top of page

KUTII NI BORA KULIKO DHABIHU.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Kumtolea Bwana ni kwema sana,lakini kuna kosa maana kama hakuna utii,hali hii inaonesha kwamba Bwana hapendezwi na wingi,au unono wa dhabihu kama utii umekosekana. Kipimo chema cha matoleo si wingi wa sadaka,au ukubwa wa sadaka,bali ni utii. Kumbe kuitii sauti yake,na maelekezo / taratibu zake ndio jambo la msingi sana. Ni vyema utambue kwamba, sadaka yako inapimwa katika kipengele cha utii wa Neno la Mungu. Ni vyema usitoe chochote kama utii haupo,kwa maana ukitoa kwa moyo wa ukaidi,ujue sadaka yako ni bure,wala haitakuwa na majibu. Wewe ni mmoja kati ya watu watoaji,ni vyema ukajifunza mambo haya kwa kina ili kusudi usije ukawa unapoteza huku ukifikiri unapata.

Suala la utoaji ni suala nyeti sana,na halina budi kufundishwa kwa waamini mara kwa mara,kwa maana mtu anaweza akatazamia apokee baraka wakati wa matoleo yake,badala yake akapokea laana. Mara nyingi tumekuwa tukitoa dhabihu zetu lakini mioyo yetu imefarakana na Bwana. Tangu zamani,historia inaonesha kwamba Mungu mwenyewe alizikataa sadaka za waovu,lakini pamoja na kuwakataa waovu wenyewe ( Isaya 1:11-17,Zab.51:16-17,Amosi 5:21-24). Hii ni kuonesha kwamba Bwana hafurahii na uovu hata kidogo. Biblia inarekodi kukataliwa kwa sadaka ya Kaini kama kwa sababu ya kukosa kutii. Ibada ilikuwa ni moja tu,lakini ndani ya ibada hiyo hiyo mmoja akakubaliwa pamoja na sadaka yake na mwingine akakataliwa pamoja na sadaka yake! ( Mwanzo 4:1-7)

Hapo ni vyema ukajifunza tena,kwamba si wote ndani ya ibada ya matoleo wanaweza wakakubaliwa na Bwana, ikiwa kama suala la utii likipimwa. Hata leo,wapo watoaji wanaotoa ndani ya maelekezo ya Bwana na hatimaye hukubaliwa,lakini pia lipo kundi kubwa la watoaji wanaojitahidi kutoa kingi nje ya maelekezo ya Bwana, na hatimaye hawakubaliwi ingawa wao wametoa mengi zaidi. Kumbuka,maneno haya“Utii” na “dhabihu” yote haya ni mambo ya rohoni/yanayohusisha moyo wa mtu,kwa maana palipo na hazina yako ilipo ndipo palipo na moyo wako.

  1. Kutii huja kwa kusikia.

Kuna “kusikiliza” na “kusikia” kusikia kunahusisha na kuelewa kile kinacholengwa,ili ukifanyie kazi. Kwa lugha nyingine kusikia kunahusisha na kutenda. Hata hivyo,mtu aweza kusikia lakini asitii!!! Lakini kile ambacho Bwana anataka kwako,ni wewe usikie kwanza,kisha ndipo uchukue hatua ya kutii. Tunajifunza kwa Sauli,mtu ambaye hakuweza kutii kile alichoambiwa,na matokeo yake,Sauli alidhani kuwa Bwana atapokea sadaka zake huku akiwa si mtii wa sauti ya Bwana. Biblia inasema;“Naye Samweli akasema,je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihuSawasawa na kuitii sauti ya BWANA?Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu,Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.” 1 Samweli 15:22

Bwana alihakikisha Sauli anaambiwa neno lake. Na ndivyo,hata sasa Bwana anahakikisha usikie neno lake,ili kusudi usije ukapata laana katika utoaji wako badala ya baraka. Ni ukweli usiopingika kwamba, Sauli alimwasi Bwana, na kwa sababu hiyo anajaribu kumtolea Bwana matoleo yaliyonona akidhani Bwana atalidhia sadaka zinazotoka kwenye moyo wake wa kuasi. Sauli wa leo wapo wengi wenye kuleta mapesa na matoleo makubwa makubwa wakijaribu kuficha dhambi zao katika matoleo!

Wakidhani kuwa Bwana atayapokea matoleo yao. Watu wa namna hii,ni kana kwamba wanajaribu kumdhihaki Mungu ambaye hadiakiwi,lakini ni watu wanaomjaribu mtumishi wa Mungu/mchungaji. Na bahati mbaya,wapo watumishi ambao hupokea matoleo ya namna hii hali wakijua uovu unaofanyika na watu hao,nao hawasemi kitu kwa maana wamepokea tayari.

Ebu fikiria kama Samweli angelipokea sadaka za Sauli aliye mwovu na si mtii wa sauti ya Bwana, hivi ingelikuwaje? Hivi Samweli angelikuwa na sauti juu ya Sauli huku akiwa amepokea matoleo? Bila shaka kama Samweli angelipokea dhabihu za Sauli, ingembidi awe mpole,na hatimaye utumishi wake ungeingia dosari. Ni vyema kumsikiliza Mungu, akiwa amezikataa dhabihu basi na iwe hivyo. Lakini wengi hufanya kinyume na uelewa,hivyo watu wafundishwe somo la utoaji ili waelewe vyema.Mtoaji ajifunze,kumlingana Mungu katika haki ndio bora zaidi ya dhabihu.

  1. Bwana anataka nini kwako?

“Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!“ Mika 6:8. Ukisoma andiko hili mstari wa 6 & 7 utagundua alikuwa Bwana akizungumza na mtoaji. Na hapa mstari wa 8, anajaribu kukupa dawa ya kuponya tatizo la utoaji. Kile anachotaka kwako ni “uweze kutenda haki” yaani uepukane na uovu,uwe mtu uliyemlingana Bwana kabla ya kutoa kwako.

Kama ukiona hujapatana na mshtaki wako,basi patana naye kwanza,hivyo ndivyo afanyavyo mtu wa haki. Lakini pia “rehema na unyenyekevu ” unahitajika kwako. Hapa,Bwana ametoa nafasi ya bure ya toba,utengeneze na yeye,lakini pia ujishushe kwa kunyenyekea. Kitendo cha “unyenyekevu” ni kitendo cha kutembea katika utii wa sauti ya Bwana,ndicho Bwana anachokitaka kwako.(kumbuka; Vile utakavyokuwa mtii wa Neno analofundisha mchungaji wako,ni sawa kabisa na kuitii sauti ya Bwana).

Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900

Na.Mch. G.Madumla

Whatsapp namba +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Kommentare


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page