UCHUNGU NA UTUNGU – BUSTANI EDENI
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 27, 2017
- 5 min read

Na Mch.Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Imeandikwa “ Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Mwanzo 3:16
Baada ya Adamu na Hawa kuasi kwao pale bustanini,matokeo ya kuasi kwao yakachukua nafasi mara moja. Kumbe basi,kuna matokeo mabaya kwa kila dhambi uitendayo
Ujapomficha Mungu katika dhambi uitendayo kumbuka kwa Mungu upo wazi,kwa maana Yeye Mungu akujua mwisho wako hata mwanzo wako. Hivyo dhambi imesimamisha adhabu.
Kwa kuwa Mungu wetu ni Mungu afanyaye mambo yake katika uzuri na utaratibu,tunaona akizungumza na Adamu “ Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?” Mwanzo 3:11
Adamu badala ya kukubali kosa,na kutubu bali yeye akamlaumu mkewe kuonesha kwamba ndio sababisho la dhambi.Mwanamke ( Hawa) naye akashindwa kutubu naye akamtaja nyoka kuwa ndio kisababisho cha dhambi hiyo. Mungu alipofika kwa nyoka,hakuuliza bali alimtandika adhabu ya moja kwa moja. Kumbe hapo tunajifunza kwamba,;
01. Ukiwa umefanya dhambi yoyote ile,hutakiwi kujitetea mbele za Mungu bali unatakiwa ukubali kwanza na utubu kusudi usije adhibiwa. Leo wapo watu wanaoadhibiwa kwa sababu wanajitetea hali wao ni wadhambi wakubwa,mfano utakuta mtu yupo mbele za Bwana akiomba“ Bwana Mungu kwa kweli nimefanya kadha ndogo sana,lakini sasa tatizo ni mke wangu,maana mimi nilimwambia tusiibe ila yeye akaniambia tuibe….”
02. Nafasi ya toba ni neema ya hali ya juu- kulikuwa hakuna sababu ya Bwana Mungu kwenda kumuuliza Adamu na Hawa juu ya dhambi zao,bali angeliweza kuwaadhibu papo hapo. Bali tunaona Mungu akatoa nafasi ya toba kama neema,lakini wao akina Adamu hawakuitumia vizuri. Mpendwa umepewa nafasi sasa ya toba kama neema ya kurejea kwa Bwana kwa upya,tumia mlango huo wa toba,kwa sababu ni neema. Tubu sasa.
Baada ya nyoka kutandikwa na adhabu,sasa Bwana Mungu amemgeukia mwanamke na kumpa adhabu“ Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Mwanzo 3:16 Sasa tujifunze hapo;
Neno “hakika” maana yake ni“ ninathibitisha,kweli kabisa,ninakuhakikishia“. Hivyo Mungu akathibitisha kuongeza uchungu na utungu katika kuzaa kwa mwanamke.
Nini maana ya maneno haya mawili “ uchungu” na “utungu“?
Awali ya yote ni lazima ujue kwamba maneno haya ni maneno mawili tofauti kwa sababu kila moja limebeba maana tofauti,la sivyo yangelikuwa na maana moja basi kungelikuwa hakuna sababu ya kuyataja yote mawili.
Neno “uchungu” ile hali ya mateso ndani ya moyo,hali yakuumia kwa moyo kwa sababu ya…Au ni ile hali ya kubeba teso,chukizo,au duku duku ndani ya moyo wa aliyeumizwa. Hali ya uchungu haiji automatically/ moja kwa moja, pasipo kuumizwa moyoni. Mara nyingi uchungu ukikaa moyoni huleta maangaiko kiasi cha kutaka kujiua au kuua. Na uchungu ni mlango wa mapepo kwa sababu unashughulika na moyo wa mtu. Wengi waliobeba na uchungu wanakuwa ni watu wa visasi na watu wa hasira,wasiosamehe wengine.
Bali neno “utungu” ni ile adha,au mateso wakati wa mwanamke azaapo. Mateso ya namna hii yanasubiri mpaka wakati wa kuzaa kwa mwanamke. Hivyo ni hali ya kuumia,adha na maumivu makali sana lakini ni ya kitambo tu. Kama wewe ni mwanamke uliyezaa utanielewa ninazungumzia ni hali gani wakati wa kuzaa kwako ulikutana nayo. Utungu kwa kweli ni hali fulani isiyoelezeka kwa sababu inaumaa sana kwa kitambo cha kuzaa.
Hivyo Mungu akasema kwa mwanamke “ nitakuzidishia uchungu na kuzaa kwako;utazaa kwa utungu...” hii ikiwa na maana kwamba kama Mungu alizidisha uchungu (sio utungu) kwa mwanamke basi ni dhahili kabisa mwanaume nae alikuwa na sehemu fulani ya uchungu moyoni mwake. Kwa sababu kitendo cha kuzidisha kwa mmoja kina maana ya kwamba mwingine alikuwa naye anasehemu ila mwenzake amezidishiwa zaidi yake.
Ikiwa ni hivyo badi ni dhahili kabisa kwamba uchungu uliwavaa wote wawili kama roho. Na ndio maana tunaona Adamu na Hawa wakitoka katika uso wa Mungu wakiwa na roho ya uchungu ndani yao. Angalia hili,walipopata Kaini na Habili,Kaini akamuua Habili ndugu yake kwa sababu ndani yake kulikuwa na roho ya uchungu,na hapo uchungu ukaleta mauti ( Mwanzo 4:7-8)
Hata leo,uchungu unawazuilia wengi kumuona Bwana. Ni kweli uchungu ulizidishwa kwa mwanamke kuliko mwanaume na ndio maana tunaona uchungu unavyowakalia wanawake wengi wasiookoka. Mapepo mengi huingia kwa mlango huu wa uchungu,tazama wimbi la wadada/wanawake walivyokamatwa na uchungu. Hata wanaume leo hii wana uchungu mioyoni mwao. Sijajua kwako kama bado unasumbuliwa na roho hii.
Na kwa habari ya kuzaa kwa utungu,tunaona mwanamke akitoka mbele za Bwana na kifungo hiki cha utungu katika kuzaa kwake. Inawezekana kabisa sula la kuzaa halikuwa na utungu bali Mungu aliweka njia yake ya kuzaa bila hayo mateso. Biblia inaeleza kwamba utungu unahusishwa na mateso yapatikanayo wakati wa kuzaa kwa mwanamke
“Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia.” 1 Samweli 4:19
“ Wakasafiri kutoka Betheli, hata ukabaki mwendo wa kitambo tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa kuzaa, na utungu wake ulikuwa mzito.Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu, mzalisha akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine.” Mwanzo 35:16-17( Soma pia; Wagalatia 4:27,Zab 48:6,Ufunuo 12:2,Isaya 13:8)
Wanawake wa ndoa za agano la kale waliishi chini ya adhabu hii ya uchungu mioyoni na utungu katika kuzaa kwao. Haikuwa mpango wa Mungu mwanamke apitie machungu na utungu,bali dhambi isiyotubiwa ndio sababisho kuu.
Tukiyatazama mambo haya mawili “uchungu na utungu” katika mtazamo wakiroho tunagundua ya kwamba yote ni roho. Uchungu ni roho iletayo mauti na maangamizo,bali utungu uleta mateso kwa kitambo na kupokea ahadi njema.
Mfano,yeyote mwenye uchungu ndani ya moyo wake,hukusudia mabaya,tena huongozwa na hila na kukosa amani/raha au faraja ya moyo. Angalia ikiwa wewe umekwazwa na kukwazika tena hatimaye ukambeba mtu aliyekukwaza moyoni mwako,basi utapitia mateso ya kutokuwa na furaha wakati wote haswa pale umuonapo mtu aliyekukwaza.
Lakini kwa habari ya utungu,(kwa sababu utungu unahusiswa na mimba wakati wa kuzaa) unakufanya upitie mateso fulani makali kwa muda huku hukitaraji kuzaa kitu chema. Mfano; unaweza ukawa una mimba ya huduma fulani ya Mungu labda unataka ufungue kituo cha watoto yatima,au shule,sasa kwa sababu bado hujafungua;huduma hiyo inakuwa mithili ya mimba ndani yako. Sasa,ili uweze kufikia lengo lako unahitajika uzae na hapo ndipo utungu huja.
Angalia; kitendo cha kuhangaika kufunga na kukesha kuomba,tena na kuanza kutafuta pesa ni sawa na utungu kwa muda tu kisha hatimaye na huduma uanzishwa kama vile mwanamke mwenye mimba uteseka kwa kitambo tu,hatimaye muda si mrefu hukumbatia mwana.
Habari njema;
Ujio wa Bwana Yesu ameleta neema ya wokovu kwa kila aaminiye. Watu wote si wanawake wala si wanaume bali wametengwa mbali na roho hii kwa njia ya kumpokea Bwana Yesu awe Bwana na mwokozi wetu. Adhabu ya uchungu haina tena nafasi kwako ikiwa utampokea Yesu,yaani utaokoka na kufuata yote Mungu akuagizayo. Mwanamke aliye nje ya Yesu amejawa na uchungu,bali akiokoka Yesu anashughulikia adhabu hiyo
Hata utungu wakati wa kuzaa kwa mwanamke. Ukiokoka vizuri na kusimama wokovuni,basi Yesu upunguza utungu wakati wa kuzaa. Mwanamke aliyeokoka vizuri anaweza kuingia LEBA na kutoka chap chap huku akiwaacha wanawake wenzake katika utungu mkali.
Mpokee Yesu sasa naye atafuta adhabu hii,waweza kunipigia kwa simu zangu hizi ; +255 683 877 900
What’s app number ni+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Σχόλια