top of page

SIKUKUU TATU MUHIMU ZA WAYAHUDI.

Na Mch Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi sana…

Wayahudi wana kalenda kuu mbili;

  1. Kalenda ya dini

  2. Kalenda ya serikali.

Kwa mujibu wa kalenda ya dini,wayahudi wameamriwa waafhimishe sikukuu kubwa tatu kwa mwaka,ingawa zipo sikukuu nyingine za kidini zilizoamriwa. Sikukuu hizi tatu wakati mwingine zinaitwa “ sikukuu za BWANA ” leo hii duniani pote tunaadhimisha moja kati ya sikukuu zao kwa sababu nasi sikukuu hiyo inatuhusu kwa maana tumekwisha nunuliwa kwa damu ya thamani ya mwana-kondoo,sikukuu hiyo ni “ pasaka“. Lengo mama la ujumbe huu ni kukufahamisha sikukuu tatu muhimu kwa Wayahudi,zilizoanzia kwenye agano la kale lakini zikiendelea pia kwenye agano jipya na moja wapo na wewe inakuhusu sana.

“ Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu. Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu [ Pasaka]; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu; tena, sikukuu ya mavuno [ Pentekoste ], hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya [ Vibanda ] , mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani.17 Mara tatu katika mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU.” Kutoka 23:14-17

Kwa mujibu wa Neno hilo tunaziona sikukuu zote tatu zikitajwa. Lakini ebu angalia kwa makini mstari wa kumi na saba na utagundua kwamba Wayahudi walitakiwa wakusanyike pamoja kwa ajili ya sikukuu hizo. Na hilo ndilo lipo mpaka sasa,Wayahudi wanaheshimu sana sikukuu zilizoamriwa na Bwana,ndio maana kipindi cha sikukuu zao kinawalazimu kusafiri na kurudi makwao kwa ajili tu ya sikukuu. Unaweza ukaliona hili unapowaangalia Wayahudi waliotawanyika leo hii,kipindi cha sikukuu zao wengi inawarazimu kurejea makwao.  Kwa mujibu wa Neno,sikukuu hizo ni;

  1. Pasaka.

  2. Pentekoste

  3. Sikukuu ya vibanda.

Katika sikukuu ya Pasaka na sikukuu ya vibanda zinafutiwa na sikukuu ndogo kila moja isipokuwa sikukuu ya Pentekoste haina sikukuu ndogo. Kivipi?

01. Pasaka.( mwezi wa Abibu kwa kalenda ya leo ni March-Aprili)

Neno “Pasaka” kwa Kiyahudi ni “ Pehsakh” au “ passover”  lenye maana ya “ukombozi uliofanyika kwa njia ya damu ya mwana-kondoo iliyopakwa kwenye miimo ya milango ya nyumba za wa-Israeli,Bwana akapita juu asiwadhuru kwa pigo lolote, (passing over)“(Kutoka 12:13). Ilikuwa ni ukombozi kwa Waisraeli kutolewa utumwani Misri,Bwana akasema siku hii itakuwa ukumbusho kwenu,“nanyi mtaifanya iwe sikukuu” katika vizazi vyenu vyote kwa amri ya milele- Kutoka 12:14. Sikukuu hii inafuatiwa na sikukuu ya “mikate isiyotiwa chachu na malimbuko ya kwanza” sikukuu hizi mbili zinazofuatiwa huitwa ni sikukuu ndogo ambazo zinakuwa zikienda au kufuatiwa na sikukuu ya Pasaka. Umuhimu wa sikukuu hii ni kukumbuka jinsi ambavyo Waisraeli walivyokombolewa kutoka katika utumwa huko Misri -Kutoka 12:14

02.Pentekoste ( Mwezi Sivan,sawa na June)

Neno hili“Pentekoste” ilikuja siku hamsini baada ya Pasaka,na hii ndio sikukuu ya kipekee kati ya zile mbili ambapo sikukuu hii haina muambatano wa sikukuu ndogo nyingine (Kama ilivyo kwa Pasaka na sikukuu ya vibanda). Umuhimu mkubwa wa sikukuu hii ni kuwakumbusha Wayahudi kuhusu Mungu aliposhuka na utisho wake kwenye mlima Sinai kipindi Musa anapewa sheria,hasa kwenye Kutoka 19:15-16.Katika agano la kale sikukuu hii ilijulikana kwa majina kama;

  1. Sikukuu ya majuma ( Kumbukumbu 16:9-10)

  2. Sikukuu ya mavuno ( Kutoka 23:16)

  3. Sikukuu ya malimbuko ( Hesabu 28:16)

03. Sikukuu ya vibanda ( Mwezi Ethanimu,sawa na mwezi Septemba-Octoba)

Ikumbukwe kwamba Waisraeli walipotoka utumwani Misri walitembea sana jangwani kwa muda mrefu. Bwana “aliwatweza“akitaka waanze kunyenyekea;na wengi walikufa wakiwa jangwani kwa sababu ya manunguniko yao,Bwana aliwaangamiza. Wakiwa jangwani wakapiga mahema ( vibanda). Bwana akawataka wakumbuke miaka waliotumia kukaa jangwani kwenye vibanda. ( Walawi 23:23-25). Umuhimu mkubwa wa sikukuu hii ni kuwakumbusha Wayahudi miaka walioishi huko jangwani. Sikukuu hii inafuatana na sikukuu ya “Baragumu na siku ya upatanisho“

Sasa angalia hapa;

Katika agano jipya,Bwana Yesu yeye mwenyewe ndio pasaka wetu ( 1 Wakorintho 5:7),hii ikiwa na maana zaidi ya agano la kale kwa sababu Yesu ndiye mwana-kondoo aliyechinjwa kwa ajili yako na kwa ajili yangu. Yeye Yesu alikula pasaka siku moja kabla ya Pasaka ya kiyahudi yaani alikula Pasaka na wanafunzi wake Alhamisi ( Luka 22:7-23),kisha siku inayofuata siku ya Pasaka,Yeye Yesu akasurubiwa damu ikiatoka maana ni mwana-kondoo aichukuaye dhambi za ulimwengu.

 Kisha siku ya“ sikukuu ya malimbuko “,yaani siku ya tatu akafufuka katika wafu kama maandiko yasemavyo. Na siku hamsini baadaye kwenye “Pentekoste” Yeye Yesu akamwaga Roho yake kwa wanafunzi wake 120 waliokuwa hekaluni. Vivyo hivyo,sikukuu ya vibanda itatimizwa kwenye nyakati za kanisa,hii ikiwa na maana kwamba sasa kanisa lipo kwenye mkusanyiko ambako Yeye Yesu atalinyakua kanisa lake. 

Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,basi nifahamishe tupate kumtukuza Mungu pamoja. Lakini inawezekana labda unahitaji MAOMBI kwa maana nawe unapitia changamoto hii,Basi kwa yote nipigie sasa kwa + 255 683 877 900

What’s app namba ni +255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page