top of page

KWA NINI MUNGU ALIIPOKEA SADAKA YA HABILI, NA KUIKATAA SADAKA YA KAINI?


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi sana.

“ Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.“ Mwanzo 4:4-5

Mtu mmoja akanichekesha akasema labda kwa sababu Mungu anapenda nyama, sio mboga mboga ndio maana aliipokea sadaka ya Habili . Hahahaaa😁😁😁!!! Amesahau Mungu si mwanadamu wala si mtu, Yeye ni Mungu na atabaki kuwa Mungu, hali nyama wala chochote. Ni muumbaji wa vyote katika vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana. Anyway!

Kumbuka ;simulizi hii ndio simulizi ya kwanza ya matoleo iliyorekodiwa kwenye biblia, ingawa bila shaka inaonesha matoleo hayakuanzia hapo. Kitabu chenyewe ni Mwanzo ikiwa na maana mwandishi anataka ujue mwanzo wa sadaka iliyotolewa kwamba ; moja ya sadaka ilikubaliwa na nyingine ilikataliwa. Na hapo ndipo tunajiuliza kwa nini sadaka moja ikubaliwe na nyingine ikataliwe na Mungu ?

Ingawa biblia haikuonesha wazi wazi utoaji wa sadaka uliofanywa na Adamu na Hawa, lakini kwa kuwa watoto wao walitoa basi bila shaka na wao walikuwa watoaji. ( kumbuka, Bwana Mungu aliwapa kama kielelezo cha utoaji sadaka wa wanyama pale alipochinja mnyama na damu ya mnyama ikatoka kisha Bwana Mungu akawavisha nguo ya ngozi ya huyo mnyama Mwanzo 3:21)

Hivyo; Ni Mungu ndiye aliyeamuru apewe sadaka na sio Adamu na Hawa waliamuru kumtolea sadaka Mungu. Suala la sadaka ni la Mungu mwenyewe akitutaka tumtolee, Yeye ndiye ameweka sadaka itolewe kwake, lakini inatolewaje? Hivyo ikiwa kama kulikuwa na sadaka zilizoendelea kutolewa na Adamu na Hawa, basi hakuna la kushangaa tunapoona Kaini na Habili wakimtolea Mungu sadaka.

Inaonesha kuwa, Kaini na Habili walikwisha fundishwa utaratibu mzima wa utoaji. Utaratibu wa utoaji ulilenga kwa wanyama ( kwamba mnyama atolewe sadaka, kumbuka huu ni Mwanzo kabla ya sheria) , kama fidia ya dhambi walizozifanya tunaweza kuliona hili pale tunapoangalia matoleo yaliyotolewa na ndugu hawa wawili haswa kwa kusoma Mwanzo 4:7, ambapo Kaini hakufanya utaratibu aliofundishwa. Tunamuona mmoja ya watoto wa Adamu, Habili akitii utaratibu wa matoleo.

Neno linatuambia Kaini alitoa mazao ya shamba kwa kuwa alikuwa mkulima wa ardhi na Habili akatoa wazaliwa wa kwanza wa wanyama wake. Sasa suala la utoaji sadaka halikutegemea wanamiliki nini? Ndio watoe. Yaani Haikumpasa Kaini kutoa mazao ya ardhi iliyokwisha kulaaniwa kwa kigezo cha yeye Kaini kuwa mkulima,!!! Bali alikuwa na nafasi ya kumtolea Bwana sadaka ya mnyama pia. Kwa sababu hata Adamu na Hawa waliendelea kumtolea Mungu ingawa hatuambiwi kwamba walikuwa ni wafugaji au wakulima, ila walitoa kama wanyama kama sehemu ya ibada.

Imeandikwa; “ Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; …. ” Waebrania 11:4. Na ukisoma chanzo cha imani ni kusikia Neno la Mungu ( Warumi 10:17). Hivyo, inaonesha dhahiri kabisa Kaini na Habili walisikia kabla ya kutoa sadaka zao mbele za Bwana. Kwa habari ya Habili alitoa “ kwa imani” sababu alisikia maelekezo sahihi ya kiungu katika eneo la utoaji bali inaonesha kwamba Kaini hakutoa kwa imani kwa sababu ya kutokutii kile alichokisikia kwenye eneo zima la utoaji sadaka. Angalia, Habili alipotoa kwa sababu ya imani na kutii alichoelekezwa aliona haitoshi kutoa kama kutoa bali “kutoa kilichonona” yaani kutoa kilicho bora zaidi ambacho moyo wake utahusika nacho.

Hivyo, Mungu alipomuona Kaini hakufanya vizuri, alimpa nafasi yamkini atarejea kwenye utaratibu na kanuni nzuri za utoaji, lakini hata hivyo Kaini hakuona sababu ya kurekebisha makosa yake mbele za Mungu. Mungu akamwuliza “ Kama ukitenda vyema hutapata kibali? … ” Mwanzo 4:7. Bwana Mungu alikwisha muona Kaini nje ya mstari na anajaribu kumrudisha lakini hata hivyo Kaini hakuwa tayari maana sasa ana uchungu, hasira na roho ya mauaji inamnyemelea.!!! Hivyo ni hali ya kutotii na uasi wa Kaini kulimfanya kumtolea Mungu vitu vinyonge vya viwango vya chini kabisa, tena kutoa nje ya utaratibu uliowekwa, na hatimaye Bwana Mungu Kwa kuwa Yeye ni wa haki,Mungu alisimama kwenye haki, hakuitakabali sadaka ya Kaini. Lakini ebu jiangalie leo, katika eneo hili la matoleo, Je ni kweli unamtolea Mungu sawa sawa na imani yote na kuitii sauti yake? Au unatoa kwa sababu wakati wa sadaka imefika?

Lipo la kujifunza hapo; ikiwa Bwana aliweza kuikataa sadaka ya Habili anaweza pia kuikataa sadaka ya mmoja wetu leo, sababu Mungu ni yule yule jana, leo na hata milele. Kama mmoja atamtolea sadaka Mungu kama alivyomtolea Kaini basi ni dhahiri sadaka yake itakataliwa. Sadaka yafaa itolewe kwanza kwa imani, moyo ukihusika. Lakini pili sadaka itolewe sawa sawa na msukumo wa Roho mtakatifu ndani yako.

Wasiliana nami ikiwa umebarikiwa nifahamishe +255 683 877 900

What’s app ni +255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla

UBARIKIWE.

コメント


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page