UCHUMBA ~ 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 22, 2019
- 4 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Hali ya binti kuposwa na kijana wa kiume kwa lengo la kuolewa huitwa “ uchumba “. Uchumba unahusisha na ahadi ya ndoa kati ya wawili waliopendana kwa hiari yao wenyewe. Neno “ahadi ya ndoa” ni neno muhimu sana katika uchumba, na kwa kuwa ni muhimu sana neno hili uwakilishwa na “pete” kama ahadi ya ndoa inayotazamiwa hivi karibuni.
Tamaduni za kale zimebadilika ukilinganisha na tamaduni na mila tulizonazo leo. Zipo tamaduni na mila nyingi zinazoeleza mambo ya uchumba, lakini hata hivyo biblia Kama dira na mwongozo wetu, haikunyamaza katika eneo hili la uchumba. Ingawa hatuoni mara nyingi mambo ya uchumba na ndoa kwenye biblia, lakini yalikuwapo.
Uchumba wa Isaka na Rebeka ( Mwanzo 24:50-54)👫
Hili ndilo tukio kubwa na la kwanza la uchumba lililorekodiwa kwenye biblia. Kwa mara ya kwanza tunaona utaratibu wa kutafuta mke, kuposwa, suala la maali, pamoja na ndoa likitajwa kwenye biblia. Ingawa utamaduni wa leo umebadilika kwa sababu ya utandawazi, lakini bado tunalo la kujifunza tunaposoma biblia kwenye Mwanzo 24 yote.
Biblia inatuambia kwamba Ibrahimu kama mzazi wa kijana aitwae Isaaka. Aligundua kwamba kijana wake amefikia umri wa kuoa. Kwa maana kila alipomwangalia alijua kwamba kijana anahitaji mwenzake. Biblia haituambii kwamba Ibrahimu alimuuliza Isaka kama anahitaji kuoa au lah! Lakini bila shaka! tunajua Ibrahimu kama mzazi anajua wakati sahihi wa kijana wake kuoa.
Hata leo, ukiwa kama mzazi unajua wakati wa kijana wako kuoa au kuolewa. Sio mpaka uambiwe bali ukimcheki tu binti yako, unaona kabisa anahitaji kuolewa. Hata kijana wako wako wa kiume, ukimcheki jinsi alivyo alivyo unagundua huu ndio wakati wake au bado si wakati wake. Hivyo, kumbe upo wakati wa kuoa /kuolewa na kuna wakati usio wa kuoa/kuolewa.
Mzazi ndiye anayepaswa kwanza kujua nyakati hizi, na sio mtoto. Kwa sababu unapomchunguza mtoto kqa ukaribu utagundua ni wakati gani alio nao. Na hapo unaweza kumshauri ili asije akakosea (labda asije akakosea kama wewe ulivyokosea, leo ni kujuta). Kama mzazi utachelewa kujua jambo hili, utasababisha mtoto kukosea!!! 😭😭😭
Hivyo Ibrahimu akampeleka mtu aende kumposea binti kijana wake. Maana alijua binti gani anayestahili awe mke wa mwanaye. Si kila binti alistahili kuolewa na Isaka, bali kulikuwa na kigezo ambacho ni binti wachache tu ndio walikidhi vigezo hivyo. Maana Ibrahimu Ibrahimu alimwagiza mposaji (mshenga) akisema ;
“ nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao;bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.” Mwanzo 24:3-4
Ibrahimu anajaribu kumpa maelekezo sahihi ya mke anayetafutwa kwa ajili ya mwanae Isaka. Kigezo cha kwanza anasema kwamba binti ni lazima atokee kutoka kwa ndugu zake wala sio kwa Wakanaani. Hii aina maana kwamba kwa Wakanaani hakukuwa na mabinti warembo, wazuri bali walikuwepo lakini mabinti hao walikuwa ni waabudu sanamu/ hawana Mungu wa kweli /watu wa mataifa.
Hivyo sifa ya mchumba anayepaswa kuolewa na Isaka mtu wa Mungu anapaswa awe ni mtu wa Mungu pia. Je leo unapotafuta mchumba, unatafuta tu mtu yeyote? Unajua madhara yake ya kuwa na mchumba mmataifa? Usiombee nakwambia!!! Nenda kawaulize waliofunga ndoa wa watu wasiookoka, uone ndoa yao ikoje🏃🏃🏃
Lakini ebu angalia vizuri tena, na utagundua Isaka hakufanya jitihada yoyote ya kumtafuta mchumba, bila shaka aliomba kwa kuwa mzee wake ni mtu wa agano, hivyo inawezekana waliomba lakini Isaka alitafutiwa mchumba hatimaye akawa mke. Leo vijana hawataki kutafutiwa mchumba, wanaona ni mambo ya kizamani. Hivyo wanajikuta wakikosa hata kushauriwa kwa maana mambo yote wameyafanya wao wenyewe wenyewe. Kumbuka, mzazi /mlezi wako ana yajua hayo mambo kabla yako, mzee wako ni muhimu kumshirikisha. Wakati mwingine atakushauri na utajikuta ndio unapona kwenye tatizo la huyo unayemwona wewe ni mzuri.
Bahati mbaya leo, mambo yemebadilika kwa maana vijana hutafuta wachumba hata kwenye mitandao ya kijamii Sasa, sijui mchumba aliyepatikana kwenye mtandao kama ataweza kuwa ni mume/mke mwema? Sijui??? Inategemea kwa kweli, lakini uwezekano wa ubaya ni mkubwa sana!
Biblia inatuambia baadhi ya sifa alizonazo Rebeka aliyechumbiwa. Kwanza alikuwa mzuri na bikira, yaani hajui mume. Alikuwa mnyenyekevu ( Mwanzo 24:15-20). Lakini hata hivyo Rebeka mrembo wa watu alikuwa mchapa kazi maana biblia inatuambia alikuwa akienda kuteka maji ya familia. Sifa hizi chache zilizoandikwa, vipi leo? Unaziangalia unapotafuta mchumba? Leo, ni ngumu kidogo kuziona sifa hizi kwa kijana au binti.
Ni kweli wapo warembo wengi lakini mhh! Mabikira wachache!!! Au wapo wakaka wengi lakini mhh!! Wamekwisha tumika sana!!! Tena wapo vijana lakini ni wavivu kupindukia, kazi yao ni kupaka kucha rangi, au kunyoa kiduku kwa wakaka.!!! Jiulize mchumba wako yupoje? Anasifa hizi??? Kama hana kuna kazi mpendwa ya kufanya!!! 🏃🏃🏃🏃
Hakuna kitu muhimu sana kwako kama kuwa na mchumba ambaye ni sahihi. Ni muhimu kujua sana habari ya uchumba! Biblia inatuambia Isaka alikutana na Rebeka kimwili pale tu walipokuwa ndani ya ndoa. Umeona hilo? Hii inafudhihilishia kuwa;
Uchumba sio ndoa. 👰
Wako watu ambao ni “wachumba sugu” huu ni mwaka wa 4 sasa, na unaelekea mwaka wa 5 bado ni wachumba tu. Wengine kuzaa na wamezaa bado ni wachumba. Sasa uchumba wamegeuza na kuita ndoa, yaani kila mmoja anasema, mume anasema“mke wangu huyu.. , ” na mke anasema “mume wangu huyu… ” hivi kweli, unathubutu kuharalisha ndoa wakati hata mahali hujamaliza!!!
Au hata mahali hujatoa!!! Jamani, unasomaga biblia gani hiyo usiyoeleza mambo haya? Fahamu tu, uchumba sio ndoa. Kama uko na mtu kwa muda wote huo, ujue Mungu hapendi na anakuona katika uzinzi wako unaoufanya kila siku.!
Tatizo liko wapi? Huna pesa ya kuoa au huna nyumba? Na ni nani huyo aliyekuambia kuoa ni pesa? Au kuoa ni gharama? Usichanganye na neno “harusi” kwa maana harusi ndio gharama, lakini ndoa haina gharama, ndoa ni ya Bwana hapo kanisani bali harusi ni “mbwembwe “ zako mwenyewe. Unaweza usifanye mbwembwe hizo, na bado ndoa ikawa nzuri tu….
ITAENDELEA…
Ikiwa kama umejifunza kitu, nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
What’sapp namba .+255 746 446 446
Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments