NGUVU YA HAZINA ILIYOSITIRIKA.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 28, 2019
- 4 min read
Updated: Sep 29, 2022

Kwa ufupi… ( Ukihitaji kujifunza zaidi somo hili,fanya mawasiliano hapo chini,22 Dec. @ Beroya)
( Kumbuka; Somo hili ni mbegu,kwa maana limebeba mafunuo makubwa ya kumtoa mtu mahali fulani alipo kama ataelewa vyema,pia ni mbegu kwa wachungaji watakaoweza kujifunza kisha kulifundisha kanisa, lakini ni mbegu kwako unayesoma sasa,ili utambue hazina iliyositirika.)
Tunapozungumzia kuhusu “ hazina iliyositirika ” tuna maana ya kito cha thamani kilichofichwa kwa sababu ya uthamani wake,na kito hicho kina nguvu ya kubadilisha historia nzima ya maisha ya mtu. Kawaida,hazina ina tabia ya “kufichwa“,upatikanaji wake ni mgumu,tazama “ dhahabu,almasi ama shaba” mfano wa vito vya thamani kubwa ulimwenguni,ambavyo vimesitirika chini,ardhi imeficha hazina hizo.
Na mtu awaye yote mwenye kutamani kuipata hazina iliyositirika mfano wa dhahabu,mtu huyo atalazimika kulipa gharama kubwa ya pesa,muda pamoja na nguvu ya kuitafuta. Kazi hiyo,inaweza ikamghalimu kupoteza kazi nyingine ili afanye kazi moja tu kwa muda mrefu. Lakini habari njema ni kwamba akifanikiwa kuipata,basi maisha yake hubadilika kwa ujumla kwa maana ameipata hazina adhimu. Katika utafiti nilioufanya,nimegundua kwamba kila mtu hutamani kupata “hazina” lakini watu wengi hawapo tayari kulipa gharama!!! Sijui
kwako,lakini ukumbuke ya kwamba kila kitu kizuri,kina gharama kubwa!
Biblia inatupa mfano ulio wazi juu ya thamani ya hazina iliyositirika shambani. “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.” Mathayo 13:44. Yesu anaeleza mambo makubwa mawili katika mfano huu.
A) Ufunuo kwa habari ya ufalme wa mbinguni
Kwanza ni habari ya ufalme wa mbinguni ambao thamani yake ni kubwa kupita dhahabu au almasi,au madini yoyote,na huo ndio ufunuo mama wa Mathayo 13:44 .Anaeleza kwamba, ufalme wa mbinguni unapogundulika upo mahali fulani,basi yeye agunduaye analazimika kuuza vitu vyote alivyonavyo ili aupate ufalme huo.
Ufalme wa mbinguni unapofananishwa na hazina,ina maana si wengi wauonao bali wachache. Hivyo,pale ambapo kunafanyika mapenzi ya Mungu ( labda kanisani mahali ambapo kweli inahubiriwa) mtu agunduapo hapo,na kuona thamani yake, atakuwa radhi kukubali kupoteza alivyonavyo ili apatikane hapo kwenye mapenzi ya Mungu. Ndio maana Paulo anasema kwenye Wafilipi 3:8 kwamba vitu vyote vilivyokuwa vya thamani kwake aliviona havina thamani na kukubali kupata hasara kwa vitu hivyo ili ampate Kristo. “ Kristo” ni hazina kubwa yenye nguvu kuliko dhahabu au almasi!
B) Kwa habari ya hazina iliyositirika shambani ( Mathayo 13:44)
Biblia inasema hazina iliyositirika ndani ya shamba iliyofananishwa na ufalme wa mbinguni.Yule mwenye shamba alikuwa na hazina ndani ya shamba lake,lakini hata hivyo hakuiona hazina hiyo,mtu mwingine tena mpita njia tu,aliiona. Na alipoiona,alienda akaificha zaidi hapo hapo shambani. Sasa,angalia; kilichomfanya huyu mjanja aliyeiona hazina ndani ya shamba la mtu mwingine ni nini? Na kwa nini aliificha zaidi? Bila shaka kuna kitu cha ziada alichonacho huyu aliyeiona,bila shaka alikuwa mchunguzi na mtu mwenye
kutafakari,kwa maana si rahisi kabisa kuigundua hazina iliyositirika kwenye shamba la mtu mwingine. Lakini hata hivyo waweza kuiona,lakini ukashindwa kuitambua! Huyu ndugu mjanja“ aliipekecha” kisha akagundua ni hazina ya thamani. Kwa ujanja wake aliificha tena,chini zaidi,ili mwenye shamba asije akaiona. Na hapo ndipo wazo la kuuza alivyonavyo lilipokuja,maana alijua akiuza alivyonavyo atalinunua tu shamba la mtu mmoja hivi asiyeona nini alichonacho! Hii inatufundisha kwamba kuna watu wamebeba hazina, lakini hawajatambua hata sasa. Lakini kuna “ mjanja fulani” yeye aweza kuona ni nini wewe umebeba!
Wakati natafakari kuhusu hazina iliyositirika na mfano huo,nikagundua kila mmoja ana hazina ndani yake,lakini wengi hatuoni wala kutambua. Wengi hatuoni kabisa! Kama yule bwana shamba asiyegundua shamba lake limebeba nini? Hata wewe una hazina za ndani,lakini hujui tu,kwa hiyo unaishi bora liende huku kuna hazina kubwa! Na ndio maana unaweza ukamwona mtu akiishi kwenye maisha ambayo si yake,maisha ya viwango vya chini huku akiwa amebeba hazina kubwa inayoweza kumtoa,hii yote ni kwa sababu hajatambua amebeba nini!!!
Sikia,
Mungu alimuuliza Musa swali moja wakati Mungu anamtuma Musa amwendee Farao kwa ajili ya kuwakomboa Waisraeli,Mungu alimuuliza Musa, “ una nini mkononi mwako? “ Musa akajibu vyema kabisa kwamba ana fimbo. Lakini sasa tazama, vile Musa alivyokuwa akiitazama fimbo aliyokuwa nayo ni tofauti kabisa na vile Mungu alivyoitazama. Musa aliitazama fimbo kama si kitu cha maana,lakini Mungu aliona miujiza kwenye fimbo,aliziona ishara nyingi zinazoweza kufanywa kwa fimbo tu! Hivyo fimbo ya Musa ilikuwa ni hazina iliyositirika kwenye upeo wa macho yake…
Mara nyingi umekuwa ukitizama tofauti kabisa na atazamavyo Mungu. Kile ulichonacho unakiona si kitu,lakini Mungu hutumia hicho hicho kukifanya kuwa ni kitu kwako. Iwapo kama una kitu ambacho unakiona si kitu,kama vile Musa anavyoitazama fimbo yake,basi ujue hiyo ni hazina ambayo imesitirika ndani yako. Kumbuka kila mtu ana kitu! Nacho ni hazina yenye nguvu,ndio maana Mungu alipomtokea Musa,alijua kwamba Musa ana kitu,hata akamwuuliza “una nini?” Ni vigumu kuulizwa una nini hali huna kitu!
Hivyo,hazina iliyositirika inaweza ikawa;
Karama/huduma iliyositirika – Matendo 13:2 ( ufafanuzi wa kina,tuwasiliane)
Kipawa/ujuzi uliositirika – Mwanzo 36:1( Ufafanuzi wa kina tuwasiliane)
Biashara / kazi iliyositirika – 2 Wafalme 4:1-7 ( Ufafanuzi,tuwasiliane)
Hivyo,utagundua hakuna mtu hata mmoja asiye na hazina. Lakini changamoto kubwa hazina zimefichwa! Je wawezaje kujua umebeba hazina gani? Je inawezekanaje ukawa na hazina lakini hujui kama unayo lakini mwingine akajua? Je nini changamoto ya hazina? Na maswali mengi ambayo unaweza ukajiuliza. Nami sina uwezo wa kuyajibu yote hapa,lakini changamoto ya hazina ndani yako zinaweza zikawa;
01. Kukosa ufunuo na maarifa.
Wengi hawajitambui kama yule bwana shamba. Ufunuo ni kitu cha muhimu sana,pamoja na maarifa. Ebu cheki,pale Samweli alipokuwa mdogo na mafunuo hayakuwepo halisi kwake,Bwana akiwa anataka kuzungumza naye,kumwonesha mambo mengi,lakini yeye hajui wala hana ufunuo wowote. Ilimsumbua kwa muda mrefu,na Bwana alikaza kumsemesha.
Sasa ni rahisi kwa Samweli kuwa na hazina za utumishi lakini zimesitirika kwa sababu ufunuo wa Roho haupo. Lakini si hivyo tu,maarifa ni moja kitu muhimu sana. Sasa wengi tunakwamisha na changamoto hii ya kwanza,tupo mbali na ufunuo na papo hapo tumeyakataa maarifa ama hatuna maarifa kabisa! Hiyo pekee inaficha hazina zako ulizonazo.!!! n.k(Ni vyema ukajua kwamba una kitu ndani yako,lakini ni kwa namna gani unaweza ukakijua vyema! Hata ukakitumia )
Kwa maelezo zaidi ya ujumbe huu,tafadhali usisite kuwasiliana nami moja kwa moja kwa + 255 683 877 900
What’sapp namba +255 746 446 446
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
コメント