top of page

PASAKA ( UKOMBOZI )


“Ukombozi / Pasaka”

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Sikukuu ya Pasaka ni sikukuu iliyoamriwa na Bwana kwa “amri ya milele” ( Kutoka 12:14). Leo,ulimwengu mzima unaadhimisha sikukuu hii kwa namna yake,lakini sisi tuliookolewa tuna namna yetu pia ya kuadhimisha ambapo sisi tuna ibada ya urejesho. Tukikumbuka “Kufufuka kwake Kristo ” ambaye kwanza,aliteswa,akafa,akazikwa na kisha siku ya tatu akafufuka katika wafu kama yanenavyo maandiko ( 1 Wakorintho 15:3-4). Tendo la kufufuka kwake ndilo hasa linatukutanisha sote kuwa kitu kimoja na hapo ndipo tunakamilishwa wokovu wetu.

Kufufuka kwake Kristo kulikuwa na viashilia viwili;

  1. Yeye yu hai,anaishi hata sasa. Leo,kama ukienda Israeli kwenye eneo la bustani ya “Garden tomb” ( mahali alipolazwa Yesu baada ya kufa) utakutana na neno hili “He is not here, he has risen yaani hayupo hapa amefufuka“

  2. Hakushikwa na uchungu wa mauti ( Matendo 2:24). Kaburi halikumweza.

Hivyo,tunapouangalia msalaba wa Yesu, tunauona ni msalaba ulio wazi,kwa maana Yesu hayo hapo,bali amefufuka. Tena,tunapolitazama kaburi la Yesu,tunaliona kuwa ni kaburi lililowazi,kwa maana amekwishafufuka,kama alivyosema. Huo ndio ukweli wenyewe,na katika ukweli huu,hatupaswi kuwa na huzuni tunapoingia kwenye sikukuu za Pasaka hata kama ni Ijumaa kuu,huzuni ziwe mbali nasi kwa maana Yesu Yeye alikwishafufuka mara moja,hafi tena wala kuteswa tena.

Neno “ukombozi” limebeba maana mbili za msingi;

  1. Kurejesha kilichopotea.

  2. Kuweka huru kwa kulipia gharama kama “fidia” – Kristo alitukomboa maana yake alitoa uhai wake kama fidia -Mathayo 20:28,1 Timotheo 2:5-6,Waefeso 1:7

Kristo alitoa uhai wake,kwa maana ndio ukombozi wenyewe. Hata hivyo,sisi hatuelewagi wala kuona thamani ya kile kilichofanyika juu yetu.

  1. Pasaka kibiblia ni nini hasa?

Pasaka ni ukombozi halisi wa asili ya mwanadamu katika maeneo matatu,“kiroho,kimwili na nafsi”. Hakuna tafsiri muhimu ya kibiblia kuhusu Pasaka kama hiyo ya ukombozi. Maeneo hayo matatu yalimghalimu Yesu kuendea msalaba. Swali unaloweza kuwa nalo ni hili “ kwani katika hayo maeneo ni nini hasa kilikombolewa? “. Kumbuka, ili tuweze kujua ni nini kilikombolewa,ni lazima tujue kwanza ni nini kilipotea.

01.Kiroho.

Mwanadamu wa kwanza Adamu,aliumbwa kwa mfano wa Mungu na kwa sura ya Mungu ( Mwanzo 1:26). Alifanana na Mungu kwa mfano wake na kwa tabia ya Mungu ( sura ya Mungu). Alikuwa ni mkamilifu,mwenye haki,mtakatifu n.k. Hivyo alikuwa na “ushirika mmoja na Mungu” Biblia inaweka wazi juu ya uhusiano uliopo kati ya Mungu na mtu wa kwanza,;

“ Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone.“ Mwanzo 3:8. Andiko hili,linaonesha kuwa Mungu alikuwa na utaratibu wa kushuka na kuzungumza na mtu limwuumba. Kitendo cha kushuka na kuzungumza nao,ni kitendo cha“ ushirika mkubwa”

02.Kimwili – Maisha yao hayakuwa na kikomo cha kuishi. Wala hawakuwa na mgonjwa,mateso yoyote katika mwili. Hapakuwa na udhaifu wa kimwili wa aina yoyote.

03.Nafsi – Walipewa nguvu ya kumiliki ( Mwanzo 1:28). Hii ilikuwa nguvu ya kutawala vyote vilivyoumbwa na Bwana Mungu, isipokuwa kuwatala watu.Hayo ndio mambo muhimu yalipokuwepo ndani ya Adamu.

  1. Lakini mara baada ya anguko la dhambi,nini kilitokea?

Katika kila nafasi,kulikuwa na upotevu. Kwa mfano,

01. Kiroho

Adamu alikufa kiroho saa ile ile alipoasi. Kwa maana tabia ya dhambi ni kuleta mauti kama malipo yake. Hata leo,dhambi ikiingia ndani yako ujue utakufa kwanza kiroho ( Waefeso 2:1). Lakini pia,tokeo jingine lilikuwa ni kupoteza ule ushirika wa kiungu. Kwa hiyo,shida ikaingia kwenye roho ya Adamu. Ushirika haukuwepo tena!

02.Mwili -Mgonjwa yakaanza kuutawala mwili,uuaji nao ukaanza ndio maana tunaona tukio la mauaji likatokea,Kaini akainuka na kumwua mdogo wake. Mwili wa manadamu ukaanguka kwenye mateso mbali mbali,kiu na tamaa ya uovu ikainuka. Kisasi kikapanda ndani ya mtu,hata mtu na mtu wakawa maadui. Na kubwa zaidi,maisha yakafupishwa,kukawa na kikomo cha kuishi ( Mwanzo 3:19)

03. Nafsi – Mwanadamu akapoteza nguvu ya kumiliki/kutawala. Na hatimaye akaangukia kwenye laana ya umaskini na ufukara. Hata mtu akakosa kuwa na kikao duniani,akaanza kutangatanga. Na ndio maana baada ya dhambi Adamu alifukuzwa bustanini ( Mwanzo 3:24). Hii ni kusema; mwanadamu alitolewa kwenye chanzo cha utajiri ( ardhi iliyobarikiwa) na kuanza kutangatanga!!!

Sasa huyo,ndio Adamu wa kwanza mbaye amejipata kwenye shida nyingi na amepoteza mengi.

  1. Adamu wa kwanza alipoteza,na kuanguka.

  2. Lakini Adamu wa pili ni Roho yenye kuhuisha yaliyopotea.

  3. Adamu wa kwanza ni wa udongo,atoka katika nchi.

  4. Lakini Adamu wa pili atoka mbinguni.

  5. Adamu wa kwanza alianguka dhambini,

  6. Lakini Adamu wa pili hakutenda dhambi. ( soma hayo yote,1 Wakorintho 15:45-48)

.

  1. Adamu wa pili ni nani hasa?

Adamu wa pili huitwa pia Adamu wa mwisho kwa maana hakuna Adamu mwingine atakayekuja bali ni huyo aliyekwisha kuja. Adamu wa mwisho ndiye “Kristo“, Yeye alikuja kuonesha vile Adamu alivyopaswa awe. Kristo ndiye haswa Pasaka wetu ( 1 Wakorintho 5:7 )

Ni vyema ukafahamu kwamba Kristo ndiye ametukomboa katika roho kwa kuzaliwa kwa mara ya pili kwa lengo la kukomboa ushirika ule uliopotea. Lakini katika mwili,tusikamatwe na laana ya magonjwa,pia tupate kuwa na nguvu ya kutawala kwa maana Yeye mwenyewe ingawa alikuwa tajiri,lakini akafanyika maskini,ili sisi tuwe matajiri kwa umaskini wake – 2 Wakorintho 8:9

  1. Kusudi la ukombozi;

Ukombozi umebeba kusudi moja kwenye maeneo mawili;

  1. Kutoa nafasi ya kuhesabiwa haki bure kwa njia ya imani ( Warumi 3:24). Mwanadamu alikuwa hana nafasi ya kusimama mbele za Mungu kama mwenye haki,isipokuwa kwa njia ya msalaba nafasi hiyo ipo wazi kwake aaminie na kumpokea Kristo.

  2. Kututenga mbali na laana zote – Wagalatia 3:13.

Je ukombozi ulilenga kitu gani kingine. ?

  1. Kushughulikia “hukumu ya dhambi “. Kila aliyempokea Kristo anapaswa asitawaliwe na nguvu ya dhambi ( Wagalatia 6:14).

  2. Kuponywa magonjwa na udhaifu wa aina yoyote wa kimwili – Isaya 53:5

  3. Kurejesha ushirika wa kiungu. N. K

Ni muhimu sana kujua neno hili kwamba “ Katika kifo chake pale msalabani,Kristo alikuwa Mwana-Kondoo halisi wa Pasaka/ Ukombozi kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu. Na kufufuka kwake ni ushuhuda wa wazi unaoonesha kwamba yeyote atakayemwamini na kumpokea/kuzaliwa mara ya pili/kuokoka,basi hayupo tena chini ya utawala wa shetani bali amekombolewa”

Ukombozi huu ni mali yako,lakini huna budi kumwamini na kumpokea Kristo, uzaliwe mara ya pili ili kwamba uwe huru mbali na laana. Nafasi ya kuzaliwa upya ipo wazi sasa,waweza kuitumia nafasi hii leo,kwa kunipigia simu tu, ili tuombe pamoja. Ni vyema ukarejea kwenye wokovu leo,milango iko wazi kwako. Ukombozi huu ni wako!

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe na kwa MAOMBI piga sasa .+255 746 446 446

Pasaka njema!

What’s app ni +255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page