“ROHO MTAKATIFU AKASEMA…”
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 23, 2022
- 2 min read
Updated: Aug 26, 2022

Kwa ufupi,
Nataka uone neno hili “Roho mtakatifu akasema” ili uweze kuelewa kwamba Roho mtakatifu ana uwezo wa kunena / kusema . Biblia inasema Roho mtakatifu “ alisema ” kipindi ambacho manabii na waalimu walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada halisi. Hivyo mazingira ya ibada ya mitume na waalimu ilimruhusu Roho mtakatifu “kusema “ . Neno hili linatufundisha kwamba kuna mazingira ambayo ukiyatengeneza yanamruhusu / yanapelekea Roho mtakatifu kusema.
Kumbuka,Roho mtakatifu ni Mungu,hivyo hazuiliwi na mazingira au mipaka yoyote,lakini pamoja na hivyo Yeye hutumia ibada halisi kama jukwaa la kusema atakayo. Ni dhahiri kabisa ibada ya mitume na waalimu ilijawa na uwepo wa Mungu,kiasi kwamba Roho mtakatifu hakuchelewa kusema alichokusudia kusema. Ibada hiyo,iliyofanywa ilikuwa ni ibada ya “kufunga na kuomba “ kama ilivyoandikwa.
Lakini kwa nini Roho mtakatifu ajichagulie ibada ya namna hiyo ya “kufunga na kuomba “ ili aseme na watumishi wake? Si angeliweza kusema nao wakati wowote au angeliweza kujichagulia ibada nyingine ili afikishe ujumbe wake ?
Ukweli ni kwamba Roho mtakatifu aliona mioyo yao wale waifanyayo ibada hiyo ya kufunga na kuomba,bila shaka alipendezwa na “ibada halisi “ naye akaitumia ibada halisi kama pulpit/ madhabahu ya kusemea . Hivyo kikubwa ilikuwa ni mioyo iliyokuwa katika uhalisia wa kufunga na kuomba katika roho na kweli,namna hiyo kulimpa nafasi Roho mtakatifu kusema.
Je Roho mtakatifu anasema hata leo kwenye ibada za mifungo na maombi?
Ndio, anasema hata leo,lakini ni mara chache mno kwa sababu ibada nyingi zinazofanyika leo si halisi yaani ibada nyingi za mifungo na maombi zimepoteza uhalisia,nyingine ni kama maigizo fulani hivi.
Kwa sababu hiyo Roho mtakatifu naye huwa kimya akiwaacha waigizaji waendelee na maigizo ya ibada zao za kufunga na kuomba. Hivyo si kana kwamba Roho hasemi,maigizo yanapofanyika naye huwa kimya.
Roho mtakatifu anasema kwa namna gani?
Yeye hutumia sauti ya kawaida yenye kuelewaeka kwa kusudi la kuimarisha ufalme wake. Kwa mujibu wa neno,inawezekana kabisa Roho mtakatifu alisema kwa kinywa cha mmoja wa mitume au waalimu. Lakini Roho mtakatifu ana njia nyingi za kusema nasi,moja ya njia ni kuisikia sauti ya ndani yako hasa hasa pale unapokuwa uweponi mwake. Lakini katika njia hii mazingira ya uwepo wa Bwana ni muhimu sana.
Kumbuka kwamba ikiwa Bwana atapewa nafasi ya kuabudiwa ipasavyo,basi Roho mtakatifu naye atajihudhurisha na kusema ya kwake. Roho mtakatifu aliposema na mitume na waalimu alisema kuhusu “kazi ya ufalme “ akitaka atengewe watu aliowachagua Barnaba na Sauli/Paulo. Hii yote ni kuonesha kwamba kusema kwa Roho kunahusiana na kazi ya ufalme wake hasa.
Jiulize; Je una kiu ya kumsikia Roho mtakatifu? Je unatamani kuelekezwa na Roho mtakatifu? Ikiwa jibu ni ndio,basi jitahidi kutengeneza mazingira ya ibada halisi mahali ulipo Kwa maana ibada halisi hasa ibada ya kufunga na kuomba inavuta uwepo wa Mungu kwa haraka.
Kwa msaada zaidi waweza kuwasiliana nami kwa +255 683 877 900.
What’s app+255 746 446 446
Mch. G. Madumla
UBARIKIWE
コメント