SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA BIASHARA YAKO.
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 30, 2017
- 4 min read
Updated: Sep 29, 2022

Kila mfanya biashara hulenga faida maana tunapozungumzia biashara tunazungumzia faida sababu biashara bila faida imekufa kama ilivyo imani bila matendo imekufa. Hakuna awezaye kufanya biashara au kazi yoyote pasipo faida na ndio maana hata Daudi alipoiendea kazi ya kupambana na Goliath,kwanza akataka kujua atapata faida gani? Naye akawauliza wale watu pamoja na mfalme kwamba atapata faida gani ikiwa atamuua huyo Goliath wa Gathi,( 1 Samweli 17:26-27).
Daudi hakuwa mjinga kuuliza hivyo bali alitaka kujua hakika atapata faida gani na huyo ndiye mfano wa mtu mwerevu ambaye kabla ya kuanza kazi fulani hutaka kuona faida yake ikoje. Ingawa Daudi alisikia atakayemuua Goliath wa Gathi atatepewa nini,lakini akauliza tena ili sasa ajilidhishe akiyathibitisha maneno yao. Mtu mwerevu uangalia mara mbili mbili kazi fulani kutaka kujua faida yake kabla ya kuanza.,
Kama ilivyo kwa Daudi alipojua atapata nini ikiwa atamuua huyo Goliath wa Gathi, basi akaanza kazi na hakurudi nyuma maana alikwishajua malipo yake yamekaa mkao gani. Kule kujua atakachopewa kulimtia nguvu kwa kazi nzima. Na ndivyo ilivyo kwa mtu mwerevu katika biashar/kazi akiisha jua namna itakavyomlipa kamwe hataangalia nyuma ni mpaka kieleweke.
Lakini mtu mjinga yeye huanza biashara bila kuangalia faida na hasara. Akiwa katikati ya biashara ndipo anakumbuka kipengele cha faida,matokeo yake biashara inagharimu maana kaanza bila kupiga hesabu stahiki wala hakuwa na uweledi wa biashara hiyo. Wengi leo,wanaanzisha biashara bila kuangalia faida yake,na wanaanzisha kwa sababu wamemuona fulani naye kaanzisha. Wale wote wenye kufanya biashara au kazi pasipo kuwa na uelewa mzuri wa uzalishaji wanaitwa kwa jina la kitaalamu “ wafuata mkumbo”.
Mfuata mkumbo ni yule anayefanya kazi nje ya uweledi wa kazi hiyo,anafanya kwa sababu amemuona fulani naye akifanya. Hata ukimuiza kwa nini unafanya biashara/kazi hii hana majibu!!! Au.sana sana atakuambia“kwa sababu kazi hii ipo damuni..” au atakuambia“ kwa sababu ninaipenda sana kazi hii…”.Ukiona mtu wa namna hii,basi ujue hajui alifanyalo! Maana huwezi kufanya biashara au kazi kwa sababu tu unaipenda! Je kuipenda kwako kunakupa faida gani? Wewe unafikiri kuipenda kazi ndio faida? Sijui wewe mwenye biashara au kazi,unafanya kazi hiyo kwa sababu gani? Au ulifungua biashara hiyo kwa sababu ulimuona fulani? Je upo katika kusudi lako ndani ya hicho ukifanyacho sasa? Mimi sijui kwa upande wako, lakini wewe wajua!
Siku moja nikiwa nimeajiriwa na kampuni moja hapa nchini kwetu Tanzania. Kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi tuliyokuwa nayo siku hizo,hivyo tukawa tukiifukuzia mikopo kweli kweli,maana kila mfanyakazi anatafuta kutoka kimaisha. Yaani tukisikia benki fulani inatoa mikopo kwa wafanyakazi,basi hapo haipiti dakika 10 tumeshafika kwa branch manager na mara moja kuanza “ kumdadavua kuhusu utaratibu wa kupata mikopo ya chapu chapu”. Maana tulikuwa na kiu ya kudaiwa we acha tu!
Sasa benki fulani hivi iliyopo karibu nasi ikajileta yenyewe na kututaka wafanyakazi tukope mikopo kwao. Hapo ndipo niliposikia mwenzetu mmoja akasema“ mwaka huu,tunaenda kuolewa na watu wa benki,tutakoma na hii ndoa….”. Mimi sikumuelewa vizuri kipindi kile, lakini nilikuja taratibu kumuelewa nini alikuwa akimaanisha.
Hatukujua siri ya mafanikio ya kazi zetu. Hivyo, wengine walichukua mkopo na wengine walikataa. Mimi nikawaona hawa waliokataa kukopa ni wajinga fulani hivi,kwa sababu tulikuwa tukiifukuzia mikopo kweli kweli hapo awali,sasa imejileta yenyewe alafu watu wengine wanaikataa,sikuwaelewa hata kidogo!!! Basi,wenye kuchukua wakachukua na wenye kuacha wakaacha.
Sasa,wengine walikopa kwa sababu waliona wenzao wakikopa hawa ndio “wafuata mikumbo” alafu watu wa namna hii wanakuwa wengi kuliko!sijui wewe upo kwenye kundi gani. Wengine walichukua mkopo kwa sababu walikuwa na malengo fulani. Wachache walikataa.
Kundi la wachache lilikuwa mojawapo ya kundi lililo sahihi sana,maana walipopiga hesabu na kuangalia faida na hasara,wakaona hasara badala ya faida hata wakaamua kuacha. Na watu wa namna hii wana uweledi juu mikopo. Wewe Je? Inawezekana kabisa ukawa unamadeni kama nini,umekopa ukihitaji kufanikiwa katika biashara yako,lakini ulifanya nje ya ufahamu sahihi,na sasa umejikuta ukiwa kwenye mateso makali ya kulipa madeni ya watu. Yaani kama alivyojisemea yule mmoja wa wafanyakazi kwamba “ umeolewa na yeye aliyekukopesha..” kiasi kwamba hufurukuti kwake!
Wewe unafikiri mkopo ndio njia pekee ya kufanikiwa kwa biashara yako? Nenda kawaulize waliokopa wakiwa na mtazamo huu,nao watakuambia vile wanavyoumia hata wanatamani wasingelikopa. Siri ya kufanikiwa haipo kwenye mikopo kama wengi wanavyoelekeza mitazamo yao. Kufanikiwa katika biashara yako ni zaidi ya kukopa!
Kumbuka Kwa kila fanikio la kazi au biashara fulani ipo siri ndani yake ya kufanikiwa kwa sababu hakuna biashara iliyofanikiwa ikakosa siri. Zinaitwa “siri” kwa sababu zimejificha,si wengi wenyekuzijua. Kwa sababu hiyo,yeyote anayetaka kufanikiwa kibiashara basi hana budi“ kuzitafuta” . Zipo siri nyingi za kufanikiwa kibiashara,lakini mimi leo ninakufundisha siri tatu za kiroho,nazo ni kama ifuatavyo;
01. Mshirikishe Mungu katika biashara yako.
Hii ndio siri ya kwanza kuliko zote,kumshirikisha Mungu sio kumshirikisha mwanadamu. Unapoanza kuwa na wazo binafsi la biashara fulani,basi hapo usiliuze wazo lako kwa yeyote yule isipokuwa kwanza kwa Mungu Yeye awezaye kulikuza wazo hilo pamoja na biashara yako yote. Kumshirikisha Mungu kuna maana ya kumuhusisha Mungu juu ya biashara yako yote pasipo kuficha.
Unamshirikisha Mungu kwa namna gani?
Kwa kuombea wazo lako la biashara au biashara uliyokuwa nayo. Maombi haya ni mapana,ili uliwasiliana nami kwa namba zilizopo hapo chini nitakuambia ufanye maombi ya namna gani
Kuijenga madhabahu kwenye ofisi ya biashara yako ikiwa kama umekwisha kuwa nayo. ~ kumbuka; madhabahu ni kiunganishi kati yako na Mungu. Hivyo,una hakikisha ibada ikifanyika kwa kila siku uliyojipangia.
N.k
02. Kuwa mtoaji.
Siri hii ni kubwa,ukijijengea mazingira ya kutoa kwa Bwana kutoka katika pesa au mali ya biashara yako,uwe na uhakika utafanikiwa tu. Katika siri hii,ni lazima uiunganishe biashara yako na Mungu kwa matoleo. Sadaka ina nguvu ya kuunganisha. Ndio maana wale wa upande wa pili wameziunganisha biashara zao na miungu kwa njia ya utoaji. Utoaji huu,ni zaidi ya fungu la kumi,bali pia kusapoti kazi ya Mungu kutoka katika biashara yako.
03. Kujua matumizi sahihi ya damu ya Yesu.
Kumbuka kwamba,yeye anayemiliki madhabahu ndiye anayemiliki ardhi. Na kila biashara hutegemea ardhi mahali itakapokuwa. Hivyo ni lazima ujue ni jinsi gani utakavyoweza kuikomboa biashara yako na kuimiliki katika ardhi aliyokupa Bwana. Nimeshuhudia biashara nyingi zikifa si kwa sababu zimekosa mitaji! La,kwa sababu ardhi haikufunguliwa. Mambo ya kiroho yamekwamisha sana biashara za wengi.
Mfano; ardhi inaweza ikabeba laana,na endapo kutakuwa na biashara juu yake,basi usitegemee kuona faida bali hasara hata kama mfanyabiashara atakuwa ni msomi sana,hataweza kuambulia faida. Maeneo yeyote ambapo kuna ardhi iliyolaaniwa hakuna mafanikio ya ustawi wa namna yoyote ile. Sasa,kinachoweza kusafisha eneo hilo ni damu ya Yesu tu. Sijui kama unanielewa vizuri wewe usomaye sasa.
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni +255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários