top of page

DAMU KWENYE KIZINGITI CHA JUU.- 2 (Tamati)


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Kitendo cha Waisraeli kupaka damu kwenye miimo ya milango, na juu ya milango yao ni kitendo kinachoashiria kwamba mnyama mmoja (Mwana-Kondoo) amekufa, kwa ajili wale walio ndani ya nyumba. Ukweli ni kwamba wale walio ndani ya nyumba walikuwa ni wenye dhambi kama watu wengine waliopigwa [ Kama biblia isemavyo,“mshahara wa dhambi ni mauti” Warumi 6:23,Hii ina maana kwamba hata wale wazaliwa wa kwanza waliojificha ndani ya nyumba hawakustahili kupona kwa sababu wote wametenda dhambi(Warumi 3:23) ]Hivyo hawakuokolewa kwa sababu ya matendo mema,wala kwa sababu yoyote inayotokana na mambo yao,isipokuwa kwa “ neema tu,kwa njia ya imani.” (Waefeso 2:8).

Mungu alikuwa amekusudia kuwaokoa watu wake,lakini kwa utaratibu fulani unaoweza kueleweka katika hali ya kibinadamu. Utaratibu wenyewe haukuwa mzito,bali ulikuwa kwanza watu waelewe kuwa “ukombozi/pasaka” ni kazi ya Mungu,lakini watu waweze kuamini tu,kisha wafanye sawa sawa na walivyoagizwa.Suala la imani lilihitajika sana,kwa maana halikuwa ni kazi ya Mungu,bali ni kazi ya Waisraeli. Yaani Mungu alitoa nafasi kwa watu waweze kuwa na “imani” ili wapokee ukombozi wao. Hata hivyo,bado kuna waliopotea kwa sababu hawakuweza kuamini damu/ukombozi.

Kumbuka,maelekezo ya kwanza yaliyotolewa yaliwataka,Waisraeli watulie ndani kila mmoja. Asionekane mtu anazulula zulula nje kipindi hicho cha usiku (Kutoka 12:22),nao wakatulia ndani hata asubuhi. Lakini hata leo,tumeshuhudia wengi wakiangamia kwa sababu ya kukosa utulivu wa kiroho (Wengine wamepigwa na adui,kwa kutoka kwenye wokovu).

“Damu kwenye kizingiti cha juu ya mlango” ilikuwa ni alama ya wazi ya kumzuia mwaribu asifanikiwe kupiga. Kristo ndiye haswa Pasaka mwenyewe,ambaye kwa damu yake,mwaribu hana nafasi ya tena ya uharibifu ( Waebrania 2:14)

“Damu kwenye kizingiti cha juu ya mlango” kitendo hiki,kilikuwa na maana kubwa katika ulimwengu wa roho,ingawa kilifanywa kwa jinsi ya mwili. Kumbe unaweza ukaona kitu kikifanywa kwa jinsi ya mwili na kumbe kimebeba kitu kikubwa kwenye ulimwengu wa roho. Kwa maana Wamisri walipowaona Waisraeli wakiangaika kupaka damu,hawakuelewa hata wakaona wajinga,watu wasio na maana. Hata leo,unavyoweza kuachilia damu ya Yesu kazini kwako,mtu mwingine asiyeelewa atakuona huna akili,lakini ujue ni kitu kikubwa sana kinachoenda kutendeka. Kwa hiyo usinyamazishwe na wasioelewa,wewe endelea tu.

“Damu kwenye kizingiti cha juu ya mlango” Tendo hili halikufanywa na watu wengine isipokuwa wale tu,ambao walikuwa ni watu wa Mungu. Kumbe,damu ya Kristo/Mwana-Kondoo ni upuzi kwa wamataifa wanaopotea (1 Wakorintho 1 :18).Kumbe yeyote asiyeokoka,anaweza akatumia damu ya Kristo lakini kukakosekana matokeo sahihi yaliyokusudiwa! Ni vyema mtu aliye mbali na Mungu,arejee kwa toba,amwamini Kristo/aokoke kisha apate uhalali wa kutumia damu ya Mwana-Kondoo.

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900

Whatsapp +255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page