NGUVU YA SHUKRANI.
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 29, 2015
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi;
Kawaida “kushukuru” ni aina ya maombi mazuri na yenye upako/nguvu. Kwa maana yeyote anayemshukuru Mungu huonesha mambo yafuatayo;
Kulidhika – Ukimshukuru Mungu katika jambo lolote,huonesha umeridhika na ulichokipata/ulichotendewa.
Kuona wema wa Mungu – Maombi ya shukrani hueleza wema wa Mungu maishani mwako. Fikiria yale uliyoyaomba,fikiria na uliyoyapata kisha linganisha,utagundua kuwa Bwana ametenda zaidi ya yale uliyoyaomba. Huo ni wema wa Bwana kwako.
Kuna namna fulan/nguvu inayopatikana katika kushukuru,ikiwa mwenye kushukuru akishukuru kutoka rohoni bila kuigiza. Hivi unafahamu shukrani ni kama mafuta ya manukato mbele za Mungu? Ndio, ni kama mafuta. Na ndio maana ukiwa mwepesi wa kushukuru katika kila unachotendewa basi uwe na uhakika wa kupokea mengine mara dufu zaidi ya hayo uliyoyapokea. Huu ni utaratibu ambao si wengi wanafahamu. Lakini ebu tujifunze kwa Yesu;
” Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. ” Mathayo 15:33-36
Wanafunzi walikuwa na uhitaji wa chakula na kusema ukweli hakukuwa na chakula isipokuwa mikate saba na visamaki vichache. Ukilinganisha na idadi ya watu,mikate na samaki hao walikuwa hawafui dafu/hawatoshelezi kabisa. Lakini wanafunzi walimwendea Yesu,na kumwomba. Hii ndio njia ya kwanza na ya pekee,pale unapokuwa na kupungukiwa,basi sharti umwendee Yesu,na umwombe. Sasa somo halipo hasa kwa wanafunzi bali lipo kwa Yesu kile alichofanya; Biblia inasema Yesu aliomba kwa Baba,maombi yake yalitofautiana na maombi yako pale unapoomba ukihitaji kitu,kwa maana Yeye alishukuru tu. Swali? Kwa nini Yesu alimshukuru Mungu kwa mikate na visamaki hali akijua hitaji la wanafunzi ni kupata chakula zaidi kwa ajili ya kulisha mkutano mkubwa.
Yesu anatufundisha;Uwe mtu wa kushukuru kwanza kwa kile kidogo ulichonacho kabla ya kuhitaji kikubwa. Lakini ukijiuliza;ni mara ngapi umekuwa ukiomba mambo makubwa hali yale madogo uliyopewa umesahau kumshukuru Mungu? Kwani ni nani aliyekupa hayo madogo uliyonayo? Je si Mungu? Na si Yeye awezaye kukujazi na mengine? Hivyo somo kubwa ni kumshukuru Mungu kwanza kwa kile ulichonacho.
Pili Yesu aliposhukuru kitu gani kilitokea?“…akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano…” Mikate na samaki iliongezeka kisai cha kushangaza! Hii ni ajabu sana!!!!! Kumbe,Mungu aweza kuzidisha kile ulichokuwa nacho ukiwa kama utakuwa mtu wa kushukuru. Kushukuru kuna nguvu ya “kusababisha kuzidishiwa” kwa mtu mwenye kukaza kumwambia “asante Bwana kwa yote uliyonipa” Hujachelewa,anza leo kumwomba Roho mtakatifu akuwezeshe kukupa moyo wa shukrani.
Kushukuru huendana na sadaka.
Ikiwa umekusudia kumshukuru Mungu,basi jitahidi kuandaa na sadaka yako ya shukrani,ingawa si lazima lakini ni jambo jema sana kutumia mombi yako ya shukrani kwa kuyasindikiza na sadaka. Iwapo ni kwenye ibada,mshukuru Bwana Mungu wako kwa matoleo ya sadaka,inanoga sana kwa maana ni jambo la kibiblia.” Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. ” Mwanzo :8:20
Ukisoma kwa umakini kuhusu sadaka ya shukrani aliyoitoa Nuhu kwa Mungu,utagundua Mungu alihairisha kupiga mwanadamu kwa gharika,pale aliposikia harufu ya kumridhisha,hatimaye Bwana alighahili kuilaani nchi. Lakini haya yote Bwana alifanya baada ya kupokea sadaka nzuri ya shukrani kutoka kwa Nuhu. Ikiwa Nuhu alifanikiwa kumtolea Bwana sadaka nzuli ya namna hiyo,wewe pia unaweza kumtolea Bwana sadaka yako ya kushukuru,na hatimaye mambo fulani mabaya yakazuiliwa kwako kwa sadaka yako tu ya shukrani.
Yesu amfufua Lazaro,maombi ya shukrani yahusika.
” Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. “ Yoh.11:41-42
Sadaka yako ya shukrani inauwezo wa kufufua mambo yaliyokufa hata leo. Ebu fikiria kama utamtolea Bwana sadaka ya shukrani,ukimshukuru Mungu kwa biashara yako ambayo kwa kweli ni kama vile haipo au imekufa lakini ukajikaza kwa imani ukamwambia Bwana asante kwa biashara hii,pamoja na sadaka yako nzuri,Je Bwana hataifufua hiyo biashara yako iliyokuwa imekufa? Kwa imani,mimi nataka nikwambie kwamba Bwana atashughurika nayo tu,hata kama haitafufuka leo,lakini kesho itakuwa hai kwa imani. Anza leo,na utaona vile Mungu atakavyokushangaza.
Ikiwa kama umejifunza kitu, nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
What’sapp namba .+255 746 446 446
Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments