MWIMBAJI WA INJILI AMWIMBIE MWANASIASA?,
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 12, 2015
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi;
Siku za hivi karibuni tumeshuhudia waimbaji wetu wa nyimbo za injili wakiwa kwenye majukwaa ya wanasiasa wakiburudisha watu kwa kuwanadi wagombea katika nyimbo walizotunga. Hapo utakuta mwimbaji wa nyimbo za injili ameandaa wimbo wake ambao kwa kweli sio wimbo wa injili bali ni wimbo wa kumsifu mgombea wa chama fulani,kisha yeye na wanamziki wa bendi za kidunia wanaungana na kutumbuiza pamoja. Katika mtazamo wa kawaida tunaweza kujiuliza kwa nini mwanamziki wa nyimbo za injili kufanya hivyo? Je anatafuta pesa ? au anatafuta support kutoka kwao? Au ni moja ya njia ya kutafuta mashabiki?
Lakini je ni vibaya kwa mwanamziki wa nyimbo za injili kumtengenezea wimbo wa kumsifu mgombea wa siasa?
Ni vyema kufahamu kwamba Mungu tu ndiye anayestahili kusifiwa sana ( Zab.48:1,147:1,47:1-2,n.k). Mwanadamu hapaswi kusifiwa kwa nyimbo na mapambio,isipokuwa Mungu pekee. Ikiwa kama mtu yeyote atadiriki kumwinua mwanadamu atakuwa anafanya vibaya sana. Kwa waimbaji wa nyimbo za injili kushiriki katika kutunga nyimbo za kuwasifia au kuwanadi wagombea wa siasa ni makosa na ni vipaya kwa maana si kazi yao walioitiwa. Wao wameitiwa kumsifu na kumwabudu Mungu pekee,ni vyombo vya Bwana.
Kama wagombea wa chama fulani wanataka kusifiwa katika nyimbo,basi wawatafute waimbaji wengine la si waimbaji wa nyimbo za injili. Ikiwa waimbaji wa nyimbo za injili watageukia kwenye kazi isiyokuwa yao,basi wataitwa nao ni wasanii wa nyimbo za injili kwa maana kuna tofauti kati ya msanii wa nyimbo za injili na waimbaji wa nyimbo za injili. Msanii ni mtu mbunifu,anaweza akatunga na kupeleka ujumbe katika njia yake ya kibinadamu,bali mwimbaji wa nyimbo za injili ni “mtumishi wa Mungu” anayepaswa kuongozwa na Roho mtakatifu.Ukisoma elimu /masomo ya sifa na kuabudu ,utagundua kwamba waimbaji wote walipakwa mafuta kwa ajili ya kuhudumu madhabahuni tu kama vile wana wa Asafu walivyofanya huduma ya sifa. Chombo cha madhabahuni ni cha madhabahuni,iweje kitumike nje ya madhabahu ?
Nini chanzo?
01. Kushindwa kujitambua – Inavyoonekana wanamziki wengi wa nyimbo za injili hawatambui nafasi walioyokuwa nayo na ndio maana wanakubali kupelekwa pelekwa kila sehemu wakitumiwa vibaya kinyume na wito wao. Hakuna kitu kibaya kama kushindwa kujitambua. Mwimbaji wa Bwana akishindwa kujitambua haina maana hajaokoka bali ameokoka lakini ufahamu wake ni mdogo kiasi kwamba ataangamizwa kwa kukosa ufahamu sahihi. Lazima mwanamziki wa nyimbo za injili wajitambue.
02. Shule ndogo – Si wengi sana wanajifunza masomo ya mziki,masomo ya uimbaji.Kwa hiyo shule imekosekana kwa waimbaji walio wengi.Elimu ni muhimu sana katika eneo la uimbaji na upigaji wa vyombo. Hujawahi kuona mwimbaji wa injili akiimba wimbo ambao yeye mwenyewe hajui maana yake lakini ni wake,halafu hata akijua maana yake,bado hajui huo ni wimbo wa namna gani,wa sifa? au kuabudu? Kuabudu ni namna gani na kusifu ni kwa namna gani? Hayo yote yanahitaji shule!
03.Tamaa – Tamaa ya kupata fedha,kujiinua,kutunzwa n.k inawamaliza wanamziki wengi hasa barani Afrika. Utakuta mwanamziki wa nyimbo za injili hali akijua madhara yatakayomkuta endapo akifanya hayo,lakini kwa sababu ameona kuna pesa itakayopatikana basi utakuta yupo tayari kufanya maamuzi ya kutumiwa na mtu yoyote kwa lengo lolote ilimladi apewe pesa. Wengine hutumika kwa sababu anamtaka mtu mmoja kimapenzi kwa hiyo akiambiwa andika wimbo juu ya mgombea fulani,hapo yupo tayari kuandika kwa sababu za kimapenzi.
04. Utoto wa kiroho – Wanamziki wengi wa nyimbo za injili hawajakuwa kiroho kwa kuwa kwanza hawajatulia kufundishwa neno la uzima vya kutosha. Kwa hiyo wengi wamejikuta wakihama hama makanisa na kushindwa kukua vyema kiroho. Kuna waimbaji wa nyimbo za injili ambao hana baba wala mama wa kiroho wao ni wao tu,kutwa nzima ni kuangaika na makanisa wapi wakaimbe ?!!!! Sasa utakuaje kiroho mpendwa kwa staili hii? Je akitokea mtu mwenye fedha zake akikuambia kufanya kitu fulani hutakwenda? maana kuna utoto unaokusumbua,nakwambia utakwenda tu. Hivyo ni vibaya kwa mwimbaji wa Bwana kutengeneza nyimbo za kuwasifu watu wanaliopo kwenye siasa na watu wa aina yoyote ile,wa kusifiwa ni Mungu tu.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
What’s app +255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments