top of page

NUHU AINGIA NDANI YA SAFINA NA FAMILIA YAKE.

Na Mch Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi…

Nuhu alikuwa mwanadamu kama sisi lakini alikuwa mtu wa haki,mkamilifu tena aliyepata neema machoni pa Bwana. Katikati ya watu waovu,Nuhu alikuwa na mahusiano mema na Mungu wake. Vipi wewe hapo ofisini mwako katika waovu waliokuzunguka wewe U mwema? Vipi hapo unapoishi katika waovu,wewe ni mwema? Vipi hapo unaposoma katika waovu wengi,Je wewe U mwema? Kigezo cha kuzungukwa na waovu hakikunyimi nafasi ya wewe kuwa mwema yaani kuwa na mahusiano mema na Mungu wako.

Nuhu alizungukwa na watu waliojikinai yaani watu waovu wa kupindukia lakini katikati yao Nuhu aliendelea kukaza na Bwana. Kumbe inawezekana kabisa ukawa umezungukwa na wa mataifa lakini wewe ukawa ni mwema machoni pa Bwana. Hivyo Nuhu hakuwa ni malaika hivi,bali alikuwa mwanadamu kama wewe lakini alikuwa wa haki.  

Jambo moja kubwa la kujifunza kwa Nuhu ni kwamba alikuwa mwenye “utii na imani thabiti” (mfano wa mtu mwenye karama ya imani) naye Nuhu akaunda safina ili aiokoe familia yake baada ya kuonywa na Mungu ( Waebrania 11:7). Ingawa wengine hawakuona thamani ya kile alichokifanya bali yeye aliendelea mbele kuunda safina kwa mambo yasiyoonekana bado. Biblia inasema; watu nane tu kati ya wengi waliopona au waliokoka na gharika,Nuhu na mkewe,wanawe watatu na wake za wanawe ( 1 Petro 3:20-21)

“ Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe.” Mwanzo 6:18

Safina kilikuwa ni chombo kilichowakomboa watu nane waliokubali kuingia ndani ya chombo hicho. Hii ni sawa na kusema laiti kama wasingeliweza kuingia ndani ya safina basi ni wasingeliokoka na kifo. Leo hii katika agano jipya safina ni Yesu kila aingiae ndani ya Yesu U na uzima,uokoka. Kumbuka, “ agano la kale ni kivuli cha agano jipya ” Waebrania 10:1′- Na mambo hayo ya kale yameandikwa ili kutufundisha kwamba kila atakayempokea Yesu U na uzima wa milele ( Yoh.3:16)

Hivyo,Nuhu aliingia ndani ya safina yeye na familia yake. Yaani ni sawa na kusema aliingia kwenye chombo cha wokovu yeye pamoja na familia yake. Kumbe raha ya kuokoka haipo kwako tu bali na familia yako. Biblia imeandika kuhusu Nuhu kuingia ndani ya safina pamoja na familia yake ikitufundisha kwamba unapaswa kuokoka na kuwashika mikono watu wa nyumbani mwako nao waokoke. Mpango wa Mungu ni kila mmoja aokoke ( 1 Timotheo 2:3-4). Lakini kama katika siku za Nuhu,watu wengine walikataa safina nao wakaangamia wote,ndivyo wanavyoangamia leo wanaokataa wokovu katika Kristo Yesu.

Najifunza kwa Nuhu mtu ambaye hakuwaacha watu wa nyumbani mwake waangamie ingawa hawakuwa wenye haki,bali alifanya kama alivyoamriwa na Mungu akawaingiza kwenye safina. Hata sasa Bwana amekuagiza kuwafanya watu wako waingie kwa Yesu,lakini kitu kibaya wewe hufanyi hivyo,ebu jiulize; 

Je mbona uendapo kanisani,unaenda peke yako na kuwaacha wengine hapo nyumbani? Mbona baba na mama yako hawajaokoka na wewe huna habari nao? Tena mbona umewaacha ndugu zako hauwahubirii neno wageuke? Mbona watoto wako mpaka sasa hawamjui Mungu nawe umewaacha tu? Mbona huoneshi jitihada yoyote ya kupeleka wokovu kwa watu wa nyumbani mwako? Je unafikiri Mungu anapendezwa na tabia hizo?

Jifunze kwa Nuhu,Jifunze kwa Musa pia mtu aliyeulizwa na Farao kwamba mtatoka na nani huku Misri?Musa akamwambia tutatoka na watu wetu,vijana wetu ng’ombe wetu. Wewe huna budi sasa kuwa nuru kwa watu wa nyumbani mwako ili waokoke kama wewe. Ifike wakati unapokuwa kanisani uwe na mwenzi wako,usikubali kumuacha mume au mke wako nyumbani alafu wewe upo ibadani. Hapana,bali sasa alipo mumeo wewe uwepo,na alipo mkeo na wewe uwepo.

Kwa msaada zaidi na maombezi piga sasa kwa

+255 683 877 900

Namba ya what’s app ni +255 746 446 446

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page