NGUVU YA UELEWA KATIKA NENO.
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 8, 2017
- 4 min read

Na Mch.Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Katika mambo ya msingi kwa kila mwamini ni juu ya suala zima la uelewa. Faida ya neno la Mungu maishani mwako ipo katika kulielewa neno kisha ndipo ulishike na kuliishi kama atakavyo Mungu. Bila uelewa mzuri huwezi kufaidika na neno hata wokovu hauna maana ikiwa kama umekosa uelewa mzuri wa neno.
Kuna nguvu ya namna yake ya kuelewa neno la Mungu wakati unalisoma au kulisikia. Na kwa nguvu hii ndio inatujenga imara wokovu wetu. Wokovu ni kila kitu kuhusu uelewa mzuri wa neno la Mungu. Si watu wengi wanaelewa na lile neno wanalohubiriwa au kusoma. Ndani ya kila neno kuna sauti ya Mungu inayosema na wewe sasa “ Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu,…” 2 Timotheo 3:16a. Kazi kubwa si kusikia au kusoma bali kazi kubwa ni kuisikia sauti ya Mungu katika neno,kwamba Mungu anataka nini kwako sasa.
Ikiwa utafanikiwa kuisikia sauti ya Mungu katika neno ulisomalo,basi ni dhahili kwamba hakuna nguvu ya uadui wowote ule utakaofanikiwa kwako. Kwa sababu ushindi wetu upo katika kusikia sauti ya Mungu katika neno lake. Hakuna yeyote aliyesikia vizuri akaelewa na hilo neno kisha akafeli katika vita vya kiroho. Nguvu ya uelewa katika neno ni mojawapo ya silaha ya kwanza na kubwa kuliko silaha yoyote ile katika Kristo Yesu,kwa sababu kila silaha hutegemea uelewa wako juu ya neno la Mungu.
Ni mpango wa shetani kuwafunga watu kuhusu uelewa katika neno na kuwasukumia mbali hata kushindwa kujua wamepewa nini katika neno. Na ndio maana unaona leo vita ilivyogeuka badala ya wakristo kupambana na roho ya shetani,wakristo hupambana wao kwa wao. Kila mmoja akijiona yeye ni bora kuliko mwenzake. Ukiona hivyo basi ugundue kwamba hilo ni mojawapo la tokeo baya la kufungwa kuelewa wa neno la Mungu kwa usahihi zaidi.
Mtu huwa ni mjinga asipoelewa jambo
Siku moja kulikuwa na safari ya nje ya nchi. Hivyo watu wote wakawa wamekwisha ingia kwenye ndege tayari kwa safari kuelekea nje ya nchi (ulaya). Wakiwa kwenye ndege,mtu mmoja aliyekuwa ana njaa na gafla muhudumu wa ndege akawa anagawa chakula kwa abiria naye alikuwa akitamani kuchukua chakula lakini alijiuliza“endapo nitachukua chakula hiki,nikidaiwa pesa je!! Itakuweje? Maana hapa mfukoni sina pesa…” hivyo wengine wakachukua ila yeye alikataa kata kata!
Maskini!!! Hakujua kwamba tiketi yake ya ndege imejumlishwa na chakula humo humo. Kwa hiyo mtu huyo mpaka anashuka hajala kitu kwa kuwa hakuelewa kwamba ukikata tiketi ya ndege unastahili kupewa na chakula kitolewacho kama sehemu ya malipo aliyoyafanya. Alikosa vyote,kwa kigezo tu cha uelewa. Ndivyo ilivyo hata sasa. Yapo mambo ambayo unastahili kupata lakini yamefichwa katika neno. Watakayoyapata ni wale tu wenye kuelewa na lile neno.
Ikiwa neno la Mungu limekuambia usipite kushoto nawe ukasikia lakini hukuelewa hilo agizo,basi ni hakika utapita kushoto bila kujua,na ndio makosa yenyewe.!!Sasa suala sio kusikia,bali suala ni kuelewa. Hivyo ni mpango wa Mungu kwa kila aliyeokolewa awe na ufahamu mzuri na ulio sahihi katika Neno. Biblia inasema;
“ Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.” 1Timotheo 2:3-4
Chunguza kwa makini neno la Mungu lilo hapo juu. Utagundua kwamba Mungu anataka kila mtu aokoke bila kujali itikadi ya dini,kabili rangi yake. Wokovu ni kwa kila mtu atakaye mkiri Kristo Yesu kuwa Bwana na mwokozi wake kama hatua ya kwanza anayoipenda Mungu. Na baada ya hapo neno linasema,baada ya kuokolewa “watu hao waijue kweli” kweli ni neno la Mungu ( Yoh.17:17).
Kumbe ni mapenzi ya Mungu tuijue kweli na tusiwe wafungwa wa dhambi. Ukiijua kweli,hiyo kweli itakuweka huru. Kwa kuwa hiyo kweli ipo ndani ya neno,basi shetani hapendi uijue kusudi usiwe huru. Ndio maana nabii Isaya alitabiri kwamba kuna watu wamefungwa ufahamu wasielewe kusudi wasije wakaokoka ( Mathayo 13:14).
Mojawapo ya silaha kubwa anayoitumia shetani ni kukufunga ufahamu ili usielewe neno la Mungu usije ukaokoka akakukosa. Hii ni kweli kabisa, unaweza kuona jinsi gani watu walivyofungwa ufahamu leo hii. Angalia jinsi watu wanavyolala kipindi cha neno kanisani,angalia jinsi ambavyo watu wanalala pale tu wanapoanza kusoma neno,angalia jinsi ambapo hata wewe mwenyewe unavyopata uchovu wakati wa neno,hata unapiga miyayo au kuhairisha kusoma!!! Hujue hayo yote si mpango wa Mungu bali ni mpango wa shetani
Uelewa una nguvu sana katika imani hii. Ukiwa na nguvu ya namna hii,utajua ni nini cha kufanya na nini cha kutokufanya kwa wakati ulio sahihi na kwa watu walio sahihi. Labda tujifunze tena neno hili kwa kumtazama Yesu vile asemavyo. Bwana Yesu alipotoa ule mfano wa mpanzi,akaeleza aina za mbegu nne. Ya kwanza ilianguka njiani na ndege waja waila ( Soma Mathayo 13:1-9). Yesu anaeleza mfano wa mpanzi;
“ Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi.Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.” Mathayo 13:18-19
Angalia hapo;kwamba ukisikia neno la ufalme lakini usielewe nalo,hapo huja adui na kulinyakua moyoni mwako lilipopandwa. Kumbe hata kanisani mwako,unaposikia neno la ufalme linahubiriwa au kufundishwa,ikiwa hujaelewa nalo basi halitakuwa na matokeo yoyote kwa maana limekwisha nyakuliwa moyoni mwako. Hivyo basi,utagundua kuna kazi muhimu inayohitajika kufanyika kwako ili uweze kupokea nguvu ya uelewa katika neno.
Matunda ya nguvu ya uelewa katika Neno;
Kupata mafunuo halisi vile Mungu atakavyo
Kupata mafundisho,maonyo,maongozi mbali mbali,kupata hukumu juu ya dhambi uliyoifanya.
Kuwa na ujasiri wa ushuhudiaji kwa watu wote bila kujali itikadi za dini,au bila kujali cheo cha mtu.
Kujua mema na mabaya. Hapa,utakapojua mema na mabaya utaongozwa na kusaidiwa na Roho mtakatifu kuyafuata yale yote mema.
Ni nini cha kufanya sasa ili niipate nguvu hiyo ya uelewa?
01.Msirikishe mtumishi wa Mungu aliyekaribu nawe mwenye kuyajua hata,ili aweze kukuombea na kukushauri panapofaa. Maombezi ya mchungaji ni muhimu sana ili yavunje kongwa linalokufanya ushibdwe kuelewa neno.
02.Kujibidiisha katika maombi yafuatayo.
Kataa kika roho inayoleta uchovu kipindi cha neno
Vunja kila nguvu ya kipepo inayoleta uzito kipindi cha neno
Yatiishe mawazo yako yamtij Kristo( hivyo vunja ngome ya mawazo mtawanyiko kipindi cha neno)
Panda ufahamu moya wa neno la Mungu.
Kwa msaada zaidi katika eneo hili,waweza kunipigia pamoja na maombezi,piga sasa kwa namna +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments