top of page

ROHO YA HEKIMA NA MAFUNUO – 01

Updated: Aug 30, 2022


Siku moja kwenye kanisa fulani la kiroho,aliingia mtu mmoja akiwa na vifaa vya kiganga kwenye kijimfuko kidogo alichokificha ndani ya bukta kisha akavalia na suruali na koti kubwa. Kwa mwonekano wa nje huwezi kumtambua kabisa kwa maana alionekana kama washirika wengine,lakini ukweli ni kwamba kuna vitu vya giza alikuwa amevibeba. Yule jamaa akatafuta siti akakaa tuliii,ibada ikiwa inaendelea kama kawaida. Na kilipofika kipindi cha kuita watu waokoke waje mbele,yule jamaa alinyanyuka na kwenda mbele (Bila shaka nguvu za Mungu zilimnyanyua kutoka kwenye siti yake hata akajikuta yupo mbele ya madhabahu ya Bwana)

akiwa hapo mbele ya madhabahu pamoja na madawa yake ya kishirikina,kichawi. Basi mchungaji akamwongoza sala ya toba na kumwombea kisha wenyeji wakaenda kumpokea kwa kumbatia na shangwe nyingi huku akiwa na vifaa vyake vya uganga. Mpaka shughuli zote za ibada zinaisha,hakuna hata mmoja kwenye kanisa zima aliyefanikiwa kuona uchawi aliokuwa ameubeba. Akawa nao mwanzo wa ibada hadi mwisho wa ibada.


Na mwishoe yule jamaa ikabidi amtafute mchungaji mmoja hivi na kumwambia nimekuja na uchawi sasa naomba uniombee nami siyataki mavitu haya yamekuwa yakinitesa kwa muda mrefu. Haspo ndipo mchungaji pamoja na mchungaji mwingine wakamfanyia huduma kisha wakachoma moto hayo mavitu aliyokuwa ameyabeba.


Sasa angalia hapo,hivi kama huyo mtu angeliamua kumdhuru mtu ndani ya kanisa asingeliweza? Kanisa halioni!!! roho ya mafunuo haikuwepo kabisa? Ama ni nini basi,mtu kuja na uchawi kuanzia mwanzo wa ibada hadi mwisho bila kujulikana,imekuwa hatuoni kiasi hicho? Je ni unajifunza nini kwa mfano huo?


Hivi,tunawezaje kumtumikia Bwana pasipo kuona kiroho? Lakini hata hivyo jifunze tu hapo kwamba,kumbe katika ibada tunazozifanya kuna wengine si watu wazuri na wanaingiaga kwenye ibada,kwa nje waweza kuonekana ni wema na wazuri kwa mavazi yao na namna walivyojiweka lakini kumbe ni watu wabaya kupindukia!!! Sasa utawatambuaje watu wabaya namna hiyo,wale ambao ni mawakala wa shetani?


Roho ya hekima na mafunuo”ni karama za Roho mtakatifu ndani ya kanisa ili kazi yake itendeke ipasavyo. Katika zile karama 9 (1 Wakorintho 12:8-10) za Roho mtakatifu,karama moja wapo ni karama ya Neno la hekima. Lakini pia roho ya mafunuo ni kipawa /Uwezo wa Roho mtakatifu yeye awezaye kuchunguza siri za mioyo.


Hivyo roho ya hekima na mafunuo  ni msingi wa kanisa la Bwana na ni msingi wa mtu mmoja mmoja anayeifanya kazi ya Bwana ama yule tu aliyeokoka,kwa sababu watu hukimbilia kanisani ama kwa waliookoka kutafuta msaada wa kiroho,sasa kama hakuna roho ya hekima na mafunuo basi ni dhahili watu watakosa msaada huo wanaoutafuta.

  1.  Roho ya hekima na mafunuo ni nini hasa?

Hekima hutembea na mafunuo,roho ya hekima ni uwezo wa kiroho wa kupambanua mema na mabaya (1 Wafalme 3:9). Pia roho ya mafunuo ni uwezo wa kusikia na kuona kiroho. Haya mawili “hekima na mafunuo” ni kitendea kazi kikubwa kwa mtu wa Mungu. Yesu Kristo alikuwa ni tajiri wa hekima na mafunuo,ndio maana kazi yake ilifanikiwa kiasi kikubwa sana kwa muda mfupi. Ebu angalia mfano huu,ambao ndani yake tunaona roho ya hekima na mafunuo;


“ Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli.


Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia,Nionyesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa. ” Luka 20:20-26           

                                

Ukisoma vizuri kisa/mfano huo kuna mambo utayagundua,na utaona namna roho ya hekima na mafunuo ilivyofanya kazi. Kwa upande wa hekima biblia inatuambia,Yesu alijua kuwajibu kwa usahihi wake ingawa alikuwa akiwajua ni watu wa namna gani. Majibu ya Yesu yaliwafunga vinywa vyao kwa maana yalijaa hekima ya ajabu.


Kwa habari ya mafunuo,Yesu alikuwa amewajua tangu walipopanga watu hovyo wamwendee na kujifanya ni watu wa haki,tangu wanapanga mipango hiyo yeye alikuwepo hapo hapo kiroho akiona kila kitu,na tazama mstari wa 23,Biblia inasema “ alitambua hila yao”. Hekima na ufunuo ulifanya kazi pamoja hata wakashindwa kumkamata….

ITAENDELEA…


Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.


Na kwa huduma ya MAOMBI ushauri na msaada zaidi,piga sasa +255 683 877 900


What’s app namba +255 746 446 446


Na Mch.G.Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page