MWIBA – (MJUMBE WA SHETANI)
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 29, 2019
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi;
Maumivu ya “mwiba” yanatofautiana na maumivu mengine kwa maana ikiwa umejichoma mwiba na haujatolewa,basi ujue utakuuma kila siku halafu maumivu yake yanakuwa haswa pale unapojaribu kutembea ikiwa mwiba upo mguuni! Ni afadhali uumie kwa kujikata au kujichuna,kwa maana baada ya muda utapona,lakini ukiwa na mwiba usiotolewa utakuwa na maumivu ya daima. Hivyo utagundua kwamba mwiba una maumivu ya “kero” (ni maumivu madogo,lakini yapo katika hali ya uendelevu hasa kila unapokanyaga chini,ukitembea). Ukweli ni kwamba “hakuna kitu kibaya kama kupata maumivu endelevu,kwa maana inaweza kufika wakati ukachoka na hali hiyo”
Paulo mtume alikuwa ni mtu wa rohoni sana,kiasi kwamba alinyakuliwa mpaka mbinguni,akafunuliwa kwa mafunuo makubwa kiasi kwamba mafunuo hayo “hayajuzu kuyanena”. Utume wake ulikuwa ni wa ajabu mno kwa maana hakuwa miongoni mwa wale Thenashara /mitume 12 wa Yesu,lakini ndiye mtu pekee tunayewezekujifunza mengi kutoka kwake. Mtu huyu kwanza alikutana na Yesu (Matendo 9:4-5),Lakini Bwana aliendelea kumtumia kwa nguvu na uweza wa Roho mtakatifu. Ingawa alikuwa na yote hayo,lakini bado alikuwa na “mwiba” mjumbe wa shetani. Kama ilivyokuwa maumivu ya mwiba wa kawaida unapoingia mwilini,ndivyo yalivyokuwa maumivu aliyoyapata Paulo yalivyokuwa,“mwiba”ulimsumbua sana.
“Mwiba mjumbe wa shetani” ni nini hasa?
Wengi husema ni ugonjwa fulani au udhaifu fulani au mwiba wake ulikuwa ni “kukosa uwezo wa kuona vizuri” kwa maana alitokewa na Yesu kwa mwanga mkuu sana kiasi cha kupofusha macho yake (Matendo 9:3),Labda na ndio maana hata nyaraka zake ilibidi ziandikwe na Luka aliyekuwa mfuasi/mwanafunzi wake. Hayo ni mawazo na mitazamo ya wengi ambayo yanaweza kuwa kweli,lakini biblia hajiaweka wazi juu ya mwiba wa Paulo. Lakini kwa mujibu wa neno la Bwana;“Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.” 2 Wakorintho 12:7. Kwa mujibu tu wa andiko hili,inaonesha mwiba wake ulikua ni moja ya udhaifu wa mwilini aliokuwa nao ambao Mungu aliruhusu kwa makusudi ya kumnyenyekeza zaidi kwa maana alipewa mengi.
Tabia ya kawaida ya mtu mwenye utele wa kitu ni “kiburi,na kujiinua”. Lakini Mungu anajua tabia ya namna hiyo,hivyo akaachilia “mwiba”umfanye Paulo kuendelea kujishusha ingawa alikuwa na mengi. Mwiba wa Paulo hakuwa pepo au shetani,kwa maana pepo wala shetani hakuwa na nafasi kwake isipokuwa ameruhusiwa na Mungu kama kule kwa Ayubu. Mwiba amepewa jina la “mjumbe wa shetani” kwa maana kuwa yeye ndiye alitaye usumbufu wa kila aina katika miili yetu. Paulo aliomba sana kwa Bwana kwamba kimtoke kinachomsumbua,lakini haikuwa mapenzi ya Mungu kukiondoa kinachomtesa,kwa maana kwenye huo udhaifu ndipo Mungu anaonekana kwake,na ndipo Paulo apatapo nguvu ya kusonga mbele. Kwa hiyo utagundua kwamba ingawa Paulo alikuwa hautaki huo mwiba lakini bado ulimshikilia. Kwa maana hata alipokaza kumwomba Mungu, Mungu alimwambia “ Neema yangu yakutosha…” kwamba kile nilichokupa Paulo kinakutosha kabisa.
Mateso ya mwili aliyokuwa nayo,si kwa sababu alitenda dhambi fulani au laana fulani aliyokuwa nayo,bali yalikuwa ni mateso ya mwenye haki. Katika hili ni lazima ujue kutofautisha kati ya mateso ya mwili yatokanayo na dhambi na ya mtu mwenye haki,kwa sababu wengi leo huteseka kwa sababu ya dhambi na makosa yao pamoja na ujinga unaochangia kwa asilimia kubwa.Kusudi kuu la mwiba wa Paulo limeelezwa wazi kabisa,kwamba “asipate kujivuna kupita kiasi,kwa wingi wa mafunuo aliyofunuliwa” Na ndio kusudi hili hili linalosimama kwa kila mtu mwenye mwiba. Kumbuka kuwa ni rahisi kujivuna hata ukamsahau Mungu ikiwa kama huna mwiba unaokuchoma choma kila mara,na mbaya zaidi huwezi kuuondoa huo mwiba.
Je “mwiba” upo mpaka leo kwa waaminio? Au ulikuwa kwa Paulo tu?
Ili kusudi uweze kunyenyekea kwa Bwana, ni lazima upitishwe kwenye mwiba,ambao utakuchoma au kukuletea usumbufu fulani ndani yako na hapo ndipo utakapokuwa na nguvu mbele za Mungu kwa maana “uwapo dhaifu ndipo ulipo na nguvu”. Hivyo mwiba upo hata sasa kwa waaminio. Mwiba wa leo,unaweza ukawa si magonjwa na udhaifu wa kimwili,bali unaweza ikawa usumbufu wa aina yoyote ule unaolekezwa kwako moja kwa moja. Mfano hata mwana ndoa mwenzako anaweza kugeuka na kuwa mwiba,unaochoma na kuumiza kila siku. Ambapo kupitia yeye,unajikuta unamtafuta Mungu kweli kweli na kunyenyekea kwa Mungu ili ikiwezekana Bwana Mungu ambadirishe. Lakini pale unapotulia bila kumtafuta Mungu, hapo ndipo mwenzako anapanda juu na kukuchoma kwa maumivu makali. Lakini ukweli ni kwamba Mungu hajakusudia kwamba mpenzi wako wa ndoa awe mwiba kwako!! Lakini kwa sababu ya kukunyenyekeza mwiba unaweza ukaruhusiwa kwa mkeo/mumeo. Hata kwako inawezekana kuna mateso fulani uyapatayo,na umemwomba sana Bwana yatoke lakini mpaka sasa hayajatoka hali wewe ni mwenye haki,basi hapo usichoke kuomba kwa maana hapo ndipo ulipo na nguvu na mateso hayo hayana tofauti na mwiba.
Kawaida hakuna apendaye mwiba,lakini kuna wakati ni lazima ukubaliane nayo ikiwa kama ulimwomba Bwana kisha Bwana akakujibu ameachilia yeye mwenyewe. Hali hii sio ya kawaida isipokuwa kwa wale wenye vingi kwa kusudi la kuwanyenyekesha. Paulo ajapokuwa alikuwa mtume na mtumishi wa Bwana Mungu, lakini bado alikuwa ni mwanadamu ambaye katika uanadamu wake labda angeliweza kujiinua,kujisifu zaidi. Na kwa sababu ya wingi na utele wa mafunuo,mwiba kwake ulimnyenyekeza.
Kwa msaada zaidi,MAOMBI pamoja na kama umeguswa na ujumbe huu; piga sasa +255 746 446 446 What’s app ni namba hiyo hiyo
Na Mch.G.Madumla
UBARIKIWE.
コメント