NYUMBA YANGU ITAMTUMIKIA BWANA( Yoshua 24:15)
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 15, 2016
- 3 min read

Na Mch.G.Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Imeandikwa ;“ Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.” Yoshua 24:15
Yoshua anajaribu kutufundisha leo kwamba waweza kuamua ni yupi utakaye mtumikia katika maisha yako awe Mungu kwako. Maamuzi yamewekwa mikononi mwako kumtumikia Mungu ambaye ndiye BWANA au kumtumikia mungu ambaye ni mungu baali. Yoshua anasema “kama mkiona vibaya kumtumikia BWANA…” kumbe yeyote anayetumikia miungu amechagua fungu baya kwa maana ameona vibaya,tena akamuacha Bwana Mungu.
Kati ya jambo baya sana ambalo ni machukizo kwa Mungu wetu ni “ kuitumikia miungu ” yaani kuzini kiroho,pale ambapo unamuacha Bwana Mungu wako na kuigeukia miungu ya kwenu ambayo yamkini babako waliitumikia hapo zamani.
Katika biblia,pale ambapo Mungu aliwaacha watu wake wapigwe na maadui zao na wawe chukizo ni pale tu walipomuacha Mungu na kuigeukia miungu na kuitumikia.Yeye Bwana ni Mungu mwenye wivu asiyependa michanganyo ( Kumb.4:24)
Utumishi mwema unaanzia nyumbani na wala sio kanisani,na wala sio katika makusanyiko ya wapendwa. Bwana Mungu anataka nini kwako siku ya leo? Je si wewe na nyumba yako mumtumikie Yeye Mungu pekee? Je Yeye si mwema kwako na familia yako? Na sasa ndio wakati wa kuijenga madhabahu ya Bwana nyumbani kwako. Hakuna jambo jema machoni pa Bwana kama kuona ndugu wakikaa pamoja kwa umoja katika kusanyiko takatifu.
Ikiwa utawakusanya watu wa nyumbani kwako pamoja nawe,kwa kwa ajili ya ibada kila siku,basi ujue hapo hakutakuwa na mlango utakaomruhusu shetani aipige familia yako. Tazama shida iliyopo leo, kwamba hatuna ibada za nyumbani. Wakristo wengi wa leo hufanya ibada wawapo tu kanisani,na wakirudi nyumbani uenda kulala,kwa maana wamepafanya nyumbani ni sehemu ya kulala lakini kanisani wamefanya ni sehemu ya ibada. Hii ni mbaya,kwa maana ibada ya kwanza ya mwamini inatakiwa ianzie nyumbani kwake yeye na familia yake kisha,ndiposa ibada ya kanisa ifuate.
Jaribu leo,kutengeneza madhabahu ya neno la Mungu na maombi nyumbani kwako. Haijalishi wewe ni mwana ndoa au la! Bali ikiwa ni mwana ndoa jaribu kutengeneza madhabahu ya kumfanyia Bwana ibada wewe na mwenzi wako pamoja na watoto na wote wakaao hapo nyumbani kwako. Au ikiwa wewe bado hujaolewa au kuoa basi jaribu kutengeneza madhabahu ya Bwana vivyo hivyo. Kisha utaona jinsi Mungu atakavyosimama na wewe uingiapo na pale utokapo.
Jambo hili ni jambo la msingi sana kwako,kwa maana yakupasa umtumikie Bwana Mungu wewe na familia yako pamoja. Wala haipendezi kumtumikia Mungu peke yako bila familia,au bila mwenzi wako. Uwapo nyumbani,kusanya walio hapo na uanze kuomba nao kisha utamuona Bwana akitenda makuu katika familia yako.
Ziko nyumba za wapendwa ambazo kwa sasa zimegeuka kuwa ni nyumba za dawa kama vile duka la dawa kwa sababu ya magonjwa ya mara kwa mara yawapatao. Na huu sio mpango wa Mungu kuishi katika magonjwa ndani ya familia yako,bali mpango wa Mungu ni kuwa na afya njema kama roho yako ifanikiwavyo ( 3 Yoh.1:1).
Dawa ya kufanikiwa kuishi katika afya wewe na familia yako ni kuanza kumfanyia Bwana ibada uwapo nyumbani kwako wewe na familia yote. Kisha utaona vile Bwana atakavyotenda kwa kuwapigania afya zenu na gafla utashangaa nyumba yako haitakuwa nyumba ya madawa bali nyumba ya watu wenye afya za rohoni hata za miili.
Kumbuka,kuwa mkristo ina maana uwe nuru mahali unapokaa. Hivyo ifanye nuru iangaze nyumbani mwako kwa kuwa na ibada kwanza kila siku. Unaporudi nyumbani kusanya walio wako ingieani katika maombi. Uwapo nyumbani endeleza ibada ya neno na maombi na utaona ukifanikiwa katika mambo yako uyafanyayo.
Kwa msaada zaidi waweza kunipigia moja kwa moja kwa namba zifuatazo; +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.G. Madumla
UBARIKIWE.
Comments