KUFURIKISHWA NA ROHO
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 22, 2020
- 2 min read
Updated: Aug 30, 2022

Kwa ufupi,
Maji yaendayo kasi yana nguvu mno kiasi cha kusomba somba yale yatakayokuwa juu ya maji. Mto kama mto wa Yordani ambao hufurika kwenye kingo zake wakati wa mavuno kwenye kipindi cha kina Yoshua (Yoshua 3:15),maji yake yalikuwa hayavukiki kirahisi kwa maana maji yana nguvu mno. Mtu yeyote akiwa kwenye maji yenye nguvu basi ni dhahili,maji hayo yatamfurikisha yaani yatampeleka kule asikokutaka,tena kule asipofikiria kwenda,maji yatampeleka.
Kinachofanya mtu huyo kupelekeshwa ni “nguvu kubwa” iliyopo kwenye maji hayo.Hivyo,mtu kwenye maji mengi yaendayo kasi,hana maamuzi yake binasfi,isipokuwa maamuzi ni juu ya hayo maji (Wale wanaotokea kanda ya ziwa watakuwa wanaelewa maji yana nguvu gani).
Roho mtakatifu amajifunua kwa majina mengi kwenye biblia,moja ya jina linalotumika kumwelezea ni “maji” (Yoh.4:13-14,7:37-39). Roho mtakatifu ana nguvu ya kufurikisha zaidi ya nguvu ya maji ya kawaida. Mtu akiwa ndani yake kwenye kiwango cha kujazwa,ni sawa na mtu aliye ndani ya mto wa maji mengi,ambaye ndani ya maji hayo yeye hupelekwa asipopataka yeye,
kwa maana maji yenye nguvu yaweza kumpeleka kushoto ama kulia,ama kumpeleka chini na kuyaona mambo ya ndani ya maji,ama akampeleka juu zaidi.Roho mtakatifu naye hufurikisha vivyo hivyo,humfanya mtu yule aliyejazwa,kupelekwa kinyume na matakwa/mapenzi yake kibinadamu,na kuoneshwa mambo asiyoyajua,mambo yaliyojificha mno.
Mwenye kujua kufurikishwa na maji yenye nguvu ni yule tu aliyezama/aliye tayari majini,naye ndiye anayeweza akaelewa haswa nini maana ya nguvu ya maji. Ajaposema kwa watu wengine,wanaweza wasimwelewe au akashindwa kuelezea uhalisia wa kufurikishwa,lakini yeye akawa anajua vyema.
Ndio maana Paulo alipokuwa akijua siri za ufalme wa Mungu,na kuonja kipawa cha mbinguni,aliwaandikia Wakorintho kitu cha ajabu sana,akawaambia “ Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” 1 Wakorintho 2:14
Yaani anajaribu kuwaambia kwamba,mtu wa rohoni ndiye mwenye kuyatambua ya rohoni,bali yule wa tabia ya asili hawezi kuyajua hayo,hii ni sawa na kusema,
mtu asiyefurikishwa/kupelekeshwa na Roho wa Mungu kamwe hawezi kuelewa utamu wa Roho,isipokuwa yule tu analiyezama ndani ya Roho,ndiye mwenye kujua hasa mambo haya( Waswahili husema“ukitaka ujue utamu wa ngoma,uingie uwanjani ucheze). Roho wa Bwana akichukua nafasi ndani yako,kamwe huwezi kuwa wa kawaida tena , kamwe huwezi kuyafuata mapenzi yako binafsi,(tena akili zako hazitakuwa na matunda kabisa),
isipokuwa wewe utakuwa ni mtu wa kuongozwa na Roho katika yote uyafanyayo.
Yeye ni kama maji ya mto yenye nguvu,yenye kuondoa takataka,yenye kubeba uchafu na kusukumia mbali,yeye ni kama maji yenye kukuchukua kutoka point moja hadi point nyingine kama yatakavyo maji hayo. Hakika kuna raha isiyoweza kusimulika ndani ya Roho Mtakatifu.Kumbuka;ikiwa kama unahitaji kufurikishwa na maji sharti ukubali kuingia majini,kwa maana huwezi ukafurikishwa na maji hali umekaa nchi kavu.
Kuingia majini ni sawa na “ kuokoka” kisha kutamani kujazwa na Roho mtakatifu ( Labda kupitia kwenye ibada maalumu za ujazo wa Roho mtakatifu,kwa kulisoma na kutafakari Neno,kwa kuwekewa mikono na mtu anayefurikishwa n.k).
Lakini lazima umtamani Roho mtakatifu kwenye kiwango cha kufurikishwa,naye ni mwaminifu kukufurikisha.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe.
Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
What’s app + 255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários