top of page

PASAKA SIKUKUU YA MUHIMU KWAKO.

Na Mch Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Neno “sikukuu ya Bwana” leo hii imetafsiriwa vibaya na watu wasiomjua Mungu na kupelekea Pasaka kuwa maficho ya uzinzi na uasherati,maana dhambi za kila aina sasa zinapangwa kufanyika kwenye sikukuu ya Bwana,kinyume kabisa na na maana ya kiroho. Hivyo ni vyema leo nikufundishe mambo haya kiundani,kusudi unapoadhimisha pasaka uwe na ufahamu wa Kiungu. Hivyo huna budi kujifunza;

  1. Nini maana ya neno sikukuu za BWANA?

  2. Pasaka na maana yake 

  3. Kwa nini Pasaka?

01.Nini maana ya sikukuu?

Sikukuu za Bwana ni makusanyiko matakatifu ya watu wenye kunia mamoja katika Kristo Yesu wakiwa na moyo wa changamko ( Walawi 23:4)

Katika tafsiri hiyo,unajifunza kumbe sikukuu yoyote ya Bwana ni moja ya makusanyiko matakatifu yenye lengo la kumuinua Bwana kwa wa changamko. Hii ni sawa na kusema,“kusanyiko lingine nje ya kusanyiko takatifu” si sikusanyiko la Bwana na sio sikukuu ya Bwana. Ili tuweze kuelewa nini hasa maana ya sikukuu ya Bwana,Bwana Mungu ametuelezea mapema kwamba sikukuu yake ni ipi na sikukuu nyingine ni zipi!.

Suala sio kukutanika,bali suala ni kitu gani kinachofanyika katika kukutanika kwenu. Hicho kinachofanywa kwenye kutaniko ndicho kinaaeleza ni kusanyiko la namna gani! Kumbuka jambo hili,agano la kale ni kivuli cha agano jipya ( Waebrania 10:1a);hivyo basi katika agano jipya tafsiri ya sikukuu ya Bwana imepanuka na tunaadhimisha tofauti kidogo na hapo mwanzo kwa maana hapo mwanzo ( agano la kale) walikuwa wakiadhimisha siku bali sasa tunaadhimisha kwa mioyo yetu tukitafakari juu ya Mungu anataka tufanye vipi kwenye sikukuu kwa msaada wa Roho mtakatifu.

Sheria iliwataka Wayahudi wote wawe na sikukuu kwa Bwana kama moja ya kuleta kusanyiko takatifu mbele za Bwana huku wakileta sadaka zilizoamriwa. Kama moja ya desturi iliyopitishwa kizazi hata kizazi,na hata sasa. Makusanyiko ya namna hiyo yalikuwa yakiitwa “ sikukuu za BWANA”. Sikukuu hizi ni zile tu zilizoamriwa na Mungu mwenyewe. 

  1. Mfano wa sikukuu za BWANA katika agano la kale ni kama vile;

  2. Pasaka ( Passover) -Kutoka 12:1-14,Walawi 23:5 n.k

  3. Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu ( Unleavened bread) – Kutoka 12:15-20,13:3,Walawi 23:6 n.k

  4. Malimbuko ( First fruits) – Walawi 23:9-14

  5. Mavuno ( weeks,Pentekoste,harvest) – Kutoka 23:16a,34:22a,Walawi 23:15-21 n.k

  6. Sikukuu za kuzipiga baragumu Au sikukuu ya Baragumu ( Trumpets) – Kutoka 23:23-25

  7. Sikukuu ya upatanisho ( Day of atonement) – Walawi 16:23-32,Hesabu 29:7-11

  8. Sikukuu ya vibanda ( Tebernacles-booth,ingathering) -Hesabu 29:12-34,Walawi 23:23-36a Yohana 7:2

  9. Sikukuu ya kusanyiko takatifu ( Sacred assembly) – Walawi 23:36b,Hesabu 29:35-38.

  10. Sikukuu ya mapumziko ( Sabbath year) Walawi 25:8-55 n.k

  11. N.k

02. Pasaka na maana yake.

Neno “ Pasaka” ni neno la kiswahili, limetolewa kutoka neno “Passover” lenye maana ya“pita juu ya”. Bwana Mungu alipita juu ya nyumba za Waisraeli zilizopakwa damu ya mwana-kondoo,kisha nyumba za wamisri zilizokuwa hazina damu ya mwana-kondoo ziliangamizwa. Huu ulikuwa ni “ukombozi“kwa Waisraeli kutoka utumwani Misri. Hivyo aliyechinjwa alikuwa ni“Pasaka” hivyo,kwa tafsiri ya kwanza ya neno Pasaka ni jina la mwana-kondoo aliyechinjwa  kwa ajili ya kuleta ukombozi (Kutoka 12: 6:11)

Hivyo; Pasaka ni sikukuu kwa Bwana kwa ajili ya ukumbusho wa ukombozi juu ya watu wa Mungu kutolewa utumwani Misri chini ya ulinzi wa damu ya mwana-kondoo. ( Kutoka 12:14). Ingawa aliyetolewa na kuchinjwa jioni alikuwa mwana-kondoo ambaye ndie Pasaka,lakini Bwana akaamuru iwe ni sikukuu kwa amri ya milele. Leo hii tunafahamu fika kwamba Yesu ndie mwana-kondoo wa Mungu. Yeye Yesu alisurubiwa hata mauti,damu yake ikatoka maana ndie (mwana-kondoo wetu).

Kwa kuwa agano la kale ni kivuli cha agano jipya, hivyo kama vile walivyookolewa Waisraeli walikaa ndani ya nyumba iliyopakwa damu ya mwana-kondoo nao wakaokolewa ndivyo ilivyo katika agano jipya ambalo ndio picha kamili kwamba,sote tuliopakwa damu yake Yesu tumekombolewa. Yesu alitukomboa pale msalabani,damu yake ikafanya kazi nyingi kwetu,lakini mojawapo ni ulinzi dhidi ya kuaangamizwa na mapigo ya muaribu.Sikukuu hii ni muhimu sana kwako,maana wewe nawe umekombolewa kutoka utumwani dhambini,kwenye hukumu kubwa! 

kumbuka; tangu Pasaka ya kwanza kipindi cha Musa mpaka Yesu alipokuja ulimwenguni ilikuwa kama miaka 1,400 hii ni sawa na kusema ilipita karne 14. Hivyo utagundua Pasaka ni moja ya sikukuu ya zamani na ni kubwa kuliko sikukuu nyingine;ambayo inapaswa kufanyika kwa amri ya milele.Leo katika agano jipya hatukumbuki tu kifo na kufufuka kwa Bwana kwenye kipindi cha Pasaka bali tunaangalia ukombozi wetu uliofanyika pale msalabani golgota. Na ikiwa ndivyo basi ni dhahiri kabisa maana ya Pasaka itakuwa imebadilika katika namna ya kuadhimisha kiroho,kwani kwa sasa unapaswa si kukumbuka ukombozi tu bali kutafakari juu ya mahusiano yako na Mungu na kujiuliza hivi Pasaka inakusaidia nini ikiwa upo nje ya Pasaka?

Yaani ni sawa na kusema mmisri anayesherekea kuona nyumba za Waisraeli zilizopakwa damu ya mwana-kondoo kwenye miimo ya milango yao hali akijua kunapigo linalomjia kwa sababu yeye yupo nje ya damu hiyo!!!Hivi unaelewa lakini!, ukweli ni kwamba sherehe ya mtu wa namna hiyo haina maana sababu yupo nje ya damu hiyo. Hivyo ndivyo tunavyopaswa kutafakari juu ya uhusiano wako na Mungu ukoje unapoiangalia Pasaka.

Kwa wapagani Pasaka Ina maana gani?

Leo asilimia kubwa wanaosherekea Pasaka ni wale wanaosherekea kimwili kwa starehe za kila namna. Maoteli na vyumba vya wageni vinajaaga,kumbi za starehe alikadhalika zinajaa,ufukweni nako kunajaa kwa anasa za kila aina! Lakini ukijiuliza,hivi ndivyo atakavyo Bwana katika Pasaka? Je ndivyo maana ya Pasaka! Hao ndio wapagani watu wasiomjua Mungu anataka nini hasa kipindi cha Pasaka. Pasaka haiko hivyo hata mara moja!!! Hivyo kwa wapagani Pasaka haina maana ya kiroho kama sikukuu ya Bwana,bali Pasaka kwao ni sikukuu ya kutenda dhambi na uasi. Wewe Je unafanya nini Pasaka

Wakati mwingine huwa ninalia nionapo watu walioiacha njia ya Bwana. Laiti watu wangelijua ni mateso ya namna gani aliyoyapata Bwana,wangelijua ni gharama kiasi gani aliyoilipa Yesu pale msalabani labda tungeelewa vizuri ni nini hasa ya Pasaka,tungeelewa ukombozi maana yake ni nini hasa! Natamani ungeelewa vile ninavyoelewa mimi haya mambo. Kumbuka; watu waliomkataa Yesu,wamekataa wokovu ujue ni.sawa tu na wapagani wasio na dini! Hivyo Pasaka kwao haina maana!

Lengo kubwa la Pasaka

01. Ukombozi kwa aaminiye.

Katika agano la kale, waliokolewa kwa njia ya imani ndani ya Yesu Kristo. Damu ya mwana-kondoo iliyopakwa ilikuwa ni kivuli cha damu ya Yesu katika agano jipya. Lakini haya yote yalifanyika chini ya imani kama msingi mkuu. Kwa maana chukulia ingekuwepo nyumba moja ya Muisraeli kipindi hicho,kisha akakataa kuamini juu ya ukombozi wake kwa Damu itakayopakwa kwenye kizingiti cha juu ya nyumba yake alafu chukulia akaikataa kabisa,Je unafikiri ataokoka dhidi ya pigo kwa sababu yeye kazaliwa Israeli.? Jibu hapana hawezi kuokoka,bali ataangamizwa!!! 

Ndivyo ilivyo kwa maana kule kuwa mkristo wa Jumapili kwa sababu baba na mama yako ni wakristo wa dhehebu fulani,hakutakuokoa wewe. Isipokuwa utaokoka endapo utaweka imani yako kwa Yesu Kristo kwa kumpokea / kuokoka na kuendelea kukakaa kwake,damu yake ambayo imekwisha mwagiga kwa ajili yako itakuokoa,ni hivyo tu. Unaweza ukaitumia damu ya Yesu hata sasa na ukaokolewa na mapigo yakujiayo,kwa imani tu.Pasaka sio sikukuu ya kusherehekea kichwa kichwa bila kutafakari ndani ya moyo wako

02. Kujifunza ulinzi upatikanao kwa damu ya mwana-kondoo wa Mungu.

Pasaka tunapoiadhimisha hatuadhimishi siku kama siku,bali vile Bwana anavyotulinda kila siku kwa njia ya damu ya mwana-kondoo wa Mungu,Yesu. Muaribu anapokwenda kupiga nyumba nyingine,asiipige nyumba yako iliyolindwa kwa damu ya Yesu. Imo nguvu ndani ya damu ya Yesu,na ndio inayotulinda sasa pale tunapoiita. Bwana Mungu angeliweza kuwavuka Waisraeli bila kuwaambia wachukue damu ya mwana-kondoo,unafikiri asingeweza kufanya hivyo kwa uweza wake? Jibu jepesi angeweza kufanya yoyote ayatakayo,lakini ametumia damu ya mwana-kondoo akitufundisha kwamba kuna nguvu ndani ya damu ya Yesu. Nguvu hiyo ya ulinzi dhidi ya nguvu za giza ipo mpaka sasa.

03. Kwa nini Pasaka?

Kwa sababu ni sikukuu iliyoamriwa kufanyika katika vizazi vyote kwa amri ya milele ( Kutoka 12:14). Amri hii ilikuwa kwa Waisraeli wote,lakini leo pale tu unapookoka,umejiungamanisha na Kristo Yesu,na umekuwa ni mzao mpya,taifa takatifu,na hapo hapana tena myunani wala myahudi,sote tu kitu kimoja. Na ikiwa ndivyo hivyo,basi amri hiyo ya kukumbuka ukombozi uliofanywa na Yesu ambaye ndiye Pasaka wetu ni amri ya milele.

Leo hii imepita miaka zaidi ya 2000 tangu Pasaka wetu kufa na kufufuka pale msalabani. Lakini habari njema ni kwamba Yesu yu hai kati ya waliokufa. Damu yake ipo hata sasa kutenda mambo ya ajabu kwa sababu imo nguvu ndani ya damu yake. Leo hii ebu chukua hatua moja zaidi ya imani ndani ya Yesu,na kisha nipigie tuombe pamoja,yamkini Bwana amekupitisha makusudi mahali hapa ili kwa pamoja tuombe naye Bwana Mungu aliye hai akatende. Namba zangu ni;

Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page