NGUVU YA HEKIMA.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 22, 2022
- 2 min read
Updated: Aug 26, 2022

“ Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga.
Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini.
Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi.” Mhubiri 9:14-16
Kwa ufupi,
Ilikuwa ni kitendo cha uonevu mkubwa kwa mfalme mkubwa pamoja na jeshi lake kumwinukia mtawala mdogo mwenye watu wachache wakiwa katika mji mdogo. Kwa maana uwezo wa kijeshi wa mji huo mdogo ulikuwa ni hafifu,yaani mdogo sana, hawakuwa na uwezo mkubwa wa kujilinda kwa maana watu wake walikuwa ni wachache lakini pamoja na udogo wao,
bado wanainukiwa na mfalme mkubwa mbaya mwenye lengo la kuwaangamiza kabisa. Kuokoka kwa mji huu mdogo kulitegemea nguvu za Mungu tu kwa sababu mji ulikuwa na uwezo mdogo wa kujilinda. Hivyo Mungu alimwinua mtu mmoja maskini,akamjaza “nguvu ya hekima” ili kusudi auokoe mji.
Alikuwaje maskini auokoe mji ? Alitumia mbinu gani?
Bila shaka “nguvu ya hekima “ iliyokuwa ndani yake ilisababisha mji kuokoka na mkono wa adui yao. Huyu maskini alikuwa na “ufunuo wa roho “ juu ya kuuponya mji wake. Kwa maana ufunuo wa roho wenye kubeba jawabu katika mazingira magumu ni “ nguvu ya hekima “.
Hivyo,biblia haisemi kwamba maskini alitumia silaha za kivita au alitumia jeshi kuokoa mji, la hasha! Lakini alichotumia kama silaha yake ya ushindi ilikuwa ni “ nguvu ya hekima ya Mungu “ . Kumbe hekima ya Mungu ni zaidi ya silaha za kivita ziletazo ushindi,
ndio maana kuna wakati mwingine kama unataka ukoke na mabaya aliyopangwa kwako,unahitaji hekima tu.
Kwa maana watesi wako hawawezi kushindana na hekima ya Mungu ( Luka 21:15) Hivyo mtu aweza akawa na “nguvu ya hekima “ lakini ni maskini tu wa kawaida! na kwa bahati mbaya hata akawa hasikilizwi. Lakini umaskini wake hauwezi kuzuia kile alichobeba moyoni. Biblia inasema watu wa mji hawakumkumbuka,Tena walimdharau kwa sababu ya umaskini wake.
Lakini Mungu hakumsahau,wala hakumdharau kwa maana Mungu alimtumia na umaskini wake. Neno hili linatufundisha,kwamba mtu anaweza akadharaulika na jamii yake kwa sababu ya umaskini wake,lakini Mungu kamwe hawezi kumdharau maskini,Yeye uwainua waliodharauliwa.
Lakini pia, Neno linatufundisha kwamba “ usimdharau mtu hata katika umaskini wake kwa maana hujui amebeba nini ? Kwa maana huyo anayeonekana ni maskini na kudharaulika aweza kuokoa mji mzima”
Kumbuka ;
Bwana ameahidi kuwapa wanafunzi wake “ kinywa na hekima ” ili iwasaidie pale wapitapo katika mazingira magumu ( Luka 21:15). Ahadi hii ni ya kwako pia,kwa maana ikiwa wewe ni mwanafunzi wa Yesu na tena kuna mazingira magumu ya kuinukiwa na watesi wako,basi hapo unahitaji nguvu hii,ili watesi wako wasiweze kushindana nayo.
Ukumbuke biblia inasema kama mtu akipungukiwa na “hekima” na aombe ( Yakobo 1:5). Hii ina maana,maombi ni lazima ili ujazwe nguvu ya hekima ndani yako.
Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi nipigie sasa kwa +255 683 877 900.
What’s app+255 746 446 446.
Na Mch. Gasper Madumla
UBARIKIWE.
Comments