ROHO YA HEKIMA NA MAFUNUO – 03
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 14, 2020
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
“ Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;” Waefeso 1:17. Nalikuwa najiuliza kwa nini hata Paulo afanye maombi ya namna hii katika kanisa la Efeso,wakati nautafakari mstari huu,nimeona kitu fulani hivi. Ukweli ni kwamba Paulo alipoliangalia kanisa na kuona kwamba “bado kanisa halimjui Mungu” ndipo akatamani kanisa livikwe roho ya hekima na ufunuo. Ni kweli kabisa,bado hatujamjua Mungu ipasavyo,bado tuna hali ya kupapasa – papasa katika kumjua Mungu na ndio maana kuna mambo hatuyasikii wala kuyaona kiroho,tena ndio maana tunatumika kwenye viwango vya chini,Sasa kuna umuhimu wa kutaka sana kumjua Mungu.
Lakini kwa nini roho ya hekima na ufunuo ?
“roho ya hekima ” kwa ajili ya kupata maarifa yatakayokusaidia kutenda sawa sawa na ufunuo utakaopata
“roho ya ufunuo” umjue Mungu pale anapojifunua kwako.
Kujua wito wako
Kupata kuona kama aonavyo Mungu
Ili kuliishi Neno
Kusudi kubwa la Bwana anapokuita katika ngazi ya kwanza ya kuokoka,ni moja tu,nalo ni “kumjua Yeye kikamilifu ” ili uweze kumpenda na kisha umtumikie ndani ya mapenzi yake. Kumbuka ; kutumika ni zao la kumpenda Mungu,. Roho ya hekima na ya ufunuo,inakuleta katika kumjua Mungu kwa undani.
Mungu anajifunua / anajidhihilisha namna gani?
Kwa kuwa Mungu hujifunua hata sasa kwa njia nyingi na tofauti tofauti,kiasi kwamba njia zake hazichunguziki. Katika njia hizo,unahitaji kuwa na roho ya hekima na ufunuo ili kusudi umtambue kwamba ni Yeye Mungu wala si shetani. Mungu aweza kujifunua katika ndoto,maono,katika Neno,katika uumbaji wake,katika udhaifu/magonjwa/dhiki,n.k. Pasipo roho ya ufunuo,huwezi kumtambua Mungu. Kumbe kumjua Mungu hakutokani na jitihada binafsi za Mungu ingawa jitihada binafsi ni muhimu,bali kunatokana na “uwezo wa kiroho ” wa hekima na ufunuo. Kanisa linahitaji kitu kimoja tu,nacho ni “kumjua Mungu sana ” ili kuimarisha ushirika wenye nguvu kwa maana hapo ndipo penye amani na mema -Ayubu 22:21
Kuyafanya mapenzi ya Mungu kunahitaji sana roho ya hekima na ufunuo.
Mtu mwenye kutembea kwenye mapenzi ya Mungu ni yule mwenye roho ya hekima na ufunuo. Nje ya hapo mtu kamwe hawezi kutembea kwenye mapenzi ya Mungu. Kwa sababu kusikia na kuona kiroho kunaleta kumjua Mungu na kuyafanya mapenzi yake. Ukimtazama Kristo,utagundua kwamba Hazina ya hekima na ufunuo ilikuwa ndani yake,na ndio maana alitembea na Mungu ipasavyo. Kiwango chako cha kumjua Mungu kipo chini,na namna ya kuwa chini ndio namna ile ile ya kushindwa kuyafanya mapenzi ya Mungu.
Kuna mambo lazima yageuzwe,ili upewe uwezo wa hekima na ufunuo.
Ukihitaji kuona mafanikio ya kiroho hasa kupewa hekima na ufunuo,kuna mambo lazima uyaache,au uachishwe ndipo hekima na ufunuo uje ( Kwa maana haiwezekani kupewa roho ya hekima na ufunuo huku ukiwa umeshikilia mambo yako binafsi,lazima ukubali kuyapoteza kwa ajili ya kumpata Kristo ). Paulo alikuwa ni mtu aliyepewa Hekima ya ajabu na mafunuo lakini ukimfuatilizia maisha yake,utagundua kwamba kuna mengi ya kwake aliyapoteza kwa ajili ya Kristo- Wafilipi 3:8. Biblia inasema tena“ Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.
9 Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. ” Matendo 9:8-9. Huyu Sauli ndiye aliyekuwa mtume Paulo,alivyokuwa Sauli kama tusomavyo hapo,alikuwa ni mtu mwenye mambo yake binafsi,ingawa aliliudhi kanisa lakini alikuwa mshika dini ya kiyahudi ( Hii kuonesha kwamba “mshika dini”anaweza kuwa ni machukizo kwa Mungu,ikiwa hajapokea neema ya wokovu).
Bwana alimpomwita Paulo alihakikisha anamtoa kwenye matakwa yake,ili Bwana Mungu ayaweke matakwa/mapenzi yake.Kumbuka moja ya jambo muhimu sana katika roho ya hekima na ufunuo,Bwana akampofusha macho yake,akawa haoni siku tatu. Bwana akawa anashughulika na macho ya rohoni / roho ya ufunuo,kumwambia sasa hutaona vile uonavyo,wala hutasikia vile usikiavyo. Lakini ni lazima yale yote ya kwake binafsi yatakayomtenga na Bwana katika wito,yanaondolewa kwanza. Unafikiri kwa nini Bwana alimfanya Paulo asione kimwili kabisa katika siku tatu,tena bila kula? Roho ya hekima na ufunuo huitaji sana kuondolewa yote yanayohusu mapenzi ya mwili….
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Na kwa huduma ya MAOMBI ushauri na msaada zaidi,piga sasa +255 683 877 900
What’s app namba +255 746 446 446
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments