TAFUTA AMANI NA WATU WOTE.
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 23, 2017
- 3 min read

“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” Waebrania 12:14
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Miaka fulani iliyopita nilikuwa nikitafuta kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba yangu niweze kuishi mimi na familia yangu. Unajua tena,kupanga kulinichosha maana nilipokuwa nimepanga nilijihisi kana kwamba nipo utumwani Misri hali nimeokoka. Wakati nilipokuwa nikitafuta kiwanja nilijikuta nikikosa kiwanja katika sehemu nyingi nilizoenda,wakati mwingine pesa ilipungua na wakati mwingine nilikosa amani na huko nilikopelekwa.
Baada ya kutafuta tafuta nikajikuta nimefanikiwa kupata kiwanja. Nami nikamshukuru Mungu kwa hilo,hivyo nikaona sasa mambo ni shwari tayari kwa kujenga na mapema niamie. Lakini eneo lenyewe nililopata nikagundua nimepata eneo lenye watu wengi wa imani nyingine ( Waislamu na wa imani nyingine za kikristo wasiokoka)
Nami nikajikuta nimejenga hapo. (Kwa wale wanaofahamu sehemu moja inaitwa Mbezi-Kwemba alimaarufu kijijini au msikitini watakuwa wanaelewa ninachozungumza kwamba ni watu wa namna gani waliopo huko kwa miaka ya nyuma,ingawa kwa sasa wakristo wengi wameongezeka na makanisa yamejengwa)
Sasa nikajenga huko na kuamia na familia yangu kutoka Kimara. Kumbuka hapo nilipojenga ndipo nilipozungukwa na watu wa dini nyingine wanaokataa maswala ya kikristo na ni watu wa kubeza ukristo hususani ulokole wangu. Sasa nikiliangalia neno la Mungu linaniambia “ niwe na amani na watu wote,yaani waislamu,wakristo na wapagani wote” mh!!!
Unajua Neno la Mungu ni gumu hasa kuliweka katika matendo ingawa ni jepesi sana ukisaidiwa na Roho mtakatifu, lakini Neno la Mungu ni amina na kweli yaani halijawahi kudanganya; sasa kazi ipo kulitekeleza hilo neno. Kwa neno hilo,mpaka sasa sijawahi kugombana na mtu wa imani nyingine yoyote ile bali tunaishi kama ndugu hali tumetofautiana sana imani zetu. Nami najizoeza kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na watu wote kama alivyosema mtume Paulo ( Matendo24:16)
Kati ya jambo gumu ambalo mara nyingi watu wanaanguka na kumkosa Mungu ni hili la “kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu” mimi ninasemaga kwamba mkristo aliyeokoka yeyote akifanikiwa kufaulu katika eneo hili basi hakika atakuwa ameokoka sawa sawa.
Biblia inaposema “ tafuteni kwa bidii kuwa na amani na utakatifu” ina maana ni jambo gumu ndio maana unaambiwa “tafuta”. Siku zote unapoambiwa tafuta kitu fulani ina maana kitu hicho kipo mahali fulani lakini hakionekani/hakipatikani kwa wepesi bali ni katika kutafuta yaani kukubali kulipa gharama ya muda wa ziada ( kuacha kazi na kufanya kazi).
Hivyo;Si kazi ndogo uwe na amani na watu wote. Maana kuna watu wengine wamesimama kama makwazo kwako na watu hao sio waamini katika Kristo Yesu,lakini biblia inakutaku uwe na amani nao. Kitendo cha kuwa na amani na watu wote ni kitendo cha kukubali kulipa gharama,katika kuudhiwa ,kukasilishwa lakini pasipo kurudisha kisasi bali kuvumilia yote.
Na hapo ndipo wakristo wengi wa siku za leo hushindwa. Leo hii,watu wengi wamekuwa na amani na kwa watu wale tu ambao wanaotembea pamoja yaani wanaofanana kiimani. Kumbe thamani ya wokovu wako ni pale utakapoweza kuwa na amani na watu wote pasipo kuangalia itikadi za imani yao,kabila wala rangi zao pamoja na kuutafuta utakatifu.
Utakatifu unatafutwa,hauji kwa neema bali ni kwa kutafuta kila siku. Mtu hawezi kuwa mtakatifu akiwa amekosa kuwa na amani na watu haswa wale wa nyumbani kwake anapoishi,wale ndugu au jirani zake. Biblia leo inatuambia kitu kikubwa sana kwamba huwezi kumuona Mungu pasipo huo utakatifu. Hii ni sawa na kusema si wakristo wote watakaomuona Mungu pasipo huo atakatifu.
Ukiliangalia kwa ukaribu neno hili katika Waebrania 12:14,utagundua kwamba unayo kazi kubwa ya kufanya katika imani yako mbele za Mungu kwa maana kweli kabisa ukifaulu katika neno hili basi wewe hakika utakuwa umeokoka kweli kweli.
Lengo kuu la ujumbe huu,ni kukumbusha kazi/wajibu ulionao wa “kutafuta kwa bidii amani na watu wote pamoja na utakatifu” . Lakini ukumbuke kwamba huwezi kuyafanya haya bila Roho mtakatifu kukusaidia. Na ukumbuke pia Yeye Yesu Kristo ndie mfalme wa amani. Hivyo wewe unayetaka kuwa na amani na watu wote huna budi kwanza kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wako,kwa maana ukimpokea Yeye,umeipokea amani ndani yako.
Kwa msaada zaidi na maombezi,piga sasa+ 255 683 877 900
What’s app ni+255 746 446 446
Mch. G.Madumla
UBARIKIWE.
Comments