top of page

ROHO MTAKATIFU KATIKA KAZI YA KUREJESHA TUNDA LA ROHO.

Bwana Yesu asifiwe…

Fundisho hili,limefundishwa na Pastor Gasper Madumla ndiye niliyekuandikia haya yote upate ufahamu~ Bible fellowship church Jumapili ya tar.12 Nov.2017.

Kwa ufupi.

Roho mtakatifu anafahamu vizuri ya kwamba tunda lake halimo ndani yako ingawa umeokoka siku nyingi. Kwa sababu kuokoka ni kitu kingine na tunda la Roho ni kitu kingine. Na ndio maana anataka aumbe upya tunda lake ndani ya moyo wako;ili kusudi sasa uweze kuenenda katika Roho kwa maana utakapoenenda katika Roho,kamwe huwezi kutimiza tamaa za mwili wako.

Siku zote mwili umejawa na tamaa za namna nyingi hata kushindana na Roho mtakatifu,na ndio maana adui wa kwanza wa Roho mtakatifu sio shetani bali ni tamaa za mwili wako. Kwa sababu yale ambayo Roho anataka uyafanye,wewe huyafanyi tamaa za mwili zimechukua nafasi zaidi ya Roho,na ikiwa ni hivi,basi kuna sababu;Warumi 7:15-20

Kwa sababu ya ile dhambi iliyopo ndani yako,na hapo ndipo sasa matendo ya mwili huja. Matendo ya mwili ni yapi hayo? Soma Wagalatia 5 :19-21

Unaweza kweli ukawa umeokoa lakini bado unaishi katika matendo ya mwili,basi ujue huna tunda la Roho. Na hili ndilo tatizo letu tulio wengi,tumeokoka lakini bado tuna uadui, tuna ugomvi, hasira, wivu, fitina n.k na ina maana ya kwamba hatuna tunda la Roho. Tunamuhitaji Roho mtakatifu atusaidie kuumba upya tunda la Roho.

Mojawapo ya kazi ya Roho mtakatifu aifanyayo kwako ni kurejesha tunda la Roho ndani yako. Kazi hii ikiwa ni kazi ya pili ya Roho mtakatifu. Kazi ya kwanza ya Roho mtakatifu ni kuuhakikishia ulimwengu kwa habari ya dhambi,haki na hukumu kama ilivyoandikwa katika injili ya Yohana 16:8.

Hii ni wiki ya kupokea ujazo wa Roho mtakatifu kwa kanisa na mtu mmoja mmoja. Na ndio maana Roho mtakatifu anataka apewe nafasi ya kutosha katika ibada zetu. Hivyo basi ni vyema tunapoanza kujifunza Roho mtakatifu katika urejesho wa tunda la Roho kama kazi ya pili ya Roho mtakatifu,tukamjua vyema huyu Roho mtakatifu ni nani haswa? Hivyo; Kwa mujibu wa neno la Mungu, tunaweza kumuelezea Roho mtakatifu katika maana kuu tatu, kama ifuatavyo;

01.Roho mtakatifu ni Mungu halisi.

“Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. ” Matendo 5:3-4. Soma pia 2 Wakorintho 3:17,Yoh.4:24

Ana sifa ambazo Mungu pekee ndio mwenye nazo;

  1. Asili ya umilele- Waeb.9:14

  2. Yupo kila mahali – Zab.139:7-10,Yoh. 14:16

  3. Anafahamu yote -1 Wakorintho 2:10-11

  4. Anaweza yote ( Mathayo 10:17-20)

  5. Yeye ni mkweli na mwaminifu ( Yohana 14:17)

02. Roho mtakatifu ni nafsi hai.

Mojawapo ya tabia ya kila nafsi ni kuwa na uwezo ni kuhisi na katika eneo hilo anaweza kufurahishwa,au anaweza akahuzunishwa. Na ndio maana tunaonywa ya kwamba tusimuhuzunishe Roho mtakatifu katika kitabu kile cha Waefeso 4:30

Ana sifa zote za kuwa nafsi hai. Nazo ni kama ifuatavyo;

  1. Anaweza kuona – Matendo 16:7,8:18-20 ( Roho mtakatifu aliyekuwa ndani ya Petro aliona moyo wa Simoni)

  2. Anaweza kufariji – Matendo 9:31

  3. Anaweza kuongea – Matendo 13:2, Yohana 16:13

  4. Anaweza kuomba – Rumi 8:26

  5. Anaweza kufundisha na kukumbusha – Yoh.14:26

03. Roho mtakatifu ni nguvu hai ya Kiungu inayotenda kazi ndani ya mwamini, isiyoonekana kwa macho bali kwa matendo yake. Matendo 2:1-4 (ni kama vile upepo usionekana kwa macho bali tunaona matokeo yake.) Lakini pia Yeye Roho mtakatifu ni msaidizi wetu wa karibu sana Yohana 14:16

Sasa;huyo ndio Roho mtakatifu ninayemzungumzia ambaye Kwa huyo ana kazi ya kurejesha tunda la Roho ndani yako baada ya kuokoka. Tunda la Roho,ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,upole pamoja na kiasi;….” Wagalatia 5:22-23

Mwanadamu aliumbwa kwa “mfano” na kwa“sura” ya Mungu Mwanzo 1:26. Mwanadamu ni roho mwenye nafsi aishiye ndani ya mwili. Jinsi alivyo Mungu ambaye ni Roho ndivyo alivyo mtu. kwa mfano wa Mungu,mtu aliumbwa. Hii ina maana kwamba kulikuwa na mfanano mkubwa kati ya Mungu na mtu. Huo ndio “ mfano wa Mungu” lakini neno linasema pia mtu aliumbwa na kwa sura ya Mungu

Sasa, sura ya Mungu ni ipi?

Tunda la Roho ambayo ni tabia ya Mungu,Na tabia ya Yesu,Ni tabia ya Roho mtakatifu ndio sura halisi ya Mungu. Yale mambo tisa“ upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,upole, kiasi; ” yanayotengeneza TUNDA la Roho ndio sura halisi ya Mungu. shetani anaweza kuiga mambo yote lakini hana uwezo wa kuiga tunda la Roho.

Hivyo basi mwanadamu aliumbwa akiwa na mfanano na Mungu,na akiwa na ushirika mkubwa kwamba mwanadamu amuwakilishe Mungu hapa duniani. Yale yote mambo tisa mwanadamu aliumbiwa nayo toka awali. Soma Waefeso 2:10

Baada ya dhambi, shetani ndiye aliyepanda matendo ya mwili nayo matendo ya mwili ndiyo haya Wagalatia 5:19 ( angalia baada ya anguko mauaji yakaanza kutokea). Lakini Roho mtakatifu amekuja kuumba upya tunda la Roho ndani yako kwa kufisha matendo ya mwili. Wewe mwenyewe huwezi kuyafisha matendo ya mwili bila Roho mtakatifu otherwise utakuwa unaigiza tu!

Kumbuka tangia mwanzo uliumbiwa upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,upole pamoja na kiasi;. Lakini sasa jiulize upendo uko wapi kwako? Furaha ipo wapi kwako? Amani ipo wapi kwako? Na pamoja na mengine. Kama ilivyokuwa kwa Adam kupoteza mfanano pamoja na sura ya Mungu kwa sababu ya dhambi na ndivyo ilivyo kwako na kwangu tumepoteza sura ya Mungu kwa sababu ya dhambi au kwa sababu ya kushindwa kumpa nafasi ya Roho mtakatifu katika maisha yetu.

Unamwitaji Roho mtakatifu arejeshe na aumbe tena tunda la Roho ndani yako.

Sasa tufanye nini ili tuweze kupata tunda la Roho ? Ni kwa namna gani Roho mtakatifu anaweza kukurejeshea tunda lake?

01. Kwa kuzaliwa upya kwa mara ya pili. ( Kuokoka)

Unapookoka unapewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu (Yohana 1:12). Tukio moja kubwa linalotokea siku hiyo unapookoka kwa kuoshwa dhambi zako na kumpokea Bwana Yesu awe Bwana na mwokozi wako,ni tukio la Roho mtakatifu kuingia rasmi ndani yako. Hapo ndipo safari yako na Roho mtakatifu inapoanzia,nje ya hapo hakuna safari naye. Kuzaliwa kwa mara ya pili ndio asili ya mema, asili ya kurejeshewa tunda la Roho. Lengo kuu katika hatua ya kwanza ni kuhakikisha unarejeshwa katika usafi wa moyo kwa toba.

02.Kwa njia ya Neno na maombi katika Roho.

Roho mtakatifu huwa anasubiri neno liwepo ndipo na Yeye afanye kazi yake. Nje ya neno hakuna kazi ya Roho mtakatifu (Mwanzo 1:1-3). Mahali penye neno halisi ndipo penye Roho wa Bwana. Ukihitaji tunda la Roho huna budi kudumu katika neno. Pili, maombi ni muhimu sana kwa ajili ya kupata tunda la Roho. Maombi katika Roho ni zaidi ya maombi ya kawaida. Maombi katika Roho ni yale yanayompa kipaumbele Roho mtakatifu awe ndiye bosi na controller. Ndio maana watu wanaweza kunena na kumuachia vyema kwa sababu ya Roho mtakatifu akipewa nafasi ya kutosha ( Waefeso 6:18)

03. Kujizoesha kutembea katika tunda la Roho.

Mambo ya kiroho yanahitaji mazoezi sana. Mfano ukihitaji kuwa na pendo, uvumilivu kama sehemu ya tunda la Roho, huna budi kuanza kujizoeza kupenda na kuvumilia kwa yote huku ukimuomba Roho mtakatifu akusaidie. Yeye Roho mtakatifu ni msaidizi wako, hivyo lazima uoneshe unahitaji kujizoeza katika hayo yote.

Katika hatua bhii tunapaswa kuutunza utakatifu.

Lakini kwa nini tunda la Roho ?

  1. Tunalihitaji tunda la Roho kwa sababu tusiwe tena chini ya sheria Wagalatia 5:23

  2. Kwa sababu ndio sura halisi ya Mungu wetu

Na Mch Gasper Madumla

+255 683 877 900

Namba ya WhatsApp ni .+255 746 446 446

UBARIKIWE

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page