NDOA NI ZAIDI YA FURAHA.
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 17, 2018
- 3 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Ngoja nirudie hayo maelezo, maana naona kama hujanielewa vile, nasema “ Mungu hakuiweka ndoa kwa ajili ya kuleta furaha kwa wana ndoa, bali kwa ajili ya kukamilishana”. Nafikiri unaweza kufikiri kama nimekosea au kuchanganyikiwa maana watu wanajua ndoa imeletwa ili tufurahiane alafu leo mahali hapa unashangaa nikikuambia kinyume nyume. Lakini, ukweli ndio huo. Nikuulize swali hili “ni nani kwako ajuaye mapungufu yako kwa ukaribu,? Je ni mama au baba yako? Je ni boss wako ofisini, Je ni mtumishi mwenzako kanisani? Je ni rafiki yako? Je ni mwalimu wako, au je mwana-ndoa mwenzako?.
Ukijiuliza hivyo, utagundua kwamba anayekujua zaidi ni mwana-ndoa mwenzako. Ebu angalia, Je ni nani anijuaye vizuri mimi kama si mwezi wangu wa ndoa? Mke wangu anajua hata nimevaa nguo gani ya ndani kwa sasa, we unajua hilo, hata mama mzazi hajui. Sasa huyu mwenzi wangu wa ndoa ndie ana nafasi ya kwanza na karibu ya kuniambia makosa yangu. Unajua hilo?
Mungu hakukupatia huyo mpenzi wako wa ndoa ili ufurahi maisha ya ndoa bali akukamilishe kwenye safari ya wokovu. Kwa lugha nyepesi mwalimu wako wa karibu ni mwana- ndoa mwenzako na sio nabii, mchungaji au mwalimu wa kanisani. Hao ni watumishi wa Mungu ni muhimu sana kwako, lakini mwalimu aliye karibu nawe ni huyo mwenzako.
Mtu yeyote akishindwa kumsikia mwenzi wake, atafeli kwenye wokovu wake.
Unaweza kumuona mwenzi wako wa ndoa kisha ukamdharau kwa sababu nyingi tu, labda kwa sababu hajasoma kama wewe, labda unasema hakuridhishi, labda unamuona kana kwamba hana akili hivi, labda kwao ni maskini, labda ana ulemavu fulani hivi n. k. Mimi nakuambia leo huo ujapomdharau, lakini huyo ndiye mwalimu wako wa maisha. Ni yeye atakaye kusaidia katika uyafanyayo. Hivyo hivyo jinsi alivyo. Shida sio kwake shida ni kwako ambaye hajaamua kumshirikisha kikamilifu mambo yako. Ukijaribu kumshirikisha, yeye anaweza kukushauri jambo ambalo hata profesa asingeweza kukushauri. Utasema kivipi? Sikia, moyo wake ukilikubali jambo ulifanyalo, ujue kutakuwa na wepesi katika hilo. Na ndivyo ilivyo.
Ulikuwa ukifikiri umefunga ndoa ili upate furaha na mwenzako, lakini hilo sio lengo mama la ndoa. Bali lengo mama ni kikufanya wewe, ujirekebishe kila eneo kupitia mpenzi wako. Katika lugha ya kiingereza tunatumia neno “ santification ” yaani mchakato wa kuanguka na kusimama kwenye wokovu. Ni mchakato wa pili katika wokovu ( salvation). Mpendwa, katika ndoa ndio mahali pa kusaidiwa kumsimamisha mwana-ndoa wako au kusimamishwa na mwana-ndoa wako. Mchakato huo, una muhitaji mwenzako, ili pamoja mkamilishane.
Je unafikiri ulifunga ndoa na mtu mkamilifu? Au je unafikiri Mungu alikuletea mtu mkamilifu anayeweza kufanya yote?
Jibu ; hapana hukufunga ndoa na mtu mwenye kuweza kufanya yote, yeye uliye naye anakuhitaji wewe, na wewe unamuhitaji yeye, hivyo mnahitajiana kila mmoja kuonesha kwamba hakuna kati yenu aliyemkamilifu kwa mtazamo wa kuweza mambo yote. Ikiwa ndivyo, je huyo mwenzako amekuja kwa kufurahi tu ikiwa amekuja na mapungufu yake na wewe unayo yako lukuki,
Je hufikirii Bwana amekuletea huyo kwa lengo la kukamilishana kwenye safari yenu ya wokovu? Unaona eeeh!! 😀😀😀. Wakati fulani nilimsikia mwimbaji mmoja wa manyimbo ya kidunia ya huku kwetu yanaitwa “bongo fleva” aliimba kwamba anataka mke ila yeye akatumia neno “nataka demu” sasa anajaribu kutafuta mwanamke amtakaye akiianzia kutaja kiungo kimoja kimoja kwamba anataka mwanamke ambaye sura yake iwe kama ya mtu fulani, shingo kama ya mtu fulani, kifua chake kiwe kama cha mtu fulani, kiuno chake kiwe kama cha mtu fulani,akamalizia miguu iwe kama “ chupa ya bia”😀😀😀 hapo ndio kanimaliza kabisa,. Mwe!! ….. Sasa ebu angalia mnyambuliko wake, Maana mpaka anawaza hivyo aliona kasoro akatamani akusanye maumbile mbali mbali ya wanawake na kuyaweka pamoja awe mwanamke anayemtaka.
Hii ni dhahiri kabisa mwanamke anayemtaka hayupo duniani.!!! Na huu ndio mtazamo wa vijana wengi kwamba anataka mvulana au msichana fulani kama aliyemuona kwenye tamthilia. Hivyo, watu wanataka mguu kama wa fulani, kisha sura kama ya fulani, sasa huyo ni mtu gani mwenye viungo vya kuunga unga vya watu tofauti tofauti. Hata kama akitokea wa sampuli hiyo, ujue bado hajakamilika na hawezi kuja kwa ajili ya furaha bali kwa kukamilishana.
Biblia inasema “… Si vyema mtu huyo awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. “ Mwanzo 2:18. Maana yake Adamu aliyeumbwa alihitaji mtu atakayemkamilisha / atakayemsaidia maana kuna mambo ambayo Adamu asingeyaweza yeye mwenyewe hata kama angejitahidi. Ebu fikiria Je Adamu angeliweza kuzaa? Jibu hapana, Adamu asingeliweza alimuhitaji mwanamke mwenye tumbo la kuzaa. Na je Hawa angeliweza mambo yote yeye mwenyewe, jibu hapana asingeliweza. Hivyo ukimwangalia mwanamke ambaye ni mke anamuhitaji mumewe, naye mumewe anamuhitaji mkewe. Sio tu kwa furaha bali kukamilishana katika mambo yote hususani kwenye safari ya wokovu wokovu.
Ukihitaji maombi, na ukiwa umebarikiwa basi usisite kunipigia simu kama wengine wafanyavyo.
Namba zangu ni +255 683 877 900
What’s app ni +255 746 446 446
Ubarikiwe.
Comments