MWANAMKE WA MITHALI 31~02
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 13, 2018
- 3 min read

Na mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
Kumbuka;mwanamke wa mithali 31 ni Mwanamke aliyeelezwa kwenye kitabu cha mithali 31:10-31. Kupitia mwanamke huyu tunaweza kujifunza kwake mambo mengi,na hilo ndilo lengo kuu. Leo tumekuwa na wanawake wenye tabia zisizofaa mbele za Mungu,wengine wamepokea tabia hizo kutokana na hulka,au malezi na makuzi,wengine wamepata tabia hizo mashuleni waliposoma. Hivyo utaona kumekuwa na tabia na mienendo mibaya siku hizi. Ukiliangalia jambo hili kiroho utagundua kwamba shetani yupo kazini!
Lakini ashukuriwe Mungu kwa Neno lake juu ya mwanamke aliyeandikwa kwenye mithali ya 31,mwanamke huyu si bora sana kuliko wanawake watakatifu wote bali ana kitu fulani cha kujifunza kwako wewe mwanamke. Ebu leo tujifunze wajibu mmoja wa mwanamke wa mithali 31;ambapo ninaamini ni wajibu wako pia;
01. Kuaminiwa na mumewe
“Moyo wa mumewe humwamini,Wala hatakosa kupata mapato.” Mithali 31:11
Mojawapo ya shida iliyopo kwenye ndoa tulizonazo leo ni kukosekana kwa uaminifu,utakuta kila mmoja anamshuku mwenzake kwamba si mwaminifu. Lakini ukiona mwenzi wako anakushuku/ anakuhisi hisi suala la uaminifu ndani ya ndoa yenu basi ujue yeye mwenyewe naye si mwaminifu,na inawezekana uaminifu wako pia ukawa umeshuka. Mwanamke wa mithali,yeye amekuwa tofauti kidogo katika eneo hili kwa sababu biblia inatuambia kwamba moyo wa mumewe unamuamini.
Tena,mumewe anamuamini kiundani ( kwa usiri wote),na mumewe anamtegemea akimuamini katika usalama wote. Kwa sababu hiyo,ndani ya mwanamke huyu hakuna chembe hata moja kukosekana kwa uaminifu,bali ni mkweli na mwaminifu mno ndani ya ndoa yake. Kwa lugha nyepesi ni sawa na kusema kwamba mumewe haoni sababu yoyote ya kumlaumu,hata moyo wake (mume) umeweka imani yote kwake.
Unajua suala la uaminifu ni suala la ndani sana,na siku zote ukiweza kuwa mwaminifu kwa mambo madogo madogo basi ujue utaweza kuwa mwaminifu kwa mambo makubwa. Lakini ukishindwa kuwa mwaminifu kwa mambo madogo huwezi kuwa mwaminifu kwa mambo makubwa hiyo ni kanuni ya kawaida kabisa. Ebu chukulia wewe ambaye mumeo anakuachia pesa ya wiki ya chakula,alafu badala ya kufanya manunuzi ya chakula kama mlivyokubaliana,wewe unachukua kajipesa kadogo hapo kwenye ela ya chakula na kununua kasabuni kakunukia.
Mara unatoa tena kidogo unakwenda kulipia mchezo unaocheza kwa siri ( mumeo hajui),alafu papo hapo unanyofoa ela kidogo na unampelekea mangi pale dukani maana anakudai ulichukua mafuta ya kujipaka (lotion). Alafu unapoenda kununua chakula cha wiki au mwezi unajikuta pesa imepungua sana kinyume na mlivyopanga!!! Mumeo anakuuliza “vipi,mbona naona chakula kama ni kidogo ulichonunua? Ni sawa lakini? Mbona mchele si kilo 40? Anyway..” alafu na unamjibu “ ni sawa mume wangu,mbona sawa jamani,…”
Umeona hapo? Kinachomfanya huyu mwanaume kuuliza hivyo ni kwa sababu ya kukosekana kwa uaminifu ndani ya mumewe. Mimi sijui wewe ni mwaminifu kwa mambo madogo madogo?- lakini mwanamke wa mithali Yeye ni mwaminifu kiasi kwamba mumewe ameweka imani yote kwake. Unajua ili mumeo aweze kukuamini ni lazima ujifunze kuwa mwaminifu kwanza kwa mambo madogo madogo.
Ebu fikiria tena; ukiwa mumeo amekuwa akisumbuka na wewe katika mambo ya mikopo mikopo kwamba amekukataza kabisa,na amekuambia ikiwa kama unashida ya pesa umueleze,lakini papo hapo wewe hufanyi hivyo,na umekuwa “ mwanamke kopa kopa” kila mahali unadaiwa!!!.Je kwa kufanya hivyo,Hujakosa uaminifu kwa mumeo? Je unafikiri atakuamini? Je unafikiri moyo wake utakupenda? Au je unafikiri atakupa pesa yake ukafanye manunuzi yoyote? Waweza kuona jinsi ilivyokuwa mbaya!!!
Ebu Jifunze kwa mwanamke mwenzako wa mithali ambaye alikuwa ni mwaminifu na mkweli kwa mumewe. Mume wa mwanamke wa mithali hana wasi wasi na mkewe maana anamjua vyema,hivyo mume anaweza kwenda mbali na kukaa huko,hata anaporejea mambo ni mazuri tu. Lakini wee! Kwa wengine sijui kwako,lakini kwa wengine kwanza wanapenda waume zao wasafiri ili wao wapate uhuru wa kufanya mambo yao maovu!!
Leo jambo kubwa la kujifunza ni uaminifu kwa mambo madogo madogo ili uweze kuaminiwa kwa mambo makubwa. Usiseme huwezi kuwa mwaminifu kwa mambo madogo,unaweza anza leo kwa mumeo kwa yote unayoyafanya yaliyo madogo madogo kabisa,fanya kwa uaminifu wote kisha utaiona furaha ya mumeo. Ebu angalia tena,mumeo akikupa ruhusa ya kutoka labda kwenda kusalimia ndugu zako,basi jitahidi uwe mwaminifu kwenda kweli na usipige kona kona zako! Hapo ufanyavyo hivyo kwa kuchepukia njia zako mwenyewe kutakunyima kupendwa na kuaminika. Mimi sijui kama unaelewa hiki nikisemacho hapa,chukua hatua sasa…..
ITAENDELEA…
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni +255 746 446 446.
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
留言