SIFA NA KUABUDU ~ 02
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 10, 2019
- 3 min read
Updated: Sep 2, 2022

Kwa ufupi,
Kuna tofauti fulani kati ya maneno haya “sifa” na “kuabudu” ingawa kwenye makanisa yetu mara nyingi tunayatumia pamoja tu,kwa maana kwanza hatujui vizuri maana kamili ya sifa na kuabudu. Wengi tunadhani maneno hayo yanazungumzia“ nyimbo” Kitu ambacho ni sawa kwa sehemu fulani lakini kuna mengi zaidi ya hivyo. Na kwa sababu tuna mtazamo huo,basi tunajikuta tukitofautisha maneno hayo mawili pale tunapoona nyimbo za haraka haraka (kwa midundo yake )za kiroho tunaziita hizo ni nyimbo za sifa.
Na zile zinazoimbwa kwa utaratibu tunaziita ni za kuabudu. Mtazamo huu una ulakini fulani kwa maana huwezi hasa kutofautisha nyimbo za sifa na kuabudu kwa kuangalia kigezo cha mapigo ya beat/mdundo/ngoma! Lakini ndivyo wengi tunavyozania hivyo,hata mimi ndivyo nilivyokuwa nikijua. Kwa mtazamo huu kuna kitu kitakuwa kinakosekana. Lakini biblia inaeleza nini kwa habari ya “sifa na kuabudu”?
Sifa
Neno “sifa” ni “praise” lenye maana ya kusifu ukuu wa Mungu,( katika kazi yake,matendo yake,uweza wake,n.k). Bwana ameumba viumbe ili vimsifu,hata sisi wanadamu tumeumbwa ili tumsifu yeye peke yake na ndio maana Zab.150:6 inasema “Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya” hii ina maana viumbe vyote vyenye uhai havina budi kumsifu Bwana. Ukiuchunguza kwa umakini mstari huo,utagundua suala la sifa si la waimbaji peke yao,bali kila mtu na kila kiumbe. Lakini si hivyo tu,
Bwana ameamuru Yeye asifiwe na vitu/viumbe vyote alivyoviumba. Kumbuka jambo la msingi ;“Sifa inaeleza namna Mungu alivyo” – Zab. 86:12-13,8,10. Eneo hili la “sifa ” ni eneo muhimu kiasi kwamba Yeye Mungu mwenyewe ameamua kuketi hapo. Na ndio maana ikiwa kama kutakuwa na sifa njema itokayo ndani ya moyo wako,unajikuta ukifunikwa na uwepo wa Bwana ambao kwa kweli hukuuomba uje,lakini kitendo cha kumsifu Yeye tu ni ibada tosha ya kumwalika awe pamoja nawe.
Kuabudu
Kuabudu ni kueleza habari ya “tegemeo” lako kwa Bwana Mungu. (Ni kitendo cha kushuka na kutoa heshima kwa lengo la kutegemea) Mwenye kuabudu husema “hana Mungu mwingine anayemtegemea” kwa hiyo,kitendo cha kuhamisha nafasi ya kujitegemea binafsi,au kumtegemea mtu/watu na kupeleka kwake Mungu ni kitendo cha “kuabudu“. Ukisikia msamiati huu “ usiabudu sanamu” maana yake usiweke tegemeo lako kwa sanamu. Unakumbuka habari ya Yesu alipokuwa amepandishwa na Roho nyikani,ili ajaribiwe. Ibilisi kwa hila,alimwambia ;
“…haya yote nitakupa,ukianguka kunisujudia” Mathayo 4:9. Ibilisi alimtaka Yesu amwamini yeye,amtegemee yeye,ili kusudi ibilisi amrithishe mali za dunia. Kitu ambacho laiti ibilisi angelijua Yeye aliyekuwa akimjaribu ni mtu ambaye ndiye hasa mmiliki wa vitu vyote,kwa maana vyote viliumbwa kwa ajili yake na kwa njia yake ( Wakolosai 1:16). Lakini Yesu alitambua ni nani hasa wa kumtegemea,akamwambia “…Bwana Mungu ndiye wa kuabudiwe yeye peke yake”
Mathayo 4:10.Kumbuka; Bwana tangu mwanzo ameweka taratibu za kuabudiwa na Kitabu cha Walawi kinaeleza taratibu za kuabudu kama kivuli cha ibada hali ya kuabudu katika agano jipya.
Kwa hiyo ukichungulia vyema katika maneno haya “sifa“na“kuabudu” utagundua tofauti fulani ipo. Sifa na kuabudu ni ibada yenye nguvu sana machoni pa Mungu. Kwa maana ibada yoyote iliyokosa sifa na kuabudu hakika si ibada ya kweli, kwa maana kama hakuna kumsifu na kumwabudu Mungu, basi wanamwabudu nani? Je ni ibada hiyo?
La hasha,si ibada mbele za Mungu!!! Hivyo,kusifu na kuabudu ni zaidi ya nyimbo tunazoziimba,ingawa nyimbo zote za sifa na kuabudu ni sehemu tu. Kwa kuwa Mungu ni Mungu tu,hata usipomsifu au kumwabudu,hakubadilishi nafasi yake ya kuwa Mungu!!!
Wimbo wa sifa na kuabudu unapaswa uweje?
Leo “tunakizungumkuti“/ michanganyo kweli kweli juu ya nyimbo za sifa na kuabudu. Kila kukicha nyimbo zinaandikwa na kurekodiwa kisha“ kubatizwa” kwa majina kwa majina ya nyimbo za sifa na kuabudu. Lakini ukweli ni kwamba kama utachukua muda kusikiliza itagundua nyimbo nyingi si za sifa wala kuabudu,basi tu ilimladi mambo yaende!!! Hujawahi kuona nyimbo za sifa, lakini kwa kweli hazimsifii Mungu, isipokuwa ndani ya nyimbo zinamtaja Yesu, au Mungu kisha mwimbaji akizungumzia shida zake au kesi zake huku midundo/beats kuchanganywa kwa haraka haraka na watu wakifurahia sana wengine hata husema ;
“dah! Huyu mwimbaji kweli anaimba! Anasifu kweli kweli ” lakini ukimwuuliza huyo shabiki ni sifa gani ya Mungu inayozungumziwa humo,yeye atakwambia “sijui kwa kweli “. Kha! Sasa mbona unashangilia hivyo? Lakini hata ukifanikiwa kumwuuliza mwimbaji juu ya kile akiimbacho,utagundua na yeye mwenyewe hajui kabisa! Lakini anaimba kwa sababu watu wanapenda anavyoimba!!! Uwiii….
Ni jambo la kushangaza sana…
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI,piga sasa kwa namba hizi + 255 683 877 900
Whatsapp namba +255 746 446 446
Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments