NGUVU YA SADAKA ~ 05
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 14, 2017
- 4 min read

Mch.G.Madumla.
Kwa ufupi;
Bwana Yesu asifiwe…
v) Sadaka ya nadhiri
1 Samweli 1:11 “Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.”
Katika andiko hili, tunamuona Hana mkewe Elkana Mwefraimu, ambaye Bwana alikuwa amemfunga tumbo asizae. Hana akiwa kwenye maombi faragha na Mungu wake ndipo akaweka nadhiri ya kumtolea Mungu mtoto kwa kazi ya utumishi wa maisha yote ya mtoto wake. Haikuwa rahisi hivyo kama unavyofikiria sasa, lakini kwa kuwa Mungu ni mwaminifu mno alimjibu Hana. Biblia inasema Hana akaweka nadhiri “akasema…” Neno hili “akasema” ni neno la ahadi yake Hana kwa Mungu, hivyo basi kupitia andiko hilo,tunaweza kujua maana kamili ya neno nadhiri
Nadhiri ni ahadi iwekwayo mbele za Mungu kwa sababu ya uhitaji wa kitu fulani. Ni aina ya sadaka itolewayo kwa njia kunia kwa maneno/matamko mbele za Mungu.
Kwa mfano ; Hana aliyekuwa tasa aliweka ahadi/nadhiri mbele za Mungu kwamba akipata mtoto mume atamtoa na kumpa Bwana siku zote za maisha yake huyo mtoto. Hii ndio sadaka ya nadhiri. Na kweli Hana akapata mtoto na kuitimiza nadhiri yake. Laiti Hana kama asingelimtoa mtoto wake na kumpa Bwana kama alivyoahidi basi hiyo isingelikuwa nadhiri iliyokamilika.
Leo, unaweza ukaweka nadhiri na kusema kwamba kama Bwana atakupa kazi fulani basi utamtolea pesa ya mishahara miwili yote. Na endapo Bwana amekufanikisha basi ujue mishahara miwili ya mwanzo wa kazi yako yote si ya kwako tena bali ni ya Bwana. Kwa lugha ya kibiashara nadhiri ni kama kuwekeana makubaliano/mkataba na Mungu juu ya jambo/kitu fulani ukifanikiwa kupata.
Na siku zote Mungu ni mwaminifu sana, ujue ikiwa kama umeweka mkataba huo na Mungu,basi utapata tu na ukipata tu ukumbuke kuitimiza nadhiri yako la sivyo hiyo nadhiri hugeuka na kuwa dhambi mbaya kuliko unavyofikiria, maana ni afadhali usingeiweka kuliko kuiweka na usitimize.
Sadaka ya nadhiri sio sadaka ya mchezo mchezo,ni sadaka makini sana. Wengi leo wapo chini ya laana kwa sababu wamechelewa au kushindwa kutimiza nadhiri zao walizomuwekea Mungu. Watu wa namna hii hawajalaaniwa na shetani wala mtu bali Mungu mwenyewe, sasa jiulize kwamba ikiwa Mungu ndiye aliyekulaani uende kwa nani mwenye uwezo wa kushindana na Mungu juu ya laana hiyo? Kama si Mungu mwenyewe kwa huruma zake?
Nami nimeona watu wengi wamefungwa kwa muda mrefu sana hali wakiomba na kuombewa lakini vifungo vipo pale pale,na sio kana kwamba maombi yao ni mabaya, wala! Maombi ni mazuri lakini walikosea sana katika sadaka ya nadhiri. Mfano ebu jiulize ni mara ngapi unahaidi pesa au mchango fulani mbele za Mungu tena katikati ya ibada alafu unachelewa kwa makusudi kuitoa hicho ulichoahidi?
Au unaahidi mchango fulani kisha unahama na kanisa hali ukijua hukumuadi mwanadamu bali Mungu. Je unafikiria kule uendako utakuwa salama?? Wewe jiulize tu hivyo!! Au jiulize kwamba unaweza kumkimbia Mungu? Sasa unaweza ukaona mambo yako mengi hayaendi na ukafikia ni shetani, kumbe njia zako hazikuwa nzuri mbele za Mungu. Kumbuka neno hili “ Mungu hadhihakiwi, chochote upandacho ndicho utakachovuna” Wagalatia 6:7
Unapomuwekea Bwana ahadi yoyote ile,na ukashindwa kuitimiza kwa makusudi,ujue unamdhihaki Mungu,naye hadhihakiwi bali utavuna laana tu. Jichunguze sasa,je hukuweka ahadi ya ujenzi hapo kanisani,vipi mbona hujaitimiza mpaka leo? Vipi mbona hata kanisa umehama? Je hukuweka ahadi ya changizo hapo kanisani kwako,na mbona mwaka sasa unaisha na hukutoa? Ni dhambi hiyo inayokukwamisha mambo yako!
Kuna watu ambao walimuwekea Bwana nadhiri ya kumtegemeza mchungaji wao kwa pesa na mali walizokuwa nazo, lakini wameacha na wengine hawajatoa kabisa! Hiyo ni dhambi maana ni afadhali sana usingeliweka.
Mambo muhimu kwako ya kuzingatia katika sadaka hii ya nadhiri.
01. Kabla ya kuweka nadhiri mshirikishe Roho mtakatifu juu ya nadhiri hiyo.
Hatua hii ndio hatua ya kwanza kabisa ya utoaji wa nadhiri. Roho mtakatifu ni Mungu,utakapo muomba ukihitaji msaada kamili kutoka kwake,naye atakupa. Atakuambia utoe au la! Kama kutoa nadhiri basi iwe nini itakayokuwa nyepesi kwako na yeye baraka sio laana. Hili ndilo tatizo la wengi maana watu wameweka nadhiri pasipo kumshirikisha Roho mtakatifu, na kujikuta wakipata uzito wa kuiondoa nadhiri hata baadae hugeuka kuwa dhambi badala ya baraka.
02. Mshirikishe mtu wako wa karibu (Mwana ndoa mwenzako,au yeyote mtu wako wa karibu “your spouce”)
Ni vyema mtu wako wa karibu akajua kile ambacho umeweka nadhiri ili awe msaada kwako wa kukukumbusha kwa maana usije ukasahau. Kwa maana ukisahau nadhiri hiyo hugeuka kuwa dhambi,na tanzi kwako hapo ni afadhali usingeliweka nadhiri.
03. Hakikisha unaandika yote juu ya nadhiri yako.
Nadhiri ni kama njozi isiyotimia bado lakini inatazamiwa kutimia siku za usoni. Hivyo ni muhimu sana kuandika ili kusudi ukisahau upate kusumo vizuri kila ulichoahidi mbele za Mungu ( Habakuki 2:2). Usipoandika kutakuwa na uwezekano mkubwa sana wa kusahau,na utashindwa kutoa ipasavyo. Mimi nawajua watu walioweka nadhiri bila kuandika alafu bahati mbaya wakasahau na nadhiri ikageuka dhambi kwao.
04. Ukiweka nadhiri usikawie kuitoa ( Kumb.23:21-23, Muhubiri 5:4)
Ujitahidi sana kuiondoa nadhiri yako kwa namna yoyote ile maana inawezekana. Mfano mzuri; umemuwekea nadhiri Bwana kwa kusema Ukipata kazi utamtolea Bwana laki 500,000/= kisha ukapata. Na katika nadhiri hiyo ukaiweka hadharani kwenye ibada. Sasa,baada ya kupata kazi ukagundua mshahara wako ni mdogo hauwezi ukatoa laki 5 yote maana kwanza hayafikii kiasi hicho labda unalipwa tshs 300,000/=.
Kwa kuwa Mungu ni mwaminifu sana,basi ujue atakupa hiyo laki 5 lakini anaweza kukupa kwa awamu awamu. Mwezi mmoja akakupa kidogo,Baade ukapata tena kidogo hatimaye kama utazijumlisha hizo ulizozipata zote utajikuta umefanikisha lengo lako la laki 5. Lakini cha ajabu watu wakipata nusu nusu wanakisahau na hatimaye wanakula hizo nusu nusu. Mwisho wa siku wanajikuta hawajatoa nadhiri zao!! Umeona hapo!
Kumbuka;Sadaka ya nadhiri haiwekwi kwa haraka haraka bila msukumo wa ndani wa Roho mtakatifu. Na ikiwa uliweka na hujaitimiza mpaka sasa,basi unahitaji kwanza maombi ya toba kisha kuitimiza mapema haraka iwezekanavyo.
Kwa msaada zaidi waweza kunipigia simu au kunicheki kwenye whastaap yangu kwa mawasiliano yafuatayo;
ITAENDELEA….
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE..
Comments