SIRI YA KUSTAWI KATIKA MWAKA MPYA
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 31, 2019
- 4 min read
Updated: Sep 29, 2022

Kipindi cha miaka ya nyuma hivi, nilipokuwa nikisoma shule ya msingi ya Sinza- Dar,kwenye moja ya bustani ya maua ya shuleni hapo,tulikuwa na maua fulani tuliyoyaita “ maua ya saa nne“. Moja ya sifa kubwa ya maua haya ilikuwa ni kunawili kwa muda fulani hivi wa kama saa nne asubuhi hadi saa sita sita hivi za mchana wakati mwingine hadi saa saba za mchana,lakini baada ya muda fulani tena yanasinyaa na kupoteza uzuri wake kwa gafla. “Ninayakumbuka maua ya saa nne” kwa sifa yake nzuri ya kupendeza,ingawa yalipendeza kwa muda tu!!! Maua haya yamenifundisha kitu kwenye maisha tu ya kawaida,kwamba kuna vipindi tofauti tofauti,kama vile kuna kipindi utastawi na kipindi cha kutindikiwa. Lakini hakuna mtu awaye yote mwenye kupenda kutindikiwa,bali kila mmoja hupenda kustaajabu!
“Maua ya saa nne” hupendeza wakati wa jua kali!
Katika maisha ya kila mtu,kuna vipindi mbali mbali. Lakini vipindi vyote vinajumuishwa na vipindi viwili tu “ kipindi cha jua kali” na “ kipindi cha kivuli kizuri” katika vipindi hivi,vimeruhusiwa kwako,na razima upitie. Kile kipindi cha jua kali ndipo kuna kupungukiwa hata kuhidi kwamba umeachwa na Mungu. Lakini kwenye kipindi kama hiki cha jua,hapo ndipo maua ya saa nne yenyewe yanashamiri,na kuonekana yakipendeza. Hii ni neema ya ajabu! Ikiwa maua ya kawaida yanaweza kupendeza katika jua kali,wewe pia unaweza kustawi na kupendeza kwenye kipindi kigumu. Lakini nini siri ya kufikia kushamiri hasa katika mwaka mpya?
Mruhusu Yesu awe Bwana wa maisha yako.
Hii ndio siri kubwa yenye kubeba siri zote za kustawi katika mazingira ya jua,lakini pia katika kipindi chote cha mwaka mpya. Neno “bwana” huonesha mtawala / yeye anayemiliki. Watawala wa zamani walikuwa wakiitwa “ma-bwana“. Mtu ambaye yupo chini ya bwana,huyo ni mtumwa. Sasa, mtumwa hana sauti,wala maamuzi yake binafsi isipokuwa hufuata yale yote ayanenayo bwana wake pasipo kuhoji hoji. Maisha ya mtumwa yameuzwa kwa bwana wake,kwa maana bwana wake ndiye anayekula muda,nguvu na mawazo ya mtumwa wake. Wakati mwingine mtumwa hupelekwa asikopanga yeye au asipopataka n.k. Katika wokovu,Kristo naye ni “ Bwana” amechukua sifa za “ bwana “.
Hii yote ni kuonesha kwamba yeyote aliye chini yake hana tofauti na mtumwa, ingawa ni mtumwa wa haki. Kwa hiyo,mtu wa Kristo,ameyauza maisha,muda na nguvu zake kwa Kristo Yesu. Hii ikiwa na maana hata maisha yake yote yanatawaliwa na Kristo ipasavyo. Mtumwa wa namna hii,kustawi ni haki yake isiyopingwa! Ebu jifunze mifano michache ya watumwa wa haki waliouza maisha yao kwa Kristo. Mtazame mtu kama Paulo, mtu aliyeona hasara juu ya mambo yake,naye akakubali kuyapoteza yote kusudi ampate Kristo.
Biblia inasema;
“Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;” Wafilipi 3:8
Paulo hakuona maana ya kushikiria mambo yake binafsi,ambayo yangemnyima nafasi Kristo kwenye maisha yake. Alipogundua hivyo,hakuona shida kuyapoteza mambo yote ili kusudi ampate Kristo. Paulo anajaribu kukueleza kwamba alimruhusu Kristo kuwa Bwana halisi kwenye maisha yake yote. Katika hili pekee,tunajifunza kumbe inawezekana “kuyapoteza mambo yote yanayokuzuilia hasa kuzulia nafasi ya Kristo kwenye maisha yako ”
maana inawezekana. Sasa cheki utume wa Paulo ulivyofanikiwa! Kwa maana alikubali kuwa mtumwa wa Bwana. Na hii ndiyo,shida ya walio wengi kwamba watu hawajakubali kuyapoteza mambo yao binafsi,na huku wanataka kustawi! Wengine husema Kristo ndiye Bwana na mwokozi wa maisha yao! Lakini ni kwa maneno tu,hali hawajakubali wao kufanyika watumwa na Kristo awe Bwana halisi kwa mfano wa bwana na mtumwa wake.
Kuna kipindi fulani Yesu aliwafundisha wanafunzi wake siri ya kustawi na kufanikiwa. Alihakikisha wanafunzi wake wote wanakuwa jangwani mahali ambapo hawawezi kupata chakula popote pale. Yaani hawawezi kutegemea akili zao binafsi,ili awafundishe kitu. Na hapo nyikani palikuwa na makutano mengi waliokuwa wana njaa,biblia
inasema;
“Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili.Akasema, Nileteeni hapa.“ Mathayo 14:16
Mikate mitano na samaki wawili hawakuwa kitu kwa wanafunzi,lakini Yesu aliitazama mikate hiyo hiyo,na akaona kushiba kwa kusanyiko lote tofauti kabisa na walivyotazama wanafunzi. Lakini hayo yote hayakuwezekana ni mpaka mikate na samaki hao walipopelekwa kwa Bwana. Kufanikiwa kuwalisha makutano hayo yote,kulihitajika Kristo ahusike kikamilifu. Hii yote alikuwa akifundisha kwamba, siri ya kustawi ni kumuhisisha Yesu katika kila ulichonacho,inawezekana kikawa ni kidogo sana,lakini takata nikwambie ukikipeleka kwa Kristo Yesu, si kidogo hicho.
Siri nyingine nyingi zipo,lakini zote zinamezwa na siri hiyo ya Kristo afanyike Bwana halisi kwenye maisha yako. Kuna siri kama ya “ kujiwekea malengo,kufanya kazi kwa bidii,kuwa mtoaji,n.k” lakini yote hayo hutegemea uwepo wa Bwana maishini mwako. Si jambo dogo la Kristo kuwa Bwana wa maisha yako. Maana yake,katika kila unachotaka kufanya ni lazima umuhusishe yeye kwa kumwomba ruhusa kufanya ama usifanye.
Ukiwa mtumwa wa haki, akili zako hazina matunda ! Je uko tayari kukubali kustawi katika mwaka mpya wote,ikiwa jibu ni ndio,basi kubali pia kupoteza mambo yako binafsi kama vile ratiba zako,na ruhusu ratiba ya Mungu ichukue nafasi kwenye maisha yako.
Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,nifahamishe tumtukuze Bwana pamoja.
Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga + 255 683 877 900
What’s app namba + 255 746 446 446
Heri ya sikukuu ya Kristmas na mwaka mpya. Chaoo!
Na Mch. G.Madumla.
Comments