PUNDA MALANGONI MWA YERUSALEM
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 21, 2016
- 3 min read
Bwana Yesu asifiwe…

Unakumbuka,Bwana Yesu alimpanda punda wakati anaingia Yerusalem? Bila shaka utakuwa unakumbuka hilo,Sasa swali linakuja hivi; Kwa nini punda? Kwa nini asingechaguliwa mnyama mwingine? Je kuna mafunuo yoyote juu ya punda aliyepandwa na Yesu?
Au kwa nini Bwana Yesu asimpande punda,bali Yeye akampanda mwana-punda. Kwa maana ipo tofauti hapo kati ya punda na mwana-punda ingawa wote ni punda. Sijui kama umeshawahi kujiuliza hivyo. La! kama bado hujawahi kujiuliza,emu sasa jiulize swali hilo.
Awali ya yote,nikueleze kwamba habari hii ni miongoni mwa habari nzuri iliyoandikwa na wana injili wote wanne yaani Mathayo 21:1-11,Marko 11:1-10,Luka 19:29-40 na Yoh.12:12-19.Hivyo basi wote wanne wameandika,kwa maana zipo habari njema nyingine zimendikwa kwa mwana injili mmoja tu, mfano habari ya kufufuliwa kwa Lazaro,imeandikwa katika Yoh. tu.
Kwa nini ni mwana-punda isiwe ni punda?
Neno hili“mwana-punda” limebeba majina mawili yenye maana mbili tofauti ukiwa utalitenga,yaani “ mwana” na “punda“. Katika tafsiri nyepesi ya neno hili pale linapotumika kwa pamoja lina maana ya mtoto wa punda.
Lakini mtoto huyu wa punda si mtoto kama mtoto bali ni “mwana” yaani ni yule mwenye nguvu,mchapakazi na aliye na uwezo mkubwa wa kutoyumbishwa,amekuwa “mwana” ingawa anaweza akawa ni mdogo.
Ukiangalia jina hili kwa upana huo wa “mwana” ikiwa kama utalitenganisha,utagundua kwamba nafasi ya uwana ni tofauti na nafasi ya utoto. Lugha ya kiingeleza imefahuru kutofautisha vizuri majina haya mawili “mtoto na mwana” yaani “ child and son”
Angalia jinsi ilivyoandikwa hapa; “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Yoh.1:12. Biblia ya kiingeleza,inasema “children of God” sio “Sons of God”
Kwa sababu unapompokea Yesu unapewa uwezo wakufanyika mtoto,bali ukidumu kwake utafanyika “mwana” Neno “watoto” waliozungumziwa hapo sio “wana” bali ni watoto,yaani ni wale ambao wapo chini ya uangalizi kwa kuwa hawajakua kufikia hatua ya kuwa wana. Wana ni wale wenye kukua kiroho na ambao wanaoongozwa na Roho wa Mungu (Warumi 8:14)
Muangalie Yesu,anaitwa “mwana wa Mungu” angalia tena wale wote wanaomfuata kufanya mapenzi yake sawa sawa na alivyowaagiza,yaani wapo kama Yeye huitwa “wana-funzi“.
Hivyo,neno hili “mwana-punda” linaonesha nafasi ya uwana imehusika ingawa bado maana ya kwanza ya mtoto wa punda ipo vile vile. Tukichua tafsiri sahihii ya “mwana” inaonesha kuwa Yesu huwatumia “wana” katika kazi yake.
Yaani Yesu huwatumia watu wanaoongozwa na Roho wa Mungu katika kazi yake. Kuna mchakato wa kutoka katika hali ya utoto hadi ya uwana,kiasi kwamba unamsikia Roho wa Mungu wazi wazi.
Sasa,kwa nini alimtumia mwana-punda na sio farasi?
Zinawezakana zikawa sababu nyingi sana,lakini pia nami nalipofikiri swali hili nikagundua baadhi ya sababu. Kwanza kabisa yafaa kuangalia sifa za kawaida za farasi na punda. Kwa desturi ya kiyahudi,Farasi alikuwa ni mnyama anayepandwa na wafalme. Wafalme walitumia farasi kama sehemu ya usafiri wa kiheshima.
Lakini pia,farasi alitumika katika vita;wapiganaji waliwatumia farasi waendapo vitani. Hivyo desturi hizi mbili,zinaonesha kuwa mwenye kumpanda farasi kisha kuingia katika mji alikuwa akiogopwa,anatishia hata usalama wa watu.
Laiti Yesu angelimtumia farasi pale alipoingia Yerusalemu na kusanyiko lote lile lilokuwa likimfuata,basi angeonekana kama vile ni mfalme wa dunia hii kama wafalme wengine wafanyavyo,tena hata watu wangetishika kidogo.
Badala yake alitumia punda kuonesha Yeye sio mfalme wa dunia hii,bali Yeye ni mfalme wa wafalme,Mungu mwenye nguvu. Tabia ya punda ni kubeba mizigo ya watu,Yesu anaonesha wazi wazi kwamba Yeye ni mbeba mizigo yetu ya dhambi (Mathayo 11:28-30).
Yaani ni kama vile Yesu alijipanda mwenyewe,kuonesha Yeye ndio achukuae mizigo yetu ya dhambi. Hivyo kupitia mwana-punda huyu aliyepandwa na Yesu kwa mara ya kwanza,tunajifunza mambo yafuatayo tukimwangalia Yesu. Jambo kubwa lililofundishwa na wana injili wanne ni kwamba,Yeye Yesu ndie mfalme wa amani.
(i)Katika Mathayo 21:1-5; Yesu ni mfalme wa amani naye ni mpole~Punda huwakilisha amani sio fujo wala vurugu za farasi. Yeye Yesu ndie amani yetu( Zekaria 9:9,Isaya 9:6)
(ii) Katika Marko 11:9;Yesu ndie Mwokozi,aliyebarikiwa na amekuja kwa jina la Bwana~Watu walishangilia “utuokoe,utuokoe…” ikiwa na maana kwamba hakuna wokovu mahali pengine isipokuwa kwake tu,Kristo Yesu.
(iii) Katika Luka 19:37-38;Yesu ndie aliyejaa matendo na uweza mkuu,maana watu waliuona,wakashakilia. Kuonesha mbingiuni kuna amani,na utukufu mkuu
(iv) Katika Yoh.12:14-15,Yesu ndie mfalme aletaye ufalme kwako,usiogope na ufungue moyo apate kuingia.
Mungu huwatumia wanyonge kuwahaibisha wenye nguvu,tazama alivyoweza kumtumia punda aliyekuwa wa chini,akamfanya watu wamshangilie Yeye kupitia punda. Hata leo,bado Mungu huwanyanyua wanyonge kutoka mavumbini na kuwaketisha na wakuu (Zab.113:7-8)
Lakini nachelea kumaliza,ninasema hivi,huyu punda alikuwa kifungoni. Yesu akaagiza afunguliwe na apelekwe kwake kwa ajili ya kazi ya Yesu. Hata leo wapo watu waliofungwa kiroho,ambapo Bwana asema nawe nenda kawafungue kisha uwalete kwake kwa utumishi wa Mungu.
Mimi najiuliza kama wale wanafunzi wake Yesu wasingefanya kazi ya kutoka kumfungua mwana-punda,Je mwana-punda angefikaje kwa Yesu? Kumbe kuna watu wengi waliofungwa tumewazuilia kuwaleta kwa Yesu kwa sababu hatujatoka,Mungu atusaidie. Chukua hatua sasa ya kuwafikia wale wote walio kifungoni walete kwa Yesu.
Ikiwa unahitaji maombezi,jaribu kunifikia kwa namba hizi; piga sasa; +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments