UCHUMI ULIOKAMATWA NA SHETANI.
- Mch. Gasper Madumla
- May 29, 2019
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Kuwa na maisha ya hofu ya Mungu,kuwa na ushindi maeneo yote pamoja na kuwa na amani na ``utoshelevu wa kimapato” ndio hasa mpango wa Mungu kwa kila mwamini. Lakini ukweli ni kwamba wengi hatupo kwenye maisha hayo,Kwa nini basi hatufikii kuwa na maisha ya utoshelevu hali tumeokoka? Ukiliangalia jambo hili kwa ukaribu,utagundua mambo mengi yanayosababisha,katika hayo yote huwezi kukosa kuona “hila za shetani ” zilizoachiliwa kwa lengo la kukamata uchumi wako. Wimbi la umaskini linapiga watu wengi,na wengi wao wamejikuta wakikosa furaha ya kutumika kwa Bwana ingawa hatutakiwi kupoteza furaha kwa sababu ya ukura. Nami najaribu kuangazia eneo moja tu,la kiroho kile kinachoendelea sasa;Biblia inasema “ Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie Bwana; kondoo zenu na ng’ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi. ” Kutoka 10:24
Farao alikuwa ni mwiba kwa Waisraeli,mtu ambaye alikuwa na ni mungu-mtu,akiabudiwa yeye pamoja na miungu yake,mwenye moyo mgumu tangia mwanzo wake. Alikuwa tanzi kweli kweli kwa Waisraeli. Kipindi Mungu amemtuma mtumishi wake Musa ajihudhurishe mbele ya Farao,kumtaka awape ruhusa ili Waisraeli waende zao kumfanyia Bwana Mungu mkuu ibada. Farao baada ya kupigwa kwa mapigo mengi,safari hii,Farao anawaruhusu lakini akizui mali za Waisraeli. Kitu gani Farao alikuwa akifanya? Bila shaka alitaka watu wa Mungu wasitoke na mali au uchumi wao,waende mikono mitupu wasije wakatokomea huko,hivyo watoke lakini waziache mali,kwa maneno mengine Farao alikuwa ameshikilia uchumi wao,kwa lengo la waende wakiwa mafukara!!!!
Kumbuka “kitabu cha Kutoka” kinaelezea namna ya watu wa Mungu walivyotoka utumwani kuelekea katika nchi ya ahadi ni sawa na sasa,mtu kutolewa kwenye utumwa wa dhambi na kuingia kwenye wokovu (Wakolosai 1:13-14). Sasa unaweza ukatoka na kwenda wokovuni hali shetani akiwa bado ameshikilia uchumi wako,lengo lake uishi katika ufukara hali haupo katika ufukara kwa maana Kristo alikukomboa kutoka kwenye ufukara kama laana (Wagalatia 3:13,29). shetani anaweza kukamata uchumi wako,kwa lengo baya la kukuangusha kwa maana anajua ukiishi kwenye ufukara kwake ni furaha na ni njia ya kukufanya unyonge!!!
Farao alikuwa akijua shida watakayoipata ikiwa kama watatoka bila uchumi,shida ya kwanza itakayowapata ni;
Wangeweza kurejea nyuma.
Wangetembea kwenye manunguniko.
Ukweli ni kwamba uchumi wako ukikamatwa na adui, unaweza ukaanza kuyafikiri mambo ya Misri (mambo ya zamani kabla ya wokovu wako),lakini pia kulalamika kunakuwa ni sehemu ya maisha yako kitu ambacho hakitakiwi kuonekana kwa mwana wa Mungu. Farao alikuwa na akili ingawa akili zake zilikuwa hazina akili,yeye Farao alikuwa akijitahidi kushikilia sehemu kubwa ya ardhi. Anajua kuna nini kwenye ardhi. Leo wapo watu kama Farao ambao wameshikilia ardhi kubwa si kwa wizi bali kwa akili ili kusudi watoto wa Mungu wakose,au la wakipata basi iwe ni padogo sana. Katika hili,shetani ametufunga walokole/watoto wa Mungu wengi,kwa maana kweli tumeokoka lakini bado tumefungwa akili zetu,hatuoni umuhimu wa kukamata ardhi kwa maendeleo yetu dhidi ya waovu.
Labda nikuulize,hujawahi kuona watu wasiomjua hata Mungu,lakini wamekata ardhi kubwa,na mahali pengine wamejenga mashule,hospitali ndani yake migahawa ya chakula,n.k. Sasa kwa namna yoyote itakulazimu wewe unayemjua Mungu,kuwaendea watu kama hao,pale utakapoumwa utajikuta upo mikononi mwao,au pale unapotaka mwanao asome utajikuta upo chini yao tu. Sisemi ni dhambi kuwaendea,lakini inapaswa kwa sasa uchumi ukamatwe na watu wa Mungu,na watoto wetu wasomeshwe na watu wenye hofu ya Mungu. Hilo ndilo jambo la msingi!
Nikiangalia dunia inapoelekea ninaishia kusema ``Ee Bwana utusaidie sisi walokole!!” Ebu angalia mkono wa adui ulivyokamata uchumi wa leo! Hali inatisha kwa kweli. Fikiri wakati mkristo anapanga awe na mtoto mmoja au wawili kama wazungu,wakati huo huo wenzetu wa imani nyingine wana watoto 8 na anapanga aoe mke mwingine ili aendeleze uzazi! Sasa miaka 30 ijayo,tutakuwa wapi? Je uchumi wetu utakuawaje?. Ebu angalia maisha ya magharibi/ulaya ya leo. Wakristo hawapo busy na Mungu wao,bali busy na mambo yao hata imefika wakati makanisa yao yakiuzwa au kukodishwa,na cha ajabu sana watu wa imani nyingine ndio wanachukua nafasi hizo taratibu taratibu. Uchumi umekamatwa na adui!!!
Lakini kwako wewe,ambaye unaona kila ulifanyalo kwa kweli haufanikiwi kana kwamba unapiga hatua mbili mbele kisha unarudi nyuma hatua tatu! Basi ni lazima hali hiyo ishughulikiwe sasa,kwa njia ya “maombi na maombezi “. Kwa maana uchumi wako bila shaka umekamatwa na adui tu. Najua zipo sababu nyingine nyingi,lakini shetani pia huwezi kumkosa hapo! Ni vyema tukaanza mchakato huo wa maombi na maombezi leo,na kuongea mengi zaidi ambayo sikuweza kuyaandika.
Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe- Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI pigia kwa simu zangu hizi ; +255 683 877 900
What’s app namba .+255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments