NGUVU YA SADAKA ~ 01
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 20, 2017
- 4 min read

Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi;
Mungu yeye mwenyewe ni mtoaji mzuri,kuonesha kwamba utoaji ni asili yake kwa maana alimtoa mwanaye pekee kama sadaka/dhabihu kwa ajili yetu (Yoh.3:16).Hii yote anatufundisha kwamba Yeye ni mtoaji mzuri. Biblia inasema “Mungu aliupenda ulimwengu,hata akatoa” Neno “kupenda” ni neno muhimu sana katika utoaji wa matoleo yako. Yeye Mungu ameweka mfano kwetu,kwamba suala zima la matoleo linahitaji “kupenda moyoni” kwanza ili uweze kutoa kilicho bora. Kwa maana kila unachotoa ni lazima kianzie moyoni mwako,yaani moyo wako lazima uhusike kama alivyofanya Bwana Mungu.
Hatahivyo,hakuna sadaka kubwa kama sadaka ya Yesu Kristo pale msalabani yeye mwenyewe alifaanyika Mwana-Kondoo azichukuaye dhambi za ulimwengu (Yoh.1:29).Yeye ndio sadaka ya agano jipya iliyolipwa kwa ajili ya sadaka zote na kwa watu wote kwa maana adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake (Isaya 53:5)
Hapo zamani suala la matoleo lilikuwa ndani ya sheria kwa kuwataka watu watoe sawa sawa na sheria isemayo. Walawi 1:1-3
Lakini hata hivyo sheria iliwataka watoaji wa sadaka au dhabihu watoe kile kilichonona ndio maana andiko hilo hilo limeandikwa“...atatoa ng’ombe mume mkamilifu...” Mpaka biblia imeweka mkazo mkubwa wa namna hii,ni fika Mungu alikuwa akiwajua watu wake kwamba wanatoaka vitu vinyonge vinyonge,kwa kuliona hili,Mungu akawaagiza watoe vile vya kupendeza. Shida ya kutoa vinyonge ilikuwepo tangu zamani na Mungu aliiona shida hii,akaona awawekee sheria ya utoaji. Hivyo ni vyema tukaangazia kwenye maeneo yafuatayo kama sehemu ya fundisho hili;
Nini maana ya sadaka
Aina ya sadaka
01. Sadaka ni nini?.
Neno “ sadaka” Kwa Wayahudi sadaka huitwa “ minchah” (kiingereza huitwa offering) neno hili la Kiyahudi linatoa maana nzuri ya neno sadaka, hata neno hilo limeweza kutofautisha kati ya sadaka na dhabihu (“zebah” ni dhabihu katika lugha ya kiyahudi,katika kiingereza ni sacrifice) .Tofauti hiyo inaeleza kwamba sadaka ( minchah),ni matoleo kwa Bwana yasiyohusisha damu,ambapo dhabihu ni matoleo kwa Bwana yanayohusisha damu.Hivyo; “ Sadaka ni kitu cha thamani kinachotolewa kwa Bwana MUNGU bila kuhakiki matumizi yake.”
Sadaka – agano la kale;
“Kwa nini sadaka?’‘ Tangu mwanzo tunaona wale waliomwendea Mungu hawakwenda mikono mitupu bali walibeba dhabihu nao wakamtolea Mungu. Habari za Kaini na Habili waliojihudhurisha mbele za Mungu,walikwenda na sadaka zao. Ingawa mmoja alikubaliwa Habili na kaka yake hakukubaliwa. Lakini si hivyo tu,sadaka imeamriwa na Mungu tutoe mbele zake.(Kutoka 25:2). Katika biblia kwa mara ya kwanza utoaji unatajwa katika ibada iliyofanyika nyumbani kwa mzee Adamu. Hii ndio ibada ya kwanza kabisa ya matoleo. Katika ibada hii,tunaweza kujifunza kwamba;
Sadaka zilikuwa na utaratibu wa kuandaa na kutoa
Sadaka zilitolewa kwa Mungu moja kwa moja
Mungu anaweza kukataa sadaka,pamoja na mtoa sadaka kumkataa
Mtoaji anaweza kughadhibika katika utoaji wake,
Watoaji wanatofautiana kiroho (Kaini alitofautiana na Habiri mwenye haki)
Hata watenda dhambi nao wanaweza kumtolea Bwana sadaka,lakini wanapaswa kumgeukia Mungu.
Sadaka imebeba maisha ya mtu/mtoaji (Inaweza ikawa lango la baraka au laana)
n.k
02.Aina za matoleo ;
Kwa mujibu wa agano la kale,mahali tunapopata picha ya mambo yote tuliyapatayo katika agano jipya,kuna aina mbali mbali za matoleo.Kuna matoleo kama vile;
Sadaka za kuteketezwa (Walawi 1:1-7)
Sadaka za nafaka (Walawi 2:1-16)
Sadaka za ushirika (Walawi 3:1-17)
Sadaka za dhambi ( Walawi 4:1-5)
Sadaka za makosa (Walawi 5:14-)
Hata hivyo,sadaka nyingine leo hazina matunda kwa maana hatupo tena chini ya sheria. Lakini kuna sadaka ambazo ni muhimu kujifunza ili upate kuzielewa kwamba zimetokea wapi,na ni nini faida yake,ni vipi leo tunavyoweza kutoa. Katika sadaka hizo,nimeonelea nikuandikie chache zifuatazo;
Malimbuko.
Sadaka ya kawaida.( ile tunayoitowa mara nyingi wakati wa ibada zetu)
Mbegu.
Zaka/fungu la kumi
Sadaka ya nadhili
Sadaka ya shukrani.
Sadaka ya kinabii
Sadaka ya injili
Sadaka kwa wahitaji ( Mfano ; wajane na yatima)
i) Sadaka ya malimbuko.
Sadaka za malimbuko ni sadaka za wazao wa kwanza,au matunda ya kwanza( first fruit). Mfano unapokuwa ni mfugaji,basi sadaka ya malimbuko ni ya wale wanyama wa kwanza kwanza (wazaliwa wa kwanza wa wanyama)“ Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao waume utanipa mimi.” Kutoka 22:29
Sadaka ya malimbuko ina nguvu sana,kwa sababu ikiwa kama utatoa kwa imani na kupokelewa kwa imani kisha mchungaji akaipokea kwa maombi basi uwe na uhakika kile atakachokitamka mchungaji kitakuwa hivyo. Mfano mchungaji akitamka neno la ulinzi na kuzalisha zaidi juu ya malimbuko yako,basi itakuwa hivyo. Ikiwa wewe ni mfanyakazi,basi sadaka yako ya malimbuko itakuwa ni mshahara wako wa kwanza.Ni muhimu kumtolea Bwana zao lako la kwanza ili kusudi upate kibali juu ya kile kinachoendelea kuzaa. Mfano ni huu;
Kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa akifuga kuku yeye na mumewe. Lakini wale kuku hawakuwa na uzao wa kuongezeka,na hatimaye walikuja kufa wote kwa magonjwa. Akajikusanya kutafuta nguvu ya kuanza upya. Alipoanza upya akatoa uzao wake wa kwanza wa kuku kama sadaka ya malimbuko kanisani. Tangu siku ile mpaka leo,yule mama alikuwa na faida ya maongezeko kwa sababu Mungu alihusika kikamilifu katika ule mradi wa kuku.
Nikajifunza kitu hapo,kumbe sadaka ina nguvu sana kiasi cha kuweka ulinzi katika mradi na kufanya mradi usipolomoke. Ahaa! Sawa,basi neno la Mungu ni dhahili na kweli.Kuna siri iliyopo katika sadaka ya malimbuko,na shetani ni muongo siku zote kwa sababu anajua siri hiyo. Hivyo amejaribu kuwafunga watu wengi kiasi kwamba wasimtolee Bwana malimbuko yao. Hivi unajua kwamba yale uyapatayo yametoka kwa Bwana? Ikiwa ni hivyo basi huna budi kumtolea zao lako la kwanza kwa Mungu ili ufanikiwe zaidi…
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe pia kwa msaada zaidi na mengineyo piga kwa +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários