ROHO,NAFSI NA MWILI
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 25, 2017
- 6 min read
Updated: Sep 30, 2022

Na Mch.G.Madumla
“… nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” 1 Wathesalonike 5:23
Kwa ufupi,
Ukweli ni kwamba maneno haya matatu ( roho,nafsi na mwili) yanatofautiana kila moja, ingawa wakati mwingine yanapotumika yanaweza yakawa na muingiliano wa kimaana,kwa mfano neno “nafsi” linaweza kutumika kwa maana ya kutaja neno “mtu” Kutoka 1:5
Pamoja na hivyo,bado matatu haya yanaonekana kwenye baadhi ya vifungu vya Biblia kubeba maana tofauti hasa pale yanapotumika yote kama kifungu hiki;
“ Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” Waebrania 4:12.
Jambo la kwanza muhimu ni kuelewa kwamba maneno haya yanapotajwa yanamzungumzia mwanadamu hasa mwanadamu aliye hai. Kwa maana mwanadamu aliumbwa katika pande tatu roho,nafsi na mwili.“ BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi,
akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwanzo 2:7. Sasa “ Neno mavumbi ya ardhi” imetafsiriwa kama nyumba au gamba ambalo Bwana Mungu aliliumba kisha akapulizia puani pumzi “ pumzi” ndio uhai wenyewe au ndio roho yenyewe. Hivyo roho ya mwanadamu ni pumzi ya Mungu. Biblia inasema tena “mtu akawa nafsi hai” Sasa waweza kujiuliza mtu ni nani? . Kwa mujibu wa andiko hili,mtu halisi ni roho.
Mwanadamu ni “roho” yenye kuishi ndani ya “mwili na nafsi”. Na ndio maana roho ikitengana na mwili watu husema fulani amefariki dunia, sasa huyo fulani ni nani? Mwili pasipo roho umekufa ( Yakobo 2:26). Na ndio maana ukienda kwenye msiba na ikiwa marehemu hajafikishwa utawasikia watu wakisema “mwili wa marehemu umeshafika?” Sasa huyo mwenye mwili/marehemu ni nani kama si roho? na ndio maana watu hapo husema mwili wa marehemu fulani
I.) ROHO.
Neno hili “roho” katika lugha ya Kiyunani huitwa “ Pneuma” humaanisha “pumzi” . Pumzi ya namna hii ni pumzi iletayo uzima sawa sawa na vile alivyopulizia mavumbi ya ardhi mtu akawa nafsi hai,kama vile Ezekieli alivyoipulizia ile mifupa mikavu nayo ikaishi ( Ezekieli 37:9 ) kawaida ya roho haionekani kwa macho ya nyama. Roho ndio itiayo uzima (Yoh.6:63). Hivyo roho ni sehemu ya mtu ina ufahamu wa Mungu kwa sababu kinachotakiwa kumuabudu Mungu ni roho. roho ya mwamini inashughulika na kazi zifuatazo ( hizi ni baadhi ya kazi za roho ya mwamini) ;
01.Kazi ya ufunuo.
Habari ya ufunuo hufanyika katika roho,maana hayo ni mambo ya rohoni. Ufunuo uhusisha roho ya mwamini,(Nafsi wala mwili haviwezi kubeba ufunuo). Tunaweza tukamwangalia mtume Yohana alipokuwa katika roho akachukuliwa na maono ( Ufunuo1:9). Au weweza kusoma habari za Ezekieli nabii aliyekaa rohoni mara nyingi zaidi.
2. Kupenda au kuchukia –
Roho huitwa pia ni “Moyo ”,mtu hupenda kwa moyo. Kuonesha kwamba upendo ni suala la moyo,lakini pia chuki ni suala la moyo. Rohoni / moyoni ndipo hasa kwenye harakati zote za maisha ya mtu.
03. Kazi ya mawasiliano na Mungu / Maombi
“ kazi ya mawasiliano na Mungu” huweza kuwa ni kwa njia ya maombi,kwa maana maombi ni mawasiliano ya roho ya mwamini na Mungu wake. Au huweza kuwa ni kwa njia ya kuabudu . Kwa kuwa Mungu wetu ni Roho,nasi ni lazima tuwe rohoni tutakapo wasiliana na Mungu. Hivyo kazi ya roho ya mwamini ni kufanya mawasiliano na Mungu. Unajua hatuwasiliani na Mungu wetu kwa kutumia miili yetu,au nafsi zetu bali mioyo/roho zetu. Jifunze kwa Yesu Yeye aliweza kuwasiliana na Mungu mara kwa mara kwa kuwa alikuwa rohoni au kwa lugha nyepesi twaweza sema kuwa roho ya Yesu ilikuwa connected/imeungamanishwa na Mungu kwa mawasailiano.
03.Dhamiri.
Neno dhamiri ni nia ya ndani au utu wa ndani mwa mtu. Dhamiri ni mtu wa ndani ya mtu. Mfano tuangalie hapa,wale waliotaka kumuangamiza yule mwanamke aliyefumaniwa wakati wakizini,walipofika kwa Yesu Yesu aliwaambia Yeye asiyekuwa na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe,kisha wale watu wote wakakimbia mbele yake. Kile kilichowafanya wakimbie ni dhamiri ziliwashuhudia ya kwamba wao pia ni watenda dhambi tena watenda dhambi wakubwa (Yoh.8:9). Dhamiri ni kazi ya roho kwa maana dhamiri haifanywi na mwili wala nafsi
II) NAFSI.
Neno “nafsi” katika lugha ya Kiyunani huitwa “Psuche” lenye maana ya ``akili na hisia”. Huu ni ule ufahamu wa mtu mwenyewe. Nafsi ya mtu inaweza kuhuzunika,kufurahi.N.K( Neno hili mara nyingine litumikapo katika biblia humaanisha moyo,lakini inategemea na andiko lenyewe). Angalia mfano; pale unapoweza kujifahamu wewe ni nani? Upo wapi? Au ni nini unachokiona n.k vyote hivyo hushughulikiwa na nasfi. Au Je hata sasa unafikiri nini? Kile unachokifikiria ni kazi ya nafsi yako. Katika mambo ya kiimani,hatuwezi kutumia nafsi kuwasiliana na Bwana bali kwa njia ya roho.
Zifuatazo ni baadhi ya kazi za nafsi ya mtu.
01.Kufikiri.
Kazi hii ya kufikiri hufanywa na nafsi,au kutafakari ni kazi ya nafsi yako. Fikra ya mtu ni zao la nafsi yake. Mwamini yeyote ni lazima kuzitawala fikra zake zipate kumtii Kristo,kufikiri kunamfanya mtu kuyakumbuka yale yote yaliyopita.
02.Hisia / Kuhisi
Kuhisi kunafanywa na nafsi. Nafsi ya mtu huweza kupata furaha n.k lakini Yesu anasema hapa ; “ Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;” Mathayo 11:29
neno “ nanyi mtapata raha nafsini mwenu” lina maana ya raha ( Joy) na sio raha ya Happyness ( kwa sababu kuna furaha ya kawaida ya kitambo tu kiingereza huitwa happyness,,lakini kuna furaha ya ndani,ya kudumu inayopatikana ndani ya Yesu tu huitwa Joy). Ingawa biblia imeeleza “ raha nafsini mwenu” bali ina maana ya “raha mioyoni mwenu“
03.Utashi ( na suala la kuamua)
Hivi unajua wanyama hawana utashi bali ni kwa binadamu tu. Mungu ametuumba kwa jinsi ya ajabu tena ya kutisha,ametupa utashi tuweze kufanya maamuzi. Na ndivyo ilivyo Mungu ametushirikisha kufanya maamuzi ya kuchagua au kutokuchagua soma “ Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;” Kumb.30:19
III)MWILI.
Neno“ mwili ” katika lugha ya Kiyunani ni “ Soma” humaanisha “ gamba la nje,au mavumbi ya ardhi yaliyofunika pumzi ya Mungu”. Mwili ni hili gamba la nje la mwanadamu lionekanalo. Mwili wawaza kupendeza na pia waweza kuchukiza inategemea na sababu nyingi ( Sababu za kiroho na za kimwili). Kiimani,kila aufuatae mwili anataka kufa. Siku zote Roho hupingana na mwili ( Wagalatia 5:16-17). Mtu wa mwilini ni yule asiyemjua Mungu wa kweli,mwenye kuyafuata matendo ya mwili, matendo ya mwili ni kama vile uesharati,uchafu,ufisadi,ibada ya sanamu,uchawi,uadui,ugomvi.N.K ( Wagalatia 5:19-21)
Tabia ya mwili kwa kila mtu ni Kiburi,kujiinua,kupenda starehe.n.k
Je unajua ya kwamba kila mtu anaasili ya kiburi ndani yake? Maana kila mwili wa mwanadamu unapenda kusifiwa,kupendeza kujidai kuliko mwingine. Hata wewe usomaye ujumbe huu,una tabia hii ya asili ya kiburi ndani yako. Ila tabia hii ya kiburi inagandamizwa na Roho mtakatifu na sio kufutwa kabisa kwa sababu ikiwa utamuacha Bwana kiburi kitaibuka na hali yako itakuwa ya kiburi kama hapo kwanza kabla ya kuokoka kwako. Roho mtakatifu anagandamiza kiburi kiasi kwamba haionekani kabisa kwa yule aliyeokoka na kumaanisha katika wokovu wake. Lakini ikiwa hujaokoka itaonekana tu,ni muhimu sana uokoke na
kudumu ipasavyo katika wokovu ili tabia za asili zisifanye kazi tena ndani yako.
B.MAHUSIANO YA ROHO,NAFSI NA MWILI.
Kwa kuwa sehemu hizi tatu zinamkamilisha mtu,basi ni muhimu kujua mahusiano yake yanakuwaje. Tuanze na mahusiano kati ya Nafsi na mwili. Husiano mkubwa unaonekana kwa wepesi ni pale ulipo-okoka. Ukiokoka,roho yako ndiyo huzaliwa kwa mara ya pili,nafisi wala mwili havizaliwi mara ya pili. Ni sawa kabisa na kusema ya kwamba nafsi na mwili haviokoki wakati ule roho yako inapookoka.
Mfano mzuri unaweza ukaona mtu/roho imeokoka lakini mtu akawa bado ni mlevi au mwenye tabia za zamani hazijamwacha bado,hii yote ni kudhihilisha kwamba nafsi na mwili havijaokoka. Sasa ukiwa katika kudumu ndani ya neno la Kristo,hapo ndipo Nafsi hubadilishwa na kuanza kufanana na roho yako iliyokuwa imeokoka.
Na badiliko hilo la nafsi hupelekea mwili kugeuzwa hata kuanza kufanana na roho. Zoezi hili halifanyiki kwa siku moja,isipokuwa ni roho pekee ndio hupokea badiliko kwa siku moja ulipookoka.
roho na nafsi.
Hivi viwili hushindana kila kimoja. Kwa maana kila kimoja chaweza kuwa boss wa mwili. ( Kwa maana mwamini aweza akaongozwa kwa roho akawa rohoni au akaongozwa na nafsi yake akawa mwilini ). Hivyo huu ni uhusiano wa ndani. Dhambi ndio adui wa roho ya mwamini kufanya kazi ya Mungu katika utimilifu,hivyo roho ya mtu isipookoka haiwezi kutenda mambo ya Mungu/kumlingana Mungu bali nafsi ataitawala kuamuru mwili ufuate matendo yake(matendo ya mwilini)
Nafsi ikiisha kupokea taarifa,hufikiri na kufanyia maamuzi lakini ikiwa roho ya mtu ikiwa imepokea Yesu,maamuzi yale ya nafsi yanaweza kubatilishwa na roho pamoja na Roho (Roho wa Bwana uleta maamuzi mengine. Hivyo wakati wa kuokoka,kinachookoka ni roho,kisha nafsi na mwili wako hutakaswa kwa Neno. Kumbuka hilo ni jambo muhimu sana.
Somo hili bado ni mbegu,litaendelea
Na Mch.G.Madumla.
Kwa huduma ya maombezi piga +255 683 877 900.
What’s app +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments