top of page

SIRI YA KUINULIWA NI KUNYENYEKEA.

Shalom…

Kwa ufupi,

“Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” 1 Petro 5:6

Neno linaeleza siri kubwa ya kuinuliwa kwako kuwa ni kunyenyekea tu. Na hiyo ndio siri yenyewe. “ kunyenyekea” ni kujishusha / kutumika sio kutumikiwa / kukubali uonekane mdogo hata kudhaulika kwenye macho ya jamii. “ kunyenyekea ” si suala la maigizo kusema uigize kwa kujifanya siku moja wewe unanyenyekea. Wala si suala jepesi,bali kunyenyekea kuna gharama ya kukubali dharau,kusemwa,n.k

•Kumbuka;

Kunyenyekea ni tabia ya Yesu Kristo,ambaye Mungu alimwinua / alimwadhimisha jina kuu lipitalo majina yote,Jina la Yesu ( Wafilipi 2:8-11). Yesu alinyenyekea sana kuliko mwanadamu yeyote. Ilikuwa ni kwa ajili ya kutufundisha namna itupasavyo kutembea na Mungu. Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi ambapo kiburi ni tabia ya shetani.

Leo,tumekuwa na maombi mengi tukimtaka Bwana atupandishe kihuduma,kikazi,kiafya n.k na papo hapo tumeshindwa kuwa “wanyenyekevu” . bahati mbaya mara nyingi tunapongundua kwamba hatujainuliwa basi hapo ndipo tutaanza yale maombi yetu ninayoyapendaga “maombi ya kuvunja na kuhaharibu kazi za shetani” tukidhania kwamba shetani ndio muhusika pekee wa kutufanya tusiinuliwe. Ni kukosa maarifa ya kiungu,kwa sababu si shetani ndie muhusika pekee kwa kushindwa kuinuliwa,bali shetani anachangia sehemu tu,na sehemu inayobaki ni wewe mwenyewe unachangia,kwa sababu “umeshindwa kunyenyekea “

Laiti mtu mmoja leo atatambua siri hii,kisha kuifanyia kazi,kwa kunyenyekea mahali alipo. Hakika atapandishwa. Kuna msemo wa kiswahili mimi huwa napenda kuutumia kwamba “mwanamke anayenyenyekea kwa mumewe,ndiye atakayemtawala mumewe” Hii ikiwa na maana ; mtu yeyote kwenye uhusiano akijishusha,ujue huyo ndiye atakayekuwa boss wa mwenzie. Jiribu sasa uone hili !

Kuinuliwa ni sehemu yako katika jina la Yesu, lakini ni lazima ujifunze kunyenyekea. Mfano; mahali ulipo katika huduma = ukifanikiwa kuwakubali watumishi wengine na kukubali kuketi na kufundishwa,kisha ukakubali kutii yale uliyofundishwa,ukajiona na wewe ni mwanafunzi wa kawaida tu- hapo Bwana atainua huduma yako,Bwana atainua karama yako,na hakika utainuliwa.

Bali ukweli ni kwamba leo,watu hawajainuliwa bali wamejiinua wenyewe,kisha na kujipachika majina ya ajabu ajabu wakidhani kuwa wameinuliwa,lol mbaya hii!!!! Je hujawai kuwaona watumishi ambao wana majina makubwa makubwa tofauti hata na kazi wazifanyazo? Ebu mtazame Yesu ambaye ndiye mfano na kielelezo chetu. Yeye aliikubali kuitwa,(sio kujiita) “Rabi / mwalimu ” basi,hivyo na yatosha. Ingawa ana majina mengi. Je leo hali ikoje wa watumishi?

Ebu angalia tena – katika eneo unalofanya kazi zako za mikono – endapo utakubali kujishusha,na kuwatanguliza wenzako yaani kunyenyekea, je hutapendwa na wakuu? Je hutainuliwa? Ukweli ni kwamba utainuliwa tu,maana umenyenyekea.

Nilikuwa najiuliza,nifanye nini ili niinuliwe? Nimegundua siri hii kumbe kikubwa ni kunyenyekea ndio siri yenyewe. Katika andiko letu hilo ( 1 Petro 5:6) Paulo anazungumza jambo la ajabu sana kwamba kumbe kuinua watu ni tabia ya Mungu,naye huwainua watu wake kwa wakati wake. Neno halituambii kwamba Mungu huwainua watu kwa mipango ya watu,bali kwa wakati wake Yeye mwenyewe. Hij ni sawa na kusema,unaweza ukajitahidi na kuomba lakini ujue ikifika wakati wa Bwana, atakuinua na hakuna awezaye kukuzuia kwa sababu ni wakati wa Bwana. Lakini, unyenyekevu ndio funguo muhumi sana.

Ninawezaje kunyenyekea ?

Ikiwa kunyenyekea ni tabia ya Yesu, basi huna budi kumwomba Roho mtakatifu akupe tabia / moyo huo. Kisha anza mazoezi mara moja ya kuwatanguliza wenzako nawe ukubali kufundishwa. Ikiwa unahitaji kuwa mnyenyekevu mzuri,hakikisha usije ukajipachika majina yoyote ya ajabu ajabu,penda kuwa wewe halisi. Tambua wewe ni wa pekee,hivyo hakuna sababu za kujitafutia njia ya kutaka kujulikana au kusifiwa. Anayepaswa kusifiwa ni Mungu tu. Ukitambua hilo utaogopa hata kujisifia.

Ikiwa fundisho hili limekubariki,basi ningependa kusikia kutoka kwako kwa kuniandikia msg au kunipigia kwa namba zangu zilizopo hapo juu. Pia kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,waweza kunipigia sasa.

Na mch. Gasper Madumla.+255 683 877 900) What’s app ni+255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page