kuliko wao, na unayo nguvu ya kutamka mibaraka kwenye familia na ikiwa, kwa sababu mkubwa humbariki mdogo.


Lakini pia ukubwa unaweza ukawa wa umri kama baba au mama yako wana nafasi ya kubariki.

Ukiwa ndani ya Yesu, ujue umepewa nguvu hii ya kutamka mibaraka na mibaraka kuwa! Tumia vyema kinywa chako sasa! Mimi nimefanya hivi kutamka mibaraka ya kufaulu wanangu, na Mungu kanishangaza mambo yamekuwa hivyo.


Mungu yeye mwenyewe amebariki vitu vyote alivyoviumba kwa maana ni vyema sana. Mara nyingi tunasoma, Mungu alivyowabariki watu. Hizi ni baraka za moja kwa moja.


  1. Aina za baraka ;

  2. Baraka za wanadamu ( zinazotolewa na wanadamu kupitia kinywa.)

  3. Baraka za Kiungu ( zitokazo moja kwa moja kwa Mungu.)


01. Baraka za wanadamu. ( Watumishi wa Mungu katika kinywa) .

Fahamu ya kwamba kinywa chako kina nguvu ya kubariki au kulaani, inategemea unakitumiaje. Kumbuka baraka za namna hii utegemea maneno ya kinywa chako hasa ukiwa ndani ya Yesu;katika aina hii ya baraka tunaweza kuigawa kwenye makundi mawili;


a) Baraka juu ya vitu vitakatifu / vitu vilivyotengwa kwa ajili ya Bwana Mungu tu.


Ni pale ambapo mtumishi anapotamka baraka / anapobarikia dhabihu au sadaka. Vitu hivi vinaweza vikawa fedha, chakula, vyombo vy hekaluni / kanisani n. k mfano tusome “ mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona.” 1 Samweli 9:13. Mfano mchungaji anapotamka baraka kwenye kikombe cha ushirika (kwenye meza ya Bwana) pia ni baraka juu ya vitu vya Bwana (1 Wakorintho 10:16)


b) Baraka juu ya vitu vingine ( Mwanzo 27 sura hii Isaka akimbariki Yakobo), Marko 10:16 n. K


02. Baraka za Kiungu ( baraka za kiroho, moja kwa moja kutoka kwa Mungu mwenyewe)

Katika uumbaji wa Mungu alivibarikia vitu vyote maana vyote vilikuwa ni vyema sana ( Mwanzo 1:22,31). Na baada ya hapo Bwana Mungu akaibarikia siku na kuitasaka siku hiyo yamapumziko ( Mwanzo 2:3). Akabariki ;


  1. Kazi ya watu wake ( Kumb. 28:5, Malaki 3:11

  2. Watu wake walioKuwa Kwenye agano. (Mwanzo 9:1,Zab. 73:1 n. k)

  3. Taifa litakalo mcha Yeye, Mungu hana upendeleo ( Matendo 10:34-35)

  4. Afya, furaha na maisha ya amani ( Zab. 21:1-5) n. k


03.Baraka za Ibrahimu.


Hili ni somo linalojitegemea maana ni pana sana “Baraka za Ibrahimu” lakini kwa ujumla wake ni aina ya baraka inayotajwa sana kwenye biblia kwa maana ikiwa tu wakristo basi tumekuwa uzao wa Ibrahimu na warithi sawa sawa na ahadi ( Wagalatia 3:29). Ibrahimu alibarikiwa kwa sababu alikuwa amechaguliwa, pili alitembea na Mungu hata akahesabiwa haki kwa imani.


  • Baraka zinakujaje?


01.Kwa kumcha Bwana – Hapo Mungu ameamuru baraka ziwepo. Na ndio maana kubarikiwa halisi ni kukutana na Yesu!


02. Kwa neema ( kwa watu wachache) – Lutu alibarikiwa kuwa na mifugo mingi kwa Neema tu kupitia mgongo wa baba yake mkubwa Ibrahimu. Lutu hakuwa mwenye haki kiasi cha kupokea baraka, bali Ibrahimu alikuwa mwenye haki kwa imani, Ibrahim alipofanikiwa na Lutu akajikuta akifanikiwa ( Mwanzo 13:1-13).


Je wewe unataka kubarikiwa na Bwana?


Najua jibu ni “ndio nataka” basi anza leo kutengeneza mahusiano yako na Mungu. Hakikisha kama ulikuwa hujaokoka, okoka leo. Chukua hatua ya imani ya kurejea kwa Bwana ili mibaraka yako iwe dhahiri. Waweza kunipigia simu zangu kwa maelezo mengi pamoja na maombezi.


Ikiwa umebarikiwa naomba unijulishe pia.

Piga sasa kwa msaada zaidi;


namba hizi;+255 683 877 900


Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446


Mch. Gasper Madumla.


UBARIKIWE. 

Commentaires


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page